Chapter 6
1 Baadaye,
idadi ya wanafunzi ilipokuwa inazidi kuongezeka, kulitokea manung`uniko kati ya
wanafunzi waliosema Kigiriki na wale waliosema Kiebrania. Wale waliosema
Kigiriki walinung`unika kwamba wajane wao walikuwa wanasahauliwa katika ugawaji
wa mahitaji ya kila siku.
2 Kwa
hiyo, mitume kumi na wawili waliita jumuiya yote ya wanafunzi, wakasema,
"Si vizuri sisi tuache kulihubiri neno la Mungu ili tushughulikie ugawaji
wa mahitaji.
3 Hivyo,
ndugu zetu, chagueni miongoni mwenu watu saba wenye sifa njema, waliojawa na
Roho na wenye hekima; nasi tutawakabidhi jukumu hilo.
4 Sisi, lakini, tutashughulika na sala na kazi ya kuhubiri
neno la Mungu."
5 Jambo hilo likaipendeza jumuiya yote ya waumini.
Wakawachagua Stefano, mtu mwenye imani kubwa na mwenye kujawa na Roho
Mtakatifu, Filipo, Prokoro, Nikanora, Timona, Parmena na Nikolao wa Antiokia
ambaye hapo awali alikuwa ameongokea dini ya Kiyahudi.
6 Wakawaweka mbele ya mitume, nao wakawaombea na kuwawekea
mikono.
7 Neno la Mungu likazidi kuenea na idadi ya waumini huko
Yerusalemu ikaongezeka zaidi, na kundi kubwa la makuhani wakaipokea imani.
8 Mungu alimjalia Stefano neema tele, akampa nguvu nyingi
hata akawa anatenda miujiza na maajabu kati ya watu.
9 Lakini watu fulani wakatokea ili wabishane na Stefano.
Baadhi ya watu hao walikuwa wa sunagogi moja lililoitwa "Sunagogi la Watu
Huru", nao walitoka Kurene na Aleksandria; wengine walitoka Kilikia na
Asia.
10 Lakini hawakuweza kumshinda kwa sababu ya hekima yake na
kwa sababu ya yule Roho aliyeongoza maneno yake.
11 Kwa hiyo waliwahonga watu kadhaa waseme:
"Tumemsikia Stefano akisema maneno ya kumkashifu Mose na kumkashifu
Mungu."
12 Kwa namna hiyo, waliwachochea watu, wazee na walimu wa
Sheria. Basi, wakamjia Stefano, wakamkamata na kumleta mbele ya Baraza kuu.
13 Walileta Barazani mashahidi wa uongo ambao walisema,
"Mtu huyu haachi kamwe kusema maneno ya kupakashifu mahali hapa patakatifu
na Sheria ya Mose.
14 Kwa maana tulikwisha msikia akisema eti huyo Yesu wa
Nazareti atapaharibu kabisa mahali hapa na kufutilia mbali desturi zile
tulizopokea kutoka kwa Mose."
15 Wote waliokuwa katika kile kikao cha Baraza walimkodolea
macho Stefano, wakauona uso wake umekuwa kama wa malaika.
|