Chapter 12
1 Siku sita kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu alifika
Bethania alikoishi Lazaro ambaye Yesu alikuwa amemfufua kutoka wafu.
2 Huko walimwandalia chakula cha jioni, naye Martha akawa
anawatumikia. Lazaro alikuwa mmoja wa wale waliokuwa mezani pamoja na Yesu.
3 Basi, Maria alichukua chupa ya marashi ya nardo safi ya
thamani kubwa, akampaka Yesu miguu na kuipangusa kwa nywele zake. Nyumba yote
ikajaa harufu ya marashi.
4 Basi, Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na wawili ambaye
ndiye atakayemsaliti Yesu, akasema,
5 "Kwa nini marashi hayo hayakuuzwa kwa fedha dinari
mia tatu, wakapewa maskini?"
6 Alisema hivyo, si kwa kuwa alijali chochote juu ya
maskini, bali kwa sababu alikuwa mweka hazina, na kwa kuwa alikuwa mwizi, mara
kwa mara aliiba kutoka katika hiyo hazina.
7 Lakini Yesu akasema, "Msimsumbue huyu mama! Mwacheni
ayaweke kwa ajili ya siku ya mazishi yangu.
8 Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini hamtakuwa nami siku
zote." ic
9 Wayahudi wengi walisikia kwamba Yesu alikuwa Bethania.
Basi, wakafika huko si tu kwa ajili ya kumwona Yesu, ila pia wapate kumwona
Lazaro ambaye Yesu alimfufua kutoka wafu.
10 Makuhani wakuu waliamua pia kumwua Lazaro,
11 Maana kwa sababu ya Lazaro Wayahudi wengi waliwaasi
viongozi wao, wakamwamini Yesu.
12 Kesho yake, kundi kubwa la watu waliokuja kwenye sikukuu
walisikia kuwa Yesu alikuwa njiani kuja Yerusalemu.
13 Basi, wakachukua matawi ya mitende, wakatoka kwenda
kumlaki; wakapaaza sauti wakisema: "Hosana! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina
la Bwana. Abarikiwe mfalme wa Israeli."
14 Yesu akampata mwana punda mmoja akapanda juu yake kama
yasemavyo Maandiko:
15 "Usiogope mji wa Sioni! Tazama, Mfalme wako anakuja, Amepanda mwana
punda."
16 Wakati
huo wanafunzi wake hawakuelewa mambo hayo, lakini Yesu alipokwisha tukuzwa,
ndipo walipokumbuka kwamba hayo yalikuwa yameandikwa juu yake, na kwamba watu
walikuwa wamemtendea hivyo.
17 Kundi
la watu wale waliokuwa pamoja naye wakati alipomwita Lazaro kutoka kaburini,
akamfufua kutoka wafu, walisema yaliyotukia.
18 Kwa
hiyo umati huo wa watu ulimlaki, maana wote walisikia kwamba Yesu alikuwa
amefanya ishara hiyo.
19 Basi, Mafarisayo wakaambiana, "Mnaona? Hatuwezi
kufanya chochote! Tazameni, ulimwengu wote unamfuata."
20 Kulikuwa na Wagiriki kadhaa miongoni mwa watu waliokuwa
wamefika Yerusalemu kuabudu wakati wa sikukuu hiyo.
21 Hao walimwendea Filipo, mwenyeji wa Bethsaida katika
Galilaya, wakasema, "Mheshimiwa, tunataka kumwona Yesu."
22 Filipo akaenda akamwambia Andrea, nao wawili wakaenda
kumwambia Yesu.
23 Yesu akawaambia, "Saa ya kutukuzwa kwa Mwana wa Mtu
imefika!
24 Kweli nawaambieni, punje ya ngano hubaki punje tu
isipokuwa ikianguka katika udongo na kufa. Kama ikifa, basi huzaa matunda
mengi.
25 Anayependa maisha yake, atayapoteza; anayeyachukia
maisha yake katika ulimwengu huu, atayaweka kwa ajili ya uzima wa milele.
