Chapter 2
1 Siku ya
Pentekoste ilipofika, waumini wote walikuwa wamekusanyika pamoja.
2 Ghafla,
sauti ikasikika kutoka angani; sauti iliyokuwa kama ya upepo mkali, ikajaza ile nyumba
yote walimokuwa wamekaa.
3 Kisha,
vikatokea vitu vilivyoonekana kama ndimi za moto, vikagawanyika na kutua juu ya
kila mmoja wao.
4 Wote
wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema lugha mbalimbali kadiri Roho
alivyowawezesha.
5 Na huko
Yerusalemu walikuwako Wayahudi, watu wamchao Mungu, waliotoka katika kila nchi
duniani.
6
Waliposikia sauti hiyo, kundi kubwa la watu lilikusanyika. Wote walishtuka sana
kwani kila mmoja wao aliwasikia hao waumini wakisema kwa lugha yake mwenyewe.
7
Walistaajabu na kushangaa, wakisema, "Je, hawa wote tunaowasikia wakisema
hivi, si wenyeji wa Galilaya?
8
Imekuwaje, basi, kwamba kila mmoja wetu anawasikia wakisema kwa lugha yake
mwenyewe?
9 Baadhi
yetu ni Waparthi, Wamedi na Waelami; wengine ni wenyeji wa Mesopotamia, Yudea,
Kapadokia, Ponto na Asia,
10 Frugia
na Pamfulia, Misri na sehemu za Libya karibu na Kurene; wengine wetu ni wageni
kutoka Roma,
11
Wayahudi na watu walioongokea dini ya Kiyahudi; wengine wametoka Krete na Arabia.
Sisi sote tunasikia wakisema kwa lugha zetu wenyewe mambo makuu ya Mungu."
12 Wote
walishangaa na kufadhaika huku wakiulizana, "Hii ina maana gani?"
13 Lakini
wengine wakawadhihaki wakisema, "Watu hawa wamelewa divai mpya!"
14 Lakini
Petro alisimama pamoja na wale kumi na mmoja akaanza kuwahutubia watu kwa sauti
kubwa: "Ndugu Wayahudi nanyi nyote mnaokaa hapa Yerusalemu, sikilizeni kwa
makini maneno yangu.
15 Watu
hawa hawakulewa kama mnavyodhani; mbona ni saa tatu tu asubuhi?
16 Ukweli
ni kwamba jambo hili ni lile alilosema nabii Yoeli:
17 `Katika
siku zile za mwisho, asema Bwana, nitawamiminia binadamu wote Roho wangu.
Watoto wenu, wanaume kwa wanawake, watautangaza ujumbe wangu; vijana wenu
wataona maono, na wazee wenu wataota ndoto.
18 Naam,
hata watumishi wangu, wanaume kwa wanawake, nitawamiminia Roho wangu, siku
zile, nao watautangaza ujumbe wangu.
19
Nitatenda miujiza juu angani, na ishara chini duniani; kutakuwa na damu, moto
na moshi mzito;
20 jua
litatiwa giza, na mwezi utakuwa mwekundu kama damu, kabla ya kutokea ile siku
kuu na tukufu ya Bwana.
21 Hapo,
yeyote atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa.`
22 "Wananchi wa Israeli, sikilizeni maneno haya! Yesu
wa Nazareti alikuwa mtu ambaye mamlaka yake ya kimungu yalithibitishwa kwenu
kwa miujiza, maajabu na ishara Mungu alizofanya kati yenu kwa njia yake, kama
mnavyojua.
23 Kufuatana na mpango wake mwenyewe Mungu alikwisha amua
kwamba Yesu angetiwa mikononi mwenu; nanyi mkamuua kwa kuwaachia watu wabaya
wamsulubishe.
24 Lakini Mungu alimfufua kutoka wafu akamwokoa katika
maumivu ya kifo kwa maana haingewezekana kabisa kifo kimfunge.
