Chapter 14
1 Yesu
aliwaambia, "Msifadhaike mioyoni mwenu. Mwaminini Mungu, niaminini
na mimi pia.
2 Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; la sivyo
ningalikwisha waambieni. Sasa nakwenda kuwatayarishieni nafasi.
3 Na nikienda na kuwatayarishieni nafasi, nitarudi na
kuwachukueni kwangu, ili nanyi muwe pale nilipo mimi.
4 Mnajua njia ya kwenda huko ninakokwenda."
5 Thoma akamwuliza, "Bwana, hatujui unakokwenda,
tutawezaje basi, kuijua hiyo njia?"
6 Yesu akamjibu, "Mimi ni njia, na ukweli na uzima.
Hakuna awezaye kwenda kwa Baba ila kwa kupitia kwangu.
7 Ikiwa mnanijua mimi mnamjua na Baba yangu pia. Na tangu
sasa, mnamjua, tena mmekwisha mwona."
8 Filipo akamwambia, "Bwana, tuonyeshe Baba, nasi
tutatosheka."
9 Yesu akamwambia, "Filipo, nimekaa nanyi muda wote
huu, nawe hujanijua? Aliyekwisha niona mimi amemwona Baba. Unawezaje basi,
kusema: `Tuonyeshe Baba?`
10 Je, huamini kwamba mimi niko ndani ya Baba, naye Baba
yuko ndani yangu? Maneno ninayowaambieni nyote siyasemi kwa mamlaka yangu; Baba
aliye ndani yangu anafanya kazi yake.
11 Mnapaswa kuniamini ninaposema kwamba mimi niko ndani ya
Baba naye Baba yuko ndani yangu. Ama sivyo, aminini kwa sababu ya mambo
ninayofanya.
12 Kweli nawaambieni, anayeniamini atafanya mambo
ninayofanya mimi; naam, atafanya hata makuu zaidi, maana nakwenda kwa Baba.
13 Na chochote mtakachoomba kwa jina langu nitafanya, ili
Baba atukuzwe ndani ya Mwana.
14 Mkiniomba chochote kwa jina langu, nitawafanyieni.
15 "Mkinipenda mtazishika amri zangu.
16 Nami nitamwomba Baba naye atawapeni Msaidizi mwingine,
atakayekaa nanyi milele.
17 Yeye ni
Roho wa kweli. Ulimwengu hauwezi kumpokea kwa sababu hauwezi kumwona wala
kumjua. Lakini ninyi mnamjua kwa sababu anabaki nanyi na yu ndani yenu.
18
"Sitawaacha ninyi yatima; nitakuja tena kwenu.
19 Bado
kidogo nao ulimwengu hautaniona tena, lakini ninyi mtaniona; na kwa kuwa mimi
ni hai, nanyi pia mtakuwa hai.
20 Siku
ile itakapofika mtajua kwamba mimi niko ndani ya Baba, nanyi mko ndani yangu,
nami ndani yenu.
21
Azipokeaye amri zangu na kuzishika, yeye ndiye anipendaye. Naye anipendaye mimi
atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake."
22 Yuda
(si yule Iskarioti) akamwambia, "Bwana, itawezekanaje wewe kujidhihirisha
kwetu na si kwa ulimwengu?"
23 Yesu
akamjibu, "Mtu akinipenda atashika neno langu, na Baba yangu atampenda,
nasi tutakuja kwake na kukaa naye.
24
Asiyenipenda hashiki maneno yangu. Na neno mlilosikia si langu, bali ni lake
Baba aliyenituma.
25
"Nimewaambieni mambo haya nikiwa bado pamoja nanyi
26 lakini
Msaidizi, Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwa jina langu, atawafundisheni
kila kitu na kuwakumbusheni yote niliyowaambieni.
27 "Nawaachieni amani; nawapeni amani yangu. Siwapi
ninyi kama vile ulimwengu ufanyavyo. Msiwe na wasiwasi, wala msifadhaike.
28 Mlikwisha sikia nikiwaambieni: `Ninakwenda zangu, kisha
nitarudi tena kwenu.` Kama mngalinipenda mngalifurahi kwa sababu ninakwenda kwa
Baba, maana yeye ni mkuu kuliko mimi.
29 Nimewaambieni haya sasa kabla hayajatokea, ili
yatakapotokea mpate kuamini.
30 Sitasema nanyi tena mambo mengi, maana mtawala wa
ulimwengu huu anakuja. Kwangu mimi hawezi kitu;
31 lakini ulimwengu unapaswa kujua kwamba nampenda Baba, na
ndiyo maana nafanya kila kitu kama Baba alivyoniamuru. Simameni, tutoke
hapa!"
|