Chapter 16
1 "Nimewaambieni hayo kusudi msiiache imani yenu.
2 Watu watawatenga ninyi na masunagogi yao. Tena, wakati
unakuja ambapo kila atakayewaua ninyi atadhani anamhudumia Mungu.
3 Watawatendeeni mambo hayo kwa sababu hawamjui Baba, wala
hawanijui mimi.
4 Basi, nimewaambieni mambo haya ili saa yake itakapofika
mkumbuke kwamba niliwaambieni. "Sikuwaambieni mambo haya tangu mwanzo kwa
sababu nilikuwa pamoja nanyi.
5 Lakini sasa namwendea yule aliyenituma; na hakuna hata
mmoja wenu anayeniuliza: `Unakwenda wapi?`
6 Kwa kuwa nimewaambieni mambo hayo mmejaa huzuni mioyoni
mwenu.
7 Lakini, nawaambieni ukweli: afadhali kwenu mimi niende
zangu, maana nisipokwenda Msaidizi hatakuja kwenu. Lakini nikienda, basi,
nitamtuma kwenu.
8 Naye atakapokuja atawathibitishia walimwengu kwamba
wamekosea kuhusu dhambi, uadilifu na hukumu ya Mungu.
9 Wamekosea kuhusu dhambi kwa sababu hawaniamini;
10 kuhusu uadilifu, kwa sababu naenda zangu kwa Baba, nanyi
hamtaniona tena;
11 kuhusu hukumu kwa sababu mkuu wa ulimwengu huu amekwisha
hukumiwa.
12 "Ninayo bado mengi ya kuwaambieni, ila kwa sasa
hamwezi kuyastahimili.
13 Lakini atakapokuja huyo Roho wa kweli atawaongoza kwenye
ukweli wote; maana hatasema kwa mamlaka yake mwenyewe, bali atawaambieni yote
atakayosikia, na atasema mambo yatakayokuwa yanakuja.
14 Yeye atanitukuza mimi kwa kuwa atawaambieni yale
atakayopata kutoka kwangu.
15 Vyote alivyo navyo Baba ni vyangu; ndiyo maana nimesema
kwamba huyo Roho Mtakatifu atawaambieni yale atakayopata kutoka kwangu.
16
"Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena
mtaniona!"
17 Hapo
baadhi ya wanafunzi wake wakaulizana, "Ana maana gani anapotwambia: `Bado
kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona?`
Tena anasema: `Kwa kuwa ninakwenda kwa Baba!"`
18 Basi,
wakawa wanaulizana, "Ana maana gani anaposema: `Bado kitambo kidogo?`
Hatuelewi anaongelea nini."
19 Yesu
alijua kwamba walitaka kumwuliza, basi akawaambia, "Je, mnaulizana juu ya
yale niliyosema: `Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo
kidogo tena mtaniona?`
20
Nawaambieni kweli, ninyi mtalia na kuomboleza, lakini ulimwengu utafurahi:
mtaona huzuni lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha.
21 Wakati
mama anapojifungua huona huzuni kwa sababu saa ya maumivu imefika; lakini
akisha jifungua hayakumbuki tena maumivu hayo kwa sababu ya furaha kwamba mtu
amezaliwa duniani.
22 Ninyi
pia mna huzuni sasa; lakini nitawajieni tena, nanyi mtajaa furaha mioyoni
mwenu, na furaha hiyo hakuna mtu atakayeiondoa kwenu.
23 Siku
hiyo hamtaniomba chochote. Kweli nawaambieni, chochote mtakachomwomba Baba kwa
jina langu, atawapeni.
24 Mpaka
sasa hamjaomba chochote kwa jina langu. Ombeni nanyi mtapata ili furaha yenu
ikamilike.
25 "Nimewaambieni mambo hayo kwa mafumbo. Lakini
wakati utakuja ambapo sitasema tena nanyi kwa mafumbo, bali nitawaambieni
waziwazi juu ya Baba.
26 Siku hiyo mtaomba kwa jina langu, na siwaambii kwamba
nitamwomba Baba kwa niaba yenu;
27 maana yeye mwenyewe anawapenda ninyi, kwa sababu ninyi
mmenipenda mimi na mmeamini kwamba nimetoka kwa Mungu.
28 Mimi nilitoka kwa Baba, nikaja ulimwenguni; na sasa
nauacha ulimwengu na kurudi kwa Baba."
29 Basi, wanafunzi wake wakamwambia, "Ahaa! Sasa
unasema waziwazi kabisa bila kutumia mafumbo.
30 Sasa tunajua kwamba wewe unajua kila kitu, na huna haja
ya kuulizwa maswali na mtu yeyote; kwa hiyo tunaamini kwamba umetoka kwa
Mungu."
31 Yesu akawajibu, "Je, mnaamini sasa?
32 Wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo ninyi nyote
mtatawanyika kila mtu kwake, nami nitaachwa peke yangu. Kumbe, lakini mimi siko
peke yangu, maana Baba yu pamoja nami.
33 Nimewaambieni mambo haya ili mpate kuwa na amani katika
kuungana nami. Ulimwenguni mtapata masumbuko; lakini jipeni moyo! Mimi nimeushinda
ulimwengu!"
|