Chapter 11
1 Mtu mmoja
aitwaye Lazaro, mwenyeji wa Bethania, alikuwa mgonjwa. (Kijiji cha Bethania
kilikuwa mahali walipokaa Maria na Martha, dada yake.
2 Maria
ndiye yule aliyempaka Bwana marashi na kumpangusa kwa nywele zake. Lazaro, kaka
yake, ndiye aliyekuwa mgonjwa.)
3 Basi,
hao dada wakatuma ujumbe huu kwa Yesu: "Bwana, rafiki yako ni
mgonjwa!"
4 Yesu
aliposikia hivyo akasema, "Ugonjwa huo hautaleta kifo, ila ni kwa ajili ya
kumtukuza Mungu; ameugua ili kwa njia hiyo Mwana wa Mungu atukuzwe."
5 Yesu
aliwapenda Martha, dada yake na Lazaro.
6
Alipopata habari kwamba Lazaro ni mgonjwa, Yesu aliendelea kukaa mahali hapo
alipokuwa kwa siku mbili zaidi.
7 Kisha
akawaambia wanafunzi wake, "Twendeni tena Yudea!"
8
Wanafunzi wakamwambia, "Mwalimu! Muda mfupi tu umepita tangu Wayahudi
walipotaka kukuua kwa mawe, nawe unataka kwenda huko tena?"
9 Yesu
akajibu, "Je, saa za mchana si kumi na mbili? Basi, mtu akitembea mchana
hawezi kujikwaa kwa kuwa anauona mwanga wa ulimwengu huu.
10 Lakini
mtu akitembea usiku atajikwaa kwa maana mwanga haumo ndani yake."
11 Yesu
alipomaliza kusema maneno hayo, akawaambia, "Rafiki yetu Lazaro amelala,
lakini mimi nitakwenda kumwamsha."
12
Wanafunzi wake wakamwambia, "Bwana, ikiwa amelala, basi atapona."
13 Wao
walidhani kwamba alikuwa amesema juu ya kulala usingizi, kumbe alikuwa amesema
juu ya kifo cha Lazaro.
14 Basi,
Yesu akawaambia waziwazi, "Lazaro amekufa;
15 Lakini
nafurahi kwa ajili yenu kwamba sikuwako huko, ili mpate kuamini. Haya, twendeni
kwake."
16 Thoma
(aitwaye Pacha) akawaambia wanafunzi wenzake, "Twendeni nasi tukafe pamoja
naye!"
17 Yesu
alipofika huko alikuta Lazaro amekwisha kaa kaburini kwa siku nne.
18 Kijiji
cha Bethania kilikuwa karibu na Yerusalemu umbali upatao kilomita tatu.
19
Wayahudi wengi walikuwa wamefika kwa Martha na Maria kuwafariji kwa kifo cha
kaka yao.
20 Basi,
Martha aliposikia kwamba Yesu alikuwa anakuja, akaenda kumlaki; lakini Maria
alibaki nyumbani.
21 Martha
akamwambia Yesu, "Bwana, kama ungalikuwa hapa, kaka yangu hangalikufa!
22 Lakini
najua kwamba hata sasa chochote utakachomwomba Mungu, atakupa."
23 Yesu
akamwambia, "Kaka yako atafufuka."
24 Martha
akamjibu, "Najua kwamba atafufuka wakati wa ufufuo, siku ya mwisho."
25 Yesu
akamwambia, "Mimi ndimi ufufuo na uzima. Anayeniamini mimi hata kama
anakufa, ataishi:
26 na kila
anayeishi na kuniamini, hatakufa kamwe. Je, waamini hayo?"
27 Martha
akamwambia, "Ndiyo Bwana! Naamini kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa
Mungu, yule ajaye ulimwenguni."
28 Baada
ya kusema hayo, Martha alikwenda kumwita Maria, dada yake, akamwabia faraghani,
"Mwalimu yuko hapa, anakuita."
29 Naye
aliposikia hivyo, akainuka mara, akamwendea Yesu.
30 Yesu
alikuwa hajaingia kijijini, ila alikuwa bado mahali palepale Martha alipomlaki.
31 Basi,
Wayahudi waliokuwa nyumbani pamoja na Maria wakimfariji walipomwona ameinuka na
kutoka nje ghafla, walimfuata. Walidhani alikuwa anakwenda kaburini kuomboleza.