25 Maana Daudi alisema juu yake hivi: `Nilimwona Bwana
mbele yangu daima; yuko nami upande wangu wa kulia, na hivyo sitatikisika.
26 Kwa hiyo, moyo wangu ulifurahi; tena nilipiga vigelegele
vya furaha. Mwili wangu utakaa katika tumaini;
27 kwa kuwa hutaiacha roho yangu katika kuzimu, wala
kumruhusu mtakatifu wako aoze.
28 Umenionyesha njia za kuufikia uzima, kuwako kwako
kwanijaza furaha!`
29 "Ndugu zangu, napenda kuwaambieni waziwazi juu ya
mambo yaliyompata Daudi, babu yetu. Yeye alikufa, akazikwa, tena kaburi lake
liko papa hapa petu mpaka leo.
30 Lakini kwa vile Daudi alikuwa nabii, alijua kuwa Mungu
alimwapia kiapo kwamba atamtawaza mmoja wa uzawa wake kuwa mfalme mahali pake.
31 Daudi aliona kabla mambo yatakayofanywa na Mungu na
hivyo akasema juu ya ufufuo wa Kristo wakati aliposema: `Hakuachwa kuzimu, mwili
wake haukuoza.`
32 Basi, Mungu alimfufua huyo Yesu na sisi sote ni
mashahidi wa tukio hilo.
33 Yesu aliinuliwa juu mpaka upande wa kulia wa Mungu,
akapokea kutoka kwa Baba ile zawadi aliyoahidi yaani Roho Mtakatifu; na mnachoona
sasa na kusikia ni mmiminiko wa huyo Roho.
34 Maana Daudi mwenyewe, hakupanda mpaka mbinguni; ila yeye
alisema: `Bwana alimwambia Bwana wangu: Keti upande wangu wa kulia,
35 hadi nitakapowafanya adui zako kibao cha kukanyagia
miguu yako.`
36 "Watu wote wa Israeli wanapaswa kufahamu kwa hakika
kwamba huyo Yesu mliyemsulubisha ninyi, ndiye huyo ambaye Mungu amemfanya kuwa
Bwana na Kristo."
37 Basi, watu waliposikia hayo, walichomwa moyo,
wakawauliza Petro na wale mitume wenzake: "Ndugu zetu, tufanye nini?"
38 Petro akajibu, "Tubuni na kila mmoja wenu abatizwe
kwa jina la Yesu Kristo ili mpate kuondolewa dhambi zenu na kupokea ile zawadi
ya Roho Mtakatifu.
39 Maana, ahadi ile ilikuwa kwa ajili yenu, kwa ajili ya
watoto wenu, kwa ajili ya wote wanaokaa mbali; na kwa ajili ya kila mtu ambaye
Bwana Mungu wetu atamwita kwake."
40 Kwa maneno mengine mengi, Petro alisisitiza na
kuwahimiza watu akisema, "Jiokoeni katika kizazi hiki kiovu."
41 Wengi waliyakubali maneno yake, wakabatizwa. Watu
wapatao elfu tatu wakaongezeka katika kile kikundi siku hiyo.
42 Hawa wote waliendelea kujifunza kutoka kwa mitume, kuishi
pamoja kidugu, kumega mkate na kusali.
43 Miujiza na maajabu mengi yalifanyika kwa njia ya mitume
hata kila mtu akajawa na hofu.
44 Waumini wote waliendelea kuwa kitu kimoja na mali zao
waligawana pamoja.
45 Walikuwa wakiuza mali na vitu vyao kisha wakagawana
fedha kadiri ya mahitaji ya kila mmoja.
46 Waliendelea kukutana pamoja kila siku Hekaluni. Lakini
wakati wa kumega mkate, walikutana katika nyumba zao na wakakishiriki chakula hicho
kwa furaha na moyo mkunjufu.
47 Walimtukuza Mungu, wakapendwa na watu wote. Kila siku
Bwana aliwaongezea idadi ya watu waliokuwa wakiokolewa.
|