Chapter 18
1 Yesu alipokwisha sema hayo, alikwenda ng`ambo ya kijito
Kedroni, pamoja na wanafunzi wake. Mahali hapo palikuwa na bustani, naye Yesu
akaingia humo pamoja na wanafunzi wake.
2 Yuda, aliyemsaliti Yesu, alipajua mahali hapo kwani mara
nyingi Yesu alikutana na wanafunzi wake huko.
3 Basi, Yuda alichukua kikosi cha askari na walinzi kutoka
kwa makuhani wakuu na Mafarisayo, akaja nao bustanini wakiwa na taa, mienge na
silaha.
4 Yesu, hali akijua yote yatakayompata, akatokea,
akawauliza, "Mnamtafuta nani?"
5 Nao wakamjibu, "Yesu wa Nazareti!" Yesu
akawaambia, "Mimi ndiye." Msaliti Yuda alikuwa amesimama hapo pamoja
nao.
6 Basi, Yesu alipowaambia: "Mimi ndiye", wakarudi
nyuma, wakaanguka chini.
7 Yesu akawauliza tena, "Mnamtafuta nani?"
Wakamjibu, "Yesu wa Nazareti!"
8 Yesu akawaambia, "Nimekwisha waambieni kwamba mimi
ndiye. Basi, kama mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao."
9 Alisema hayo ili yapate kutimia yale aliyosema:
"Wale ulionipa sikumpoteza hata mmoja.")
10 Simoni Petro alikuwa na upanga; basi, akauchomoa,
akamkata sikio la kulia mtumishi wa Kuhani Mkuu. Mtumishi huyo aliitwa Malko.
11 Basi, Yesu akamwambia Petro, "Rudisha upanga wako
alani. Je, nisinywe kikombe alichonipa Baba?"
12 Kile kikosi cha askari, mkuu wake na walinzi wa Wayahudi
walimkamata Yesu, wakamfunga
13 na kumpeleka kwanza kwa Anasi; Anasi alikuwa baba mkwe
wa Kayafa ambaye alikuwa Kuhani Mkuu mwaka huo.
14 Huyo Kayafa ndiye aliyekuwa amewashauri Wayahudi kwamba
ni afadhali mtu mmoja afe kwa ajili ya taifa.
15 Simoni Petro pamoja na mwanafunzi mwingine walimfuata
Yesu. Huyo mwanafunzi mwingine alikuwa anajulikana kwa Kuhani Mkuu, hivyo
aliingia pamoja na Yesu ndani ya ukumbi wa Kuhani Mkuu.
16 Lakini Petro alikuwa amesimama nje, karibu na mlango.
Basi, huyo mwanafunzi mwingine aliyekuwa anajulikana kwa Kuhani Mkuu alitoka
nje akasema na mjakazi, mngoja mlango, akamwingiza Petro ndani.
17 Huyo msichana mngoja mlango akamwuliza Petro, "Je,
nawe pia ni mmoja wa wanafunzi wa mtu huyu?" Petro akamwambia, "Si
mimi!"
18 Watumishi na walinzi walikuwa wamewasha moto kwa sababu
kulikuwa na baridi, wakawa wanaota moto. Naye Petro alikuwa amesimama pamoja
nao akiota moto.
19 Basi, Kuhani akamwuliza Yesu juu ya wanafunzi wake na mafundisho
yake.
20 Yesu akamjibu, "Nimesema na kila mtu daima
hadharani. Kila mara nimefundisha katika masunagogi na Hekaluni, mahali
wakutanikiapo Wayahudi wote; na wala sijasema chochote kwa siri.
21 Kwa nini waniuliza mimi? Waulize wale waliosikia nini
niliwaambia. Wao wanajua nilivyosema."
22 Alipokwisha sema hayo mlinzi mmoja aliyekuwa amesimama
hapo akampiga kofi akisema, "Je, ndivyo unavyomjibu Kuhani Mkuu?"
23 Yesu akamjibu, "Kama nimesema vibaya, onyesha huo
ubaya; lakini ikiwa nimesema vema, mbona wanipiga?"
24 Basi, Anasi akampeleka Yesu akiwa amefungwa, kwa Kuhani
Mkuu Kayafa.
25 Petro alikuwa hapo akiota moto. Basi, wakamwuliza,
"Je, nawe pia si mmoja wa wanafunzi wake?" Yeye akakana na kusema,
"Si mimi!"
26 Mmoja wa watumishi wa Kuhani Mkuu, jamaa wa yule
aliyekatwa sikio na Petro, akamwuliza, "Je, mimi sikukuona wewe bustanini
pamoja naye?"
27 Petro
akakana tena; mara jogoo akawika.
28 Basi,
walimchukua Yesu kutoka kwa Kayafa, wakampeleka ikulu. Ilikuwa alfajiri, nao
ili waweze kula Pasaka, hawakuingia ndani ya ikulu wasije wakatiwa najisi.
29 Kwa
hiyo, Pilato aliwaendea nje, akasema, "Mna mashtaka gani juu ya mtu
huyu?"
30
Wakamjibu, "Kama huyu hangalikuwa mwovu hatungalimleta kwako."
31 Pilato
akawaambia, "Haya, mchukueni ninyi wenyewe, mkamhukumu kufuatana na Sheria
yenu." Wayahudi wakamjibu, "Sisi hatuna mamlaka ya kumwua mtu
yeyote."
32
Ilifanyika hivyo yapate kutimia maneno aliyosema Yesu kuonyesha atakufa kifo
gani.)
33 Pilato
akaingia tena ndani ya ikulu, akamwita Yesu na kumwuliza: "Ati wewe ndiye
Mfalme wa Wayahudi?"
34 Yesu
akamjibu, "Je, hayo ni maneno yako au wengine wamekwambia habari
zangu?"
35 Pilato
akamjibu, "Je, ni Myahudi mimi? Taifa lako na makuhani wamekuleta kwangu.
Umefanya nini?"
36 Yesu akamjibu,
"Ufalme wangu si wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu
huu watumishi wangu wangenipigania nisitiwe mikononi mwa Wayahudi. Lakini sasa
ufalme wangu si wa hapa."
37 Hapo
Pilato akamwambia, "Basi, wewe ni Mfalme?" Yesu akajibu, "Wewe
umesema kwamba mimi ni Mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili hiyo; na kwa ajili
hiyo nimekuja ulimwenguni kuwaambia watu juu ya ukweli. Kila mtu wa ukweli
hunisikiliza."
38 Pilato
akamwambia, "Ukweli ni kitu gani?" Pilato alipokwisha sema hayo,
aliwaendea tena Wayahudi nje, akawaambia, "Mimi sioni hatia yoyote kwake.
39 Lakini,
mnayo desturi kwamba mimi niwafungulie mfungwa mmoja wakati wa Pasaka. Basi,
mwataka niwafungulieni Mfalme wa Wayahudi?"
40 Hapo
wakapiga kelele: "La! Si huyu ila Baraba!" Naye Baraba alikuwa
mnyang`anyi.
|