Chapter 10
1 Yesu
alisema "Kweli nawaambieni, yeyote yule asiyeingia katika zizi la kondoo
kwa kupitia mlangoni, bali hupenya na kuingia kwa njia nyingine, huyo ni mwizi
na mnyang`anyi.
2 Lakini
anayeingia kwa kupitia mlangoni, huyo ndiye mchungaji wa kondoo.
3 Mngoja
mlango wa zizi humfungulia, na kondoo husikia sauti yake, naye huwaita kondoo
wake kila mmoja kwa jina lake na kuwaongoza nje.
4 Akisha
watoa nje huwatangulia mbele nao kondoo humfuata, kwani wanaijua sauti yake.
5 Kondoo
hao hawawezi kumfuata mgeni, bali watamkimbia kwa sababu hawaijui sauti
yake."
6 Yesu
aliwaambia mfano huo, lakini wao hawakuelewa alichotaka kuwaambia.
7 Basi,
akasema tena, "Kweli nawaambieni, mimi ni mlango wa kondoo.
8 Wale
wengine wote waliokuja kabla yangu ni wezi na wanyang`anyi, nao kondoo
hawakuwasikiliza.
9 Mimi ni mlango. Anayeingia kwa kupitia kwangu ataokolewa;
ataingia na kutoka, na kupata malisho.
10 Mwizi huja kwa shabaha ya kuiba, kuua na kuharibu. Mimi
nimekuja mpate kuwa na uzima - uzima kamili.
11 "Mimi ni mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa
uhai wake kwa ajili ya kondoo wake.
12 Mtu wa kuajiriwa ambaye si mchungaji, na wala kondoo si
mali yake, anapoona mbwa mwitu anakuja, huwaacha kondoo na kukimbia. Kisha mbwa
mwitu huwakamata na kuwatawanya.
13 Yeye hajali kitu juu ya kondoo kwa sababu yeye ni mtu wa
mshahara tu.
14 Mimi ni mchungaji mwema. Nawajua walio wangu, nao walio
wangu wananijua mimi,
15 kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Mimi
nayatoa maisha yangu kwa ajili yao.
16 Tena ninao kondoo wengine ambao hawamo zizini humu.
Inanibidi kuwaleta hao pia, nao wataisikia sauti yangu, na kutakuwako kundi
moja na mchungaji mmoja.
17 "Baba ananipenda kwani nautoa uhai wangu ili nipate
kuupokea tena.
18 Hakuna mtu anayeninyang`anya uhai wangu; mimi na nautoa
kwa hiari yangu mwenyewe. Ninao uwezo wa kuutoa na uwezo wa kuuchukua tena.
Hivi ndivyo Baba alivyoniamuru nifanye."
19 Kukawa tena na mafarakano kati ya Wayahudi kwa sababu ya
maneno haya.
20 Wengi wao wakasema, "Ana pepo; tena ni
mwendawazimu! Ya nini kumsikiliza?"
21 Wengine wakasema, "Haya si maneno ya mwenye pepo.
Je, pepo anaweza kuyafumbua macho ya vipofu?"
22 Huko Yerusalemu kulikuwa na sikukuu ya Kutabaruku.
Wakati huo ulikuwa wa baridi.
23 Naye Yesu akawa anatembea Hekaluni katika ukumbi wa
Solomoni.
24 Basi, Wayahudi wakamzunguka, wakamwuliza,
"Utatuacha katika mashaka mpaka lini? Kama wewe ndiye Kristo, basi,
tuambie wazi."
25 Yesu akawajibu, "Nimewaambieni, lakini hamsadiki.
Kazi ninazozifanya mimi kwa jina la Baba yangu zinanishuhudia.
26 Lakini ninyi hamsadiki kwa sababu ninyi si kondoo wangu.
27 Kondoo wangu huisikia sauti yangu; mimi nawajua, nao
hunifuata.
28 Mimi nawapa uzima wa milele; nao hawatapotea milele,
wala hakuna mtu atakayeweza kuwatoa mkononi mwangu.
29 Baba yangu ambaye ndiye aliyenipa hao ni mkuu kuliko
wote, wale hakuna awezaye kuwatoa mikononi mwake Baba.
30 Mimi na
Baba, tu mmoja."
31 Basi,
Wayahudi wakachukua mawe ili wamtupie.
32 Yesu
akawaambia, "Nimewaonyesheni kazi nyingi kutoka kwa Baba. Ni ipi kati ya
hizo inayowafanya mnipige mawe?"
33
Wayahudi wakamjibu, "Hatukupigi mawe kwa ajili ya tendo jema, ila kwa
sababu ya kukufuru! Maana wajifanya kuwa Mungu hali wewe ni binadamu tu."
34 Yesu
akawajibu, "Je, haikuandikwa katika Sheria yenu: `Mimi nimesema, ninyi ni
miungu?`
35 Mungu
aliwaita miungu wale waliopewa neno lake; nasi twajua kwamba Maandiko
Matakatifu yasema ukweli daima.
36 Je,
yeye ambaye Baba alimweka wakfu na kumtuma ulimwenguni, mnamwambia:
`Unakufuru`, eti kwa sababu nilisema: `Mimi ni Mwana wa Mungu?`
37 Kama
sifanyi kazi za Baba yangu msiniamini.
38 Lakini
ikiwa ninazifanya, hata kama hamniamini, walau ziaminini hizo kazi mpate kujua
na kutambua kwamba Baba yuko ndani yangu, nami niko ndani yake."
39
Wakajaribu tena kumkamata lakini akachopoka mikononi mwao.
40 Yesu
akaenda tena ng`ambo ya mto Yordani, mahali Yohane alipokuwa akibatiza, akakaa
huko.
41 Watu
wengi walimwendea wakasema, "Yohane hakufanya ishara yoyote. Lakini yale
yote Yohane aliyosema juu ya mtu huyu ni kweli kabisa."
42 Watu
wengi mahali hapo wakamwamini.
|