Chapter 21
1 Baada ya
hayo Yesu aliwatokea tena wanafunzi wake kando ya ziwa Tiberia. Aliwatokea
hivi:
2 Simoni
Petro, Thoma (aitwaye Pacha), na Nathanieli mwenyeji wa Kana Galilaya, wana
wawili wa Zebedayo na wanafunzi wake wengine wawili, walikuwa wote pamoja.
3 Simoni Petro aliwaambia, "Nakwenda kuvua
samaki." Nao wakamwambia, "Nasi tutafuatana nawe." Basi,
wakaenda, wakapanda mashua, lakini usiku huo hawakupata chochote.
4 Kulipoanza kupambazuka, Yesu alisimama kando ya ziwa,
lakini wanafunzi hawakujua kwamba alikuwa yeye.
5 Basi, Yesu akawauliza, "Vijana, hamjapata samaki wowote
sio?" Wao wakamjibu, "La! Hatujapata kitu."
6 Yesu akawaambia, "Tupeni wavu upande wa kulia wa
mashua nanyi mtapata samaki." Basi, wakatupa wavu lakini sasa hawakuweza
kuuvuta tena kwa wingi wa samaki.
7 Hapo yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu akamwambia
Petro, "Ni Bwana!" Simoni Petro aliposikia ya kuwa ni Bwana,
akajifunga vazi lake (maana hakuwa amelivaa), akarukia majini.
8 Lakini wale wanafunzi wengine walikuja pwani kwa mashua
huku wanauvuta wavu uliojaa samaki; hawakuwa mbali na nchi kavu, ila walikuwa
yapata mita mia moja kutoka ukingoni.
9 Walipofika nchi kavu waliona moto wa makaa umewashwa na
juu yake pamewekwa samaki na mkate.
10 Yesu akawaambia, "Leteni hapa baadhi ya samaki
mliovua."
11 Basi, Simoni Petro akapanda mashuani, akavuta hadi nchi
kavu ule wavu uliokuwa umejaa samaki wakubwa mia moja na hamsini na watatu. Na
ingawa walikuwa wengi hivyo wavu haukukatika.
12 Yesu akawaambia, "Njoni mkafungue kinywa."
Hakuna hata mmoja wao aliyethubutu kumwuliza: "Wewe ni nani?" Maana
walijua alikuwa Bwana.
13 Yesu akaja, akatwaa mkate akawapa; akafanya vivyo hivyo
na wale samaki.
14 Hii ilikuwa mara ya tatu Yesu kuwatokea wanafunzi wake
baada ya kufufuka kutoka wafu.
15 Walipokwisha kula, Yesu alimwuliza Simoni Petro,
"Simoni, mwana wa Yohane! Je, wanipenda mimi zaidi kuliko hawa?" Naye
akajibu, "Naam, Bwana; wajua kwamba mimi nakupenda." Yesu akamwambia,
"Tunza wana kondoo wangu."
16 Kisha akamwambia mara ya pili, "Simoni mwana wa
Yohane! Je, wanipenda?" Petro akamjibu, "Naam, Bwana; wajua kwamba
nakupenda." Yesu akamwambia, "Tunza kondoo wangu."
17 Akamwuliza mara ya tatu, "Simoni mwana wa Yohane!
Je, wanipenda?" Hapo Petro akahuzunika kwa sababu alimwuliza mara ya tatu:
"Wanipenda?" akamwambia, "Bwana, wewe wajua yote; wewe wajua
kwamba mimi nakupenda." Yesu akamwambia, "Tunza kondoo wangu!
18 Kweli nakwambia, ulipokuwa kijana ulizoea kujifunga
mshipi na kwenda kokote ulikotaka. Lakini utakapokuwa mzee utanyosha mikono
yako, na mtu mwingine atakufunga na kukupeleka usikopenda kwenda."
19 (Kwa kusema hivyo, alionyesha jinsi Petro atakavyokufa
na kumtukuza Mungu.) Kisha akamwambia, "Nifuate."
20 Hapo Petro akageuka, akamwona yule mwanafunzi ambaye
Yesu alimpenda, anafuata (Huyu mwanafunzi ndiye yule ambaye wakati wa chakula
cha jioni, alikaa karibu sana na Yesu na kumwuliza: "Bwana ni nani
atakayekusaliti?")
21 Basi, Petro alipomwona huyo akamwuliza Yesu,
"Bwana, na huyu je?"
22 Yesu akamjibu, "Kama nataka abaki mpaka
nitakapokuja, yakuhusu nini? Wewe nifuate mimi."
23 Basi, habari hiyo ikaenea miongoni mwa wale ndugu kwamba
mwanafunzi huyo hafi. Lakini Yesu hakumwambia kwamba mwanafunzi huyo hafi, ila,
"Kama nataka abaki mpaka nitakapokuja, yakuhusu nini?"
24 Huyo ndiye yule aliyeshuhudia mambo haya na kuyaandika.
Nasi twajua kwamba aliyoyasema ni kweli.
25 Kuna mambo mengine mengi aliyofanya Yesu, ambayo kama
yangeandikwa yote, moja baada ya lingine, nadhani hata ulimwengu wenyewe
usingetosha kuviweka vitabu ambavyo vingeandikwa.
|