Chapter 5
1 Mtu mmoja aitwaye Anania na mkewe Safira waliuza shamba
lao vilevile.
2 Lakini, mkewe akiwa anajua, Anania akajiwekea sehemu ya
fedha alizopata na ile sehemu nyingine akawakabidhi mitume.
3 Basi, Petro akamwuliza, "Anania, mbona Shetani
ameuingia moyo wako na kukufanya umdanganye Roho Mtakatifu kwa kujiwekea sehemu
ya fedha ulizopata kutokana na lile shamba?
4 Kabla ya kuliuza lilikuwa mali yako, na baada ya kuliuza,
bado hizo fedha zilikuwa zako uzitumie utakavyo. Kwa nini basi, uliamua moyoni
mwako kufanya jambo la namna hii? Hukumdanganya mtu; umemdanganya Mungu!"
5 Anania aliposikia hayo, akaanguka chini, akafa. Watu wote
waliosikia habari ya tukio hilo waliogopa sana.
6 Vijana wakafika wakaufunika mwili wake, wakamtoa nje,
wakamzika.
7 Baada ya muda wa saa tatu hivi, mke wake, bila kufahamu
mambo yaliyotukia, akaingia mle ndani.
8 Petro akamwambia, "Niambie! Je, kiasi hiki cha fedha
ndicho mlichopata kwa kuuza lile shamba?" Yeye akamjibu, "Naam, ni
kiasi hicho."
9 Naye Petro akamwambia, "Mbona mmekula njama
kumjaribu Roho wa Bwana? Sikiliza! Wale watu waliokwenda kumzika mume wako,
sasa wako mlangoni na watakuchukua wewe pia."
10 Mara
Safira akaanguka mbele ya miguu ya Petro, akafa. Wale vijana walipoingia,
walimkuta amekwisha kufa; hivyo wakamtoa nje, wakamzika karibu na mume wake.
11 Kanisa
lote pamoja na wote waliosikia habari ya tukio hilo, waliogopa sana.
12 Mitume
walifanya miujiza na maajabu mengi kati ya watu. Waumini walikuwa wakikutana
pamoja katika ukumbi wa Solomoni.
13 Mtu
yeyote mwingine ambaye hakuwa mwamini hakuthubutu kujiunga nao. Hata hivyo,
watu wengine wasiokuwa wa imani hiyo waliwasifu.
14 Idadi
ya watu waliomwamini Bwana, wanaume kwa wanawake, iliongezeka zaidi na zaidi.
15 Kwa
sababu hiyo, watu walikuwa wakipeleka wagonjwa barabarani na kuwalaza juu ya
vitanda na mikeka ili Petro akipita, walau kivuli chake kiwaguse baadhi yao.
16 Watu
wengi walifika kutoka katika miji ya kando kando ya Yerusalemu, wakiwaleta
wagonjwa wao na wale waliokuwa na pepo wachafu, nao wote wakaponywa.
17 Kisha,
Kuhani Mkuu na wenzake waliokuwa wa kikundi cha Masadukayo wa mahali hapo,
wakawaonea mitume wivu.
18 Basi,
wakawatia nguvuni, wakawafunga ndani ya gereza kuu.
19 Lakini
usiku malaika wa Bwana aliifungua milango ya gereza, akawatoa nje, akawaambia,
20
"Nendeni mkasimame Hekaluni na kuwaambia watu kila kitu kuhusu maisha haya
mapya."
21 Mitume
walitii, wakaingia Hekaluni asubuhi na mapema, wakaanza kufundisha. Kuhani Mkuu
na wenzake walipofika, waliita mkutano wa Baraza kuu, yaani halmashauri yote ya
wazee wa Wayahudi halafu wakawatuma watu gerezani wawalete wale mitume.
