Chapter 7
1 Basi, Kuhani Mkuu akamwuliza, "Je, mambo haya ni
kweli?"
2 Naye Stefano akasema, "Ndugu zangu na akina baba,
nisikilizeni! Mungu alimtokea baba yetu Abrahamu alipokuwa kule Mesopotamia
kabla hajaenda kukaa kule Harani.
3 Mungu alimwambia: `Ondoka katika nchi yako; waache watu
wa ukoo wako; nenda katika nchi nitakayokuonyesha!`
4 Kwa hivyo, Abrahamu alihama nchi ya Kaldayo, akaenda
kