Chapter 3
1 Siku moja, saa tisa alasiri, Petro na Yohane walikuwa
wanakwenda Hekaluni, wakati wa sala.
2 Na pale karibu na mlango wa Hekalu uitwao "Mlango
Mzuri", palikuwa na mtu mmoja, kiwete tangu kuzaliwa. Watu walimbeba huyo
mtu kila siku na kumweka hapo ili aombe chochote kwa wale waliokuwa wakiingia
Hekaluni.
3 Alipowaona Petro na Yohane wakiingia Hekaluni, aliwaomba
wampe chochote.
4 Petro na Yohane walimkodolea macho, naye Petro
akamwambia, "Tutazame!"
5 Naye akawageukia, akitazamia kupata kitu kutoka kwao.
6 Kisha Petro akamwambia, "Sina fedha wala dhahabu
lakini kile nilicho nacho nitakupa. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti,
tembea!"
7 Halafu, akamshika mkono wa kulia, akamwinua. Papo hapo
miguu na magoti yake yakapata nguvu.
8 Akaruka, akasimama na kuanza kutembea. Halafu akaingia
pamoja nao Hekaluni, akitembea na kurukaruka huku akimtukuza Mungu.
9 Watu wote waliokuwa hapo walimwona akitembea na kumsifu
Mungu.
10 Walipomtambua kuwa ndiye yule aliyekuwa anaombaomba
karibu na ule "Mlango Mzuri" wa Hekalu, wakashangaa mno hata wasiweze
kuelewa yaliyompata.
11 Watu wote, wakiwa na mshangao mkubwa wakaanza kukimbilia
mahali palipoitwa "Ukumbi wa Solomoni," ambapo yule mtu alikuwa bado
anaandamana na Petro na Yohane.
12 Basi, Petro alipowaona watu hao akawaambia,
"Wananchi wa Israeli, kwa nini mnashangazwa na jambo hili? Mbona
mnatukodolea macho kana kwamba ni kwa nguvu zetu au utakatifu wetu sisi wenyewe
tumemfanya mtu huyu aweze kutembea?
13 Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo, Mungu wa baba zetu
amemtukuza Yesu mtumishi wake. Yeye ndiye yuleyule mliyemtia mikononi mwa wakuu
na kumkataa mbele ya Pilato hata baada ya Pilato kuamua kumwacha huru.
14 Alikuwa mtakatifu na mwema; lakini ninyi mlimkataa,
mkataka mtu mwingine aliyekuwa muuaji afunguliwe.
15 Basi, mlimuua yule ambaye ni chanzo cha uzima. Lakini
Mungu alimfufua, na sisi ni mashahidi wa tukio hilo.
16 Jina la Yesu na imani katika jina hilo ndivyo vilivyompa
nguvu mtu huyu mnayemwona na kumfahamu. Imani kwa Yesu ndiyo iliyomponya kabisa
mtu huyu kama mnavyoona nyote.
17 "Sasa ndugu zangu, nafahamu kwamba ninyi na wakuu
wenu mlitenda hayo kwa sababu ya kutojua kwenu.
18 Lakini ndivyo Mungu alivyotimiza yale aliyotangaza
zamani kwa njia ya manabii wote, kwamba ilikuwa lazima Kristo wake ateseke.
19 Basi, tubuni mkamrudie Mungu ili afute dhambi zenu.
20 Fanyeni hivyo ili Bwana awape nyakati za kuburudika
rohoni na kuwaletea yule Kristo aliyemteua ambaye ndiye Yesu.
21 Ni lazima yeye abaki huko mbinguni mpaka utakapofika
wakati wa kurekebishwa vitu vyote, kama Mungu alivyosema kwa njia ya manabii
wake watakatifu wa tangu zamani.
22 Kwa maana Mose alisema, `Bwana Mungu wenu atawapelekeeni
nabii kama mimi kutoka kati yenu ninyi wenyewe.
23 Yeyote yule ambaye hatamsikiliza nabii huyo atatengwa
mbali na watu wa Mungu na kuangamizwa.`
24 Manabii wote, kuanzia Samweli na wale waliomfuata,
walitangaza habari za mambo haya ambayo yamekuwa yakitendeka siku hizi.
25 Ahadi zile Mungu alizotoa kwa njia ya manabii ni kwa
ajili yenu; na mnashiriki lile agano Mungu alilofanya na babu zenu, kama
alivyomwambia Abrahamu: `Kwa njia ya wazawa wako, jamaa zote za dunia
zitabarikiwa.`
26 Basi, ilikuwa kwa ajili yenu kwanza kwamba Mungu
alimfufua mtumishi wake, alimtuma awabariki kwa kumfanya kila mmoja wenu
aachane kabisa na maovu yake."
|