Chapter 13
1 Ilikuwa kabla ya sikukuu ya Pasaka. Yesu alijua kwamba
saa yake ya kuondoka ulimwenguni na kwenda kwa Baba ilikuwa imefika. Alikuwa
amewapenda daima watu wake walioko duniani; naam, aliwapenda mpaka mwisho!
2 Basi, Yesu na wanafunzi wake walikuwa mezani kwa chakula
cha jioni. Ibilisi alikwisha mtia Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti, nia ya
kumsaliti Yesu.
3 Yesu alijua kwamba Baba alikuwa amemkabidhi kila kitu, na
kwamba alikuwa ametoka kwa Mungu na anarudi kwa Mungu.
4 Basi, Yesu aliondoka mezani, akaweka kando vazi lake,
akachukua kitambaa na kujifunga kiunoni.
5 Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwaosha
wanafunzi wake miguu na kuipangusa kwa kile kitambaa alichojifungia.
6 Basi, akamfikia Simoni Petro; naye Petro akasema,
"Bwana, wewe utaniosha miguu mimi?"
7 Yesu akamjibu, "Huelewi sasa ninachofanya lakini
utaelewa baadaye."
8 Petro akamwambia, "Wewe hutaniosha miguu
kamwe!" Yesu akamjibu, "Nisipokuosha hutakuwa na uhusiano nami
tena."
9 Simoni Petro akamwambia, "Bwana, nioshe, si miguu
tu, bali na mikono yangu na kichwa pia."
10 Yesu akamwambia, "Aliyekwisha oga hana lazima ya
kunawa isipokuwa miguu, maana amekwisha takata mwili wote. Ninyi mmetakata,
lakini si nyote."
11 Yesu alimjua yule ambaye atamsaliti, ndiyo maana
alisema: "Ninyi mmetakata, lakini si nyote.")
12 Alipokwisha waosha miguu na kuvaa tena vazi lake,
aliketi mezani, akawaambia, "Je, mmeelewa hayo niliyowatendeeni?
13 Ninyi mwaniita Mwalimu na Bwana, nanyi mwasema vyema,
kwa kuwa ndimi.
14 Basi, ikiwa mimi niliye Bwana na Mwalimu, nimewaosha
ninyi miguu, nanyi pia mnapaswa kuoshana miguu.
15 Nimewapeni mfano, ili nanyi pia mfanye kama
nilivyowafanyieni.
16 Kweli nawaambieni, mtumishi si mkuu zaidi kuliko bwana
wake, wala mtume si mkuu zaidi kuliko yule aliyemtuma.
17 Basi, ikiwa mwayajua hayo, mtakuwa na heri
mkiyatekeleza.
18 "Haya nisemayo hayawahusu ninyi nyote. Mimi nawajua
wale niliowachagua. Lakini lazima yatimie Maandiko Matakatifu yasemayo: `Yule
aliyeshiriki chakula changu amegeuka kunishambulia.`
19 Mimi nimewaambieni mambo haya sasa kabla hayajatokea,
ili yatakapotokea mpate kuamini kuwa mimi ndimi.
20 Kweli nawaambieni anayempokea yule ninayemtuma
anaponipokea mimi; na anayenipokea mimi, anampokea yule aliyenituma."
21 Alipokwisha sema hayo, Yesu alifadhaika sana rohoni,
akasema wazi, "Kweli nawaambieni, mmoja wenu atanisaliti!"
22 Wanafunzi wakatazama wasiweze kabisa kujua anasema nani.
23 Mmoja wa wanafunzi, ambaye Yesu alikuwa anampenda sana,
alikuwa ameketi karibu na Yesu.
24 Basi, Simoni Petro akamwashiria na kusema: "Mwulize
anasema juu ya nani."
25 Mwanafunzi huyo akasogea karibu zaidi na Yesu,
akamwuliza, "Bwana, ni nani?"
26 Yesu akajibu, "Yule nitakayempa kipande cha mkate
nilichochovya katika sahani, ndiye." Basi, akatwaa kipande cha mkate,
akakichovya katika sahani, akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti.
27 Yuda alipokwisha pokea kipande hicho, Shetani
akamwingia. Basi Yesu akamwambia, "Unachotaka kufanya, kifanye
haraka!"
28 Lakini hakuna hata mmoja wa wale waliokaa pale mezani
aliyefahamu kwa nini alikuwa amemwambia hivyo.
29 Kwa kuwa Yuda alikuwa na wajibu wa kuutunza mfuko wa
fedha, baadhi yao walidhani kwamba Yesu alikuwa amemwambia anunue
vilivyohitajiwa kwa sikukuu, au kwamba alikuwa amemwambia akatoe chochote kwa
maskini.
30 Basi, Yuda alipokwisha twaa kile kipande cha mkate,
akatoka nje mara. Na ilikuwa usiku.
31 Baada ya Yuda kuondoka, Yesu akasema, "Sasa Mwana
wa Mtu ametukuzwa, naye Mungu ametukuzwa ndani yake.
32 Na kama utukufu wa Mungu umefunuliwa ndani ya Mwana,
basi, naye Mungu ataudhihirisha utukufu wa Mwana ndani yake mwenyewe, na
atafanya hivyo mara.
33 "Watoto wangu, bado niko nanyi kwa muda mfupi tu.
Mtanitafuta, lakini sasa nawaambieni yale niliyowaambia viongozi wa Wayahudi:
`Niendako ninyi hamwezi kwenda!`
34 Nawapeni amri mpya: pendaneni; pendaneni kama
nilivyowapenda ninyi.
35 Mkipendana, watu wote watajua kwamba ninyi ni wanafunzi
wangu."
36 Simoni Petro akamwuliza, "Bwana, unakwenda
wapi?" Yesu akajibu, "Niendako huwezi kunifuata sasa, lakini
utanifuata baadaye."
37 Petro akamwambia "Bwana, kwa nini siwezi kukufuata sasa?
Niko tayari kufa kwa ajili yako!"
38 Yesu akajibu, "Je, uko tayari kweli kufa kwa ajili
yangu? Kweli nakwambia, kabla jogoo hajawika utanikana mara tatu!"
|