22 Lakini
hao watumishi walipofika huko hawakuwakuta mle gerezani. Hivyo walirudi,
wakatoa taarifa mkutanoni,
23
wakisema, "Tulikuta gereza limefungwa kila upande na walinzi wakilinda
milango. Lakini tulipofungua hatukumkuta mtu yeyote ndani."
24 Mkuu wa
walinzi wa Hekalu na makuhani wakuu waliposikia habari hiyo wakawa na wasiwasi,
wasijue yaliyowapata.
25 Akafika
mtu mmoja, akawaambia, "Wale watu mliowafunga gerezani, hivi sasa wamo
Hekaluni, wanawafundisha watu."
26 Hapo
mkuu wa walinzi wa Hekalu pamoja na watu wake walikwenda Hekaluni, akawaleta.
Lakini hawakuwakamata kwa kutumia nguvu, maana waliogopa kwamba watu
wangewapiga mawe.
27 Basi,
wakawapeleka, wakawasimamisha mbele ya Baraza. Kuhani Mkuu akawaambia,
28
"Tuliwakatazeni waziwazi kufundisha kwa jina la mtu huyu; sasa mmeyaeneza
mafundisho yenu pote katika Yerusalemu na mnakusudia kutuwekea lawama ya kifo
cha mtu huyo."
29 Hapo
Petro, akiwa pamoja na wale mitume wengine, akajibu, "Lazima tumtii Mungu,
na siyo binadamu.
30 Mungu
wa babu zetu alimfufua Yesu baada ya ninyi kumwua kwa kumtundika msalabani.
31 Huyu
ndiye yule aliyekwezwa na Mungu mpaka upande wake wa kulia, akawa kiongozi na
Mwokozi, ili awawezeshe watu wa Israeli watubu, wapate kusamehewa dhambi zao.
32 Sisi ni
mashahidi wa tukio hilo, naye Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wale
wanaomtii, anashuhudia pia tukio hilo."
33 Wajumbe
wote wa lile Baraza waliposikia hayo, wakawaka hasira, hata wakaamua kuwaua.
34 Lakini
Mfarisayo mmoja aitwaye Gamalieli ambaye alikuwa mwalimu wa Sheria na
aliyeheshimika sana mbele ya watu wote, alisimama mbele ya lile Baraza, akataka
wale mitume watolewe nje kwa muda mfupi.
35 Kisha
akawaambia wale wajumbe wa Baraza, "Wananchi wa Israeli, tahadhari kabla
ya kutekeleza hicho mnachotaka kuwatenda watu hawa!
36 Zamani
kidogo, kulitokea mtu mmoja jina lake Theuda, akajisema kuwa mtu wa maana na
watu karibu mia nne wakajiunga naye. Lakini aliuawa, kisha wafuasi wake wote
wakatawanyika na kikundi chake kikafa.
37 Tena,
baadaye, wakati ule wa kuhesabiwa watu, alitokea Yuda wa Galilaya. Huyu naye,
aliwavuta watu wakamfuata; lakini naye pia aliuawa, na wafuasi wake
wakatawanyika.
38 Na sasa
pia mimi nawaambieni, msiwachukulie watu hawa hatua yoyote; waacheni! Kwa
maana, ikiwa mpango huu au shughuli hii yao imeanzishwa na binadamu, itatoweka
yenyewe.
39 Lakini
kama imeanzishwa na Mungu, siyo tu kwamba hamtaweza kuwashinda, bali mtajikuta
mnapigana na Mungu." Basi, wakakubaliana naye.
40 Hivyo
wakawaita wale mitume, wakaamuru wachapwe viboko na kuwaonya wasifundishe tena
kwa jina la Yesu; kisha wakawaacha waende zao.
41 Basi,
mitume wakatoka nje ya ule mkutano wa halmashauri wakiwa wamejaa furaha, kwani
walistahili kuaibishwa kwa ajili ya jina la Yesu.
42
Wakaendelea kila siku kufundisha na kuhubiri Habari Njema ya Kristo, Hekaluni
na nyumbani mwa watu.
|