Chapter 20
1 Alfajiri na mapema Jumapili, kukiwa bado na giza, Maria
Magdalene alikwenda kaburini, akaliona lile jiwe limeondolewa mlangoni pa
kaburi.
2 Basi, akaenda mbio hadi kwa Petro na yule mwanafunzi
mwingine ambaye Yesu alimpenda, akawaambia, "Wamemwondoa Bwana kaburini,
na wala hatujui walikomweka."
3 Petro pamoja na yule mwanafunzi mwingine wakaenda
kaburini.
4 Wote wawili walikimbia lakini yule mwanafunzi mwingine
alikimbia mbio zaidi kuliko Petro, akatangulia kufika kaburini.
5 Alipoinama na kuchungulia ndani, aliona sanda, lakini
hakuingia ndani.
6 Simoni Petro naye akaja akimfuata, akaingia kaburini;
humo akaona sanda,
7 na kile kitambaa alichofungwa Yesu kichwani. Hicho
kitambaa hakikuwekwa pamoja na hiyo sanda, bali kilikuwa kimekunjwa na kuwekwa
mahali peke yake.
8 Kisha yule mwanafunzi mwingine aliyemtangulia kufika
kaburini, akaingia pia ndani, akaona, akaaamini.
9 Walikuwa bado hawajaelewa Maandiko Matakatifu yaliyosema
kwamba ilikuwa lazima afufuke kutoka wafu).
10 Basi, hao wanafunzi wakarudi nyumbani.
11 Maria alikuwa amesimama nje ya kaburi, akilia. Huku
akiwa bado analia, aliinama na kuchungulia kaburini,
12 akawaona malaika wawili waliovaa mavazi meupe, wameketi
pale mwili wa Yesu ulipokuwa umelazwa, mmoja kichwani na wa pili miguuni.
13 Hao malaika wakamwuliza, "Mama, kwa nini
unalia?" Naye akawaambia, "Wamemwondoa Bwana wangu, na wala sijui
walikomweka!"
14 Baada ya kusema hayo, aligeuka nyuma, akamwona Yesu
amesimama hapo, lakini asitambue ya kuwa ni Yesu.
15 Yesu akamwuliza, "Mama, kwa nini unalia? Unamtafuta
nani?" Maria, akidhani kwamba huyo ni mtunza bustani, akamwambia,
"Mheshimiwa, kama ni wewe umemwondoa, niambie ulikomweka, nami
nitamchukua."
16 Yesu
akamwambia, "Maria!" Naye Maria akageuka, akamwambia kwa Kiebrania,
"Raboni" (yaani "Mwalimu").
17 Yesu
akamwambia, "Usinishike; sijakwenda bado juu kwa Baba. Lakini nenda kwa
ndugu zangu uwaambie: nakwenda juu kwa Baba yangu na Baba yenu, Mungu wangu na
Mungu wenu."
18 Hivyo
Maria Magdalene akaenda akawapa habari wale wanafunzi kuwa amemwona Bwana, na
kwamba alikuwa amemwambia hivyo.
19 Ilikuwa
jioni ya siku hiyo ya Jumapili. Wanafunzi walikuwa wamekutana pamoja ndani ya
nyumba, na milango ilikuwa imefungwa kwa sababu waliwaogopa viongozi wa
Wayahudi. Basi, Yesu akaja, akasimama kati yao, akawaambia, "Amani
kwenu!"
20
Alipokwisha sema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi, hao
wanafunzi wakafurahi mno kumwona Bwana.
21 Yesu
akawaambia tena, "Amani kwenu! Kama vile Baba alivyonituma mimi, nami
nawatuma ninyi."
22
Alipokwisha sema hayo, akawapulizia na kuwaambia, "Pokeeni Roho Mtakatifu.
23
Mkiwasamehe watu dhambi zao, wamesamehewa; msipowaondolea, hawasamehewi."
24 Thoma
mmoja wa wale kumi na wawili (aitwaye Pacha), hakuwa pamoja nao wakati Yesu
alipokuja.
25 Basi,
wale wanafunzi wengine wakamwambia, "Tumemwona Bwana." Thoma
akawaambia, "Nisipoona mikononi mwake alama za misumari, na kutia kidole
changu katika kovu hizo, na kutia mkono wangu ubavuni mwake, sitasadiki."
26 Basi, baada
ya siku nane hao wanafunzi walikuwa tena pamoja mle ndani, na Thoma alikuwa
pamoja nao. Milango ilikuwa imefungwa, lakini Yesu akaja, akasimama kati yao,
akasema, "Amani kwenu!"
27 Kisha
akamwambia Thoma, "Lete kidole chako hapa uitazame mikono yangu; lete
mkono wako ukautie ubavuni mwangu. Usiwe na mashaka, ila amini!"
28 Thoma
akamjibu, "Bwana wangu na Mungu wangu!"
29 Yesu
akamwambia, "Je, unaamini kwa kuwa umeniona? Heri yao wale ambao
hawajaona, lakini wameamini."
30 Yesu
alifanya mbele ya wanafunzi wake ishara nyingine nyingi ambazo hazikuandikwa
katika kitabu hiki.
31 Lakini
hizi zimeandikwa ili mpate kuamini kwamba Yesu ni Kristo, Mwana wa Mungu; na
kwa kuamini mpate kuwa na uzima kwa nguvu ya jina lake.
|