32 Basi,
Maria alipofika mahali pale Yesu alipokuwa na kumwona, alipiga magoti,
akamwabia, "Bwana, kama ungalikuwa hapa, kaka yangu hangalikufa!"
33 Yesu
alipomwona analia, na wale Wayahudi waliokuja pamoja naye wanalia pia, alijawa
na huzuni na kufadhaika moyoni.
34 Kisha
akawauliza, "Mlimweka wapi?" Wakamwambia, "Bwana, njoo
uone."
35 Yesu
akalia machozi.
36 Basi,
Wayahudi wakasema, "Tazameni jinsi alivyompenda!"
37 Lakini
baadhi yao wakasema, "Je, huyu aliyemfumbua macho yule kipofu, hakuweza
kumfanya Lazaro asife?"
38 Basi,
Yesu akiwa amehuzunika tena moyoni, akafika kaburini. Kaburi lenyewe lilikuwa
pango, na lilikuwa limefunikwa kwa jiwe.
39 Yesu
akasema, "Ondoeni hilo jiwe!" Martha, dada yake huyo aliyekufa,
akamwambia, "Bwana, amekwishaanza kunuka; amekaa kaburini siku nne!"
40 Yesu
akamwambia, "Je, sikukwambia kwamba ukiamini utaona utukufu wa
Mungu?"
41 Basi, wakaliondoa lile jiwe. Yesu akatazama juu
mbinguni, akasema, "Nakushukuru Baba kwa kuwa wewe wanisikiliza.
42 Najua kwamba unanisikiliza daima. Lakini nimesema hayo
kwa ajili ya watu hawa waliopo hapa ili wapate kuamini kwamba wewe ndiwe
uliyenituma."
43 Alipokwisha sema hayo, akaita kwa sauti kubwa:
"Lazaro! Toka nje!"
44 Huyo aliyekuwa amekufa akatoka nje, huku amefungwa sanda
miguu na mikono, na uso wake umefunikwa. Yesu akawaambia, "Mfungueni,
mkamwache aende zake."
45 Basi, Wayahudi wengi waliokuwa wamefika kwa Maria
walipoona kitendo hicho alichokifanya Yesu wakamwamini.
46 Lakini baadhi yao walikwenda kwa Mafarisayo wakatoa
taarifa ya jambo hilo alilofanya Yesu.
47 kwa hiyo makuhani wakuu na Mafarisayo wakafanya kikao
cha Baraza kuu, wakasema, "Tufanye nini? Mtu huyu anafanya ishara nyingi
mno.
48 Tukimwacha tu watu wote watamwamini, nao Waroma watakuja
kuliharibu Hekalu letu na taifa letu!"
49 Hapo, mmoja wao aitwaye Kayafa, ambaye alikuwa Kuhani
Mkuu mwaka huo, akawaambia, "Ninyi hamjui kitu!
50 Je, hamwoni kwamba ni afadhali kwenu mtu mmoja afe kwa
ajili ya watu, kuliko taifa zima liangamizwe?"
51 Yeye hakusema hivyo kwa hiari yake mwenyewe, bali kwa
vile alikuwa Kuhani Mkuu mwaka huo, alibashiri kwamba Yesu atakufa kwa ajili ya
taifa lao;
52 na wala si kwa ajili yao tu, bali pia apate kuwaleta
pamoja watoto wa Mungu waliotawanyika.
53 Basi, tangu siku hiyo viongozi wa Wayahudi walifanya
mipango ya kumwua Yesu.
54 Kwa hiyo, Yesu hakutembea tena hadharani kati ya
Wayahudi, bali alitoka hapo, akaenda mahali karibu na jangwa, katika mji uitwao
Efraimu. Akakaa huko pamoja na wanafunzi wake.
55 Sikukuu ya Wayahudi ya Pasaka ilikuwa karibu, na watu
wengi walikwenda Yerusalemu ili wajitakase kabla ya sikukuu hiyo.
56 Basi, wakawa wanamtafuta Yesu; nao walipokusanyika
pamoja Hekaluni wakaulizana, "Mwaonaje? Yaonekana kwamba haji kabisa
kwenye sikukuu, au sivyo?"
57 Makuhani wakuu na Mafarisayo walikuwa wametoa amri
kwamba mtu akijua mahali aliko Yesu awaarifu kusudi wamtie nguvuni.
|