26 Anayetaka kunitumikia ni lazima anifuate, hivyo kwamba
popote pale nilipo mimi ndipo na mtumishi wangu atakapokuwa. Mtu yeyote
anayenitumikia Baba yangu atampa heshima.
27 "Sasa roho yangu imefadhaika, na niseme nini? Je,
niseme: `Baba, usiruhusu saa hii inifikie`? Lakini ndiyo maana nimekuja - ili
nipite katika saa hii.
28 Baba, ulitukuze jina lako." Hapo sauti ikasema
kutoka mbinguni, "Nimelitukuza, na nitalitukuza tena."
29 Umati wa watu waliokuwa wamesimama hapo walisikia sauti
hiyo, na baadhi yao walisema, "Malaika ameongea naye!"
30 Lakini Yesu akawaambia, "Sauti hiyo haikutokea kwa
ajili yangu mimi, ila kwa ajili yenu.
31 Sasa ndio wakati wa ulimwengu huu kuhukumiwa; sasa
mtawala wa ulimwengu huu atapinduliwa.
32 Nami nitakapoinuliwa juu ya nchi nitamvuta kila mmoja
kwangu."
33 Kwa kusema hivyo alionyesha atakufa kifo gani).
34 Basi, umati huo ukamjibu, "Sisi tunaambiwa na
Sheria yetu kwamba Kristo atadumu milele. Wawezaje basi, kusema ati Mwana wa
Mtu anapaswa kuinuliwa? Huyo Mwana wa Mtu ni nani?"
35 Yesu akawaambia, "Mwanga bado uko nanyi kwa muda
mfupi. Tembeeni mngali mnao huo mwanga ili giza lisiwapate; maana atembeaye gizani
hajui aendako.
36 Basi, wakati mnao huo mwanga uaminini ili mpate kuwa
watu wa mwanga." Baada ya kusema maneno hayo, Yesu alikwenda zake na
kujificha mbali nao.
37 Ingawa Yesu alifanya miujiza hii yote mbele yao, wao
hawakumwamini.
38 Hivyo maneno aliyosema nabii Isaya yakatimia:
"Bwana, nani aliyeuamini ujumbe wetu? Na uwezo wa Bwana umedhihirishwa kwa
nani?"
39 Hivyo hawakuweza kuamini, kwani Isaya tena alisema:
40 "Mungu ameyapofusha macho yao, amezipumbaza akili
zao; wasione kwa macho yao, wasielewe kwa akili zao; wala wasinigeukie, asema
Bwana, ili nipate kuwaponya."
41 Isaya alisema maneno haya kwa sababu aliuona utukufu wa
Yesu, akasema habari zake.
42 Hata hivyo, wengi wa viongozi wa Wayahudi walimwamini
Yesu. Lakini kwa sababu ya Mafarisayo, hawakumkiri hadharani kwa kuogopa kwamba
watatengwa na sunagogi.
43 Walipendelea kusifiwa na watu kuliko kusifiwa na Mungu
44 Kisha Yesu akasema kwa sauti kubwa, "Mtu
aliyeniamini, haniamini mimi tu, ila anamwamini pia yule aliyenituma.
45 Anayeniona mimi anamwona pia yule aliyenituma.
46 Mimi ni mwanga, nami nimekuja ulimwenguni ili wote
wanaoniamini wasibaki gizani.
47 Anayeyasikia maneno yangu lakini hayashiki mimi
sitamhukumu; maana sikuja kuhukumu ulimwengu bali kuuokoa.
48 Asiyeyashika maneno yangu anaye wa kumhukumu: neno lile nililosema
ni hakimu wake siku ya mwisho.
49 Mimi sikunena kwa mamlaka yangu mwenyewe, ila Baba
aliyenituma ndiye aliyeniamuru niseme nini na niongee nini.
50 Nami najua kuwa amri yake huleta uzima wa milele. Basi,
mimi nasema tu yale Baba aliyoniagiza niyaseme."
|