Chapter 15
1 "Mimi ni mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye
mkulima.
2 Yeye huliondoa ndani yangu kila tawi lisilozaa matunda,
na kila tawi lizaalo hulisafisha lipate kuzaa zaidi.
3 Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya ule ujumbe
niliowaambieni.
4 Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu. Tawi haliwezi
peke yake kuzaa matunda lisipokaa katika mzabibu hali kadhalika nanyi hamwezi
kuzaa matunda msipokaa ndani yangu. ic
5 "Mimi ni mzabibu, nanyi ni matawi yake. Akaaye ndani
yangu, nami ndani yake, huyo atazaa matunda mengi, maana bila mimi hamwezi
kufanya chochote.
6 Mtu yeyote asipokaa ndani yangu hutupwa nje kama tawi
litupwalo nje hata likakauka. Watu huliokota tawi la namna hiyo na kulitupa
motoni liungue.
7 Mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu,
basi, ombeni chochote mtakacho nanyi mtapewa.
8 Baba yangu hutukuzwa kama mkizaa matunda mengi na kuwa
wanafunzi wangu.
9 Mimi nimewapenda ninyi kama vile Baba alivyonipenda mimi.
Kaeni katika pendo langu.
10 Mkizishika amri zangu mtakaa katika pendo langu, kama
vile nami nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake.
11 Nimewaambieni mambo haya ili furaha yangu ikae ndani
yenu, na furaha yenu ikamilike.
12 Hii ndiyo amri yangu: pendaneni; pendaneni kama
nilivyowapenda ninyi.
13 Hakuna upendo mkuu zaidi kuliko upendo wa mtu atoaye
uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.
14 Ninyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru.
15 Ninyi siwaiti tena watumishi, maana mtumishi hajui
anachofanya bwana wake. Lakini mimi nimewaita ninyi rafiki, kwa sababu
nimewajulisha yote ambayo nimeyasikia kutoka kwa Baba yangu.
16 Ninyi hamkunichagua mimi; mimi niliwachagueni na
kuwatuma mwende mkazae matunda, matunda yadumuyo, naye Baba apate kuwapa ninyi
chochote mumwombacho kwa jina langu.
17 Basi, amri yangu kwenu ndiyo hii: pendaneni.
18 "Kama ulimwengu ukiwachukia ninyi, kumbukeni kwamba
umenichukia mimi kabla haujawachukia ninyi.
19 Kama mngalikuwa watu wa ulimwengu, ulimwengu
ungaliwapenda ninyi kama watu wake. Lakini kwa vile ninyi si wa ulimwengu, ila
mimi nimewachagueni kutoka ulimwenguni, kwa sababu hiyo ulimwengu
unawachukieni.
20 Kumbukeni niliyowaambieni: mtumishi si mkuu zaidi kuliko
bwana wake. Ikiwa wamenitesa mimi, watawatesa na ninyi pia; kama wameshika neno
langu, watalishika na lenu pia.
21 Lakini hayo yote watawatendeeni ninyi kwa sababu ya jina
langu, kwani hawamjui yeye aliyenituma.
22 Kama nisingalikuja na kusema nao wasingalikuwa na hatia;
lakini sasa hawawezi kujitetea kwamba hawana dhambi.
23 Anayenichukia mimi, anamchukia na Baba yangu pia.
24 Kama nisingalifanya kwao mambo ambayo hakuna mtu mwingine
amekwisha yafanya wasingalikuwa na hatia; lakini sasa wameona niliyoyafanya
wakinichukia mimi, wakamchukia na Baba yangu pia.
25 Na hivi ni lazima yatimie yale yaliyoandikwa katika
Sheria yao: `Wamenichukia bure!`
26 "Atakapokuja huyo Msaidizi nitakayemtuma kwenu
kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia mimi.
27 Nanyi pia mtanishuhudia kwa kuwa mmekuwa nami tangu
mwanzo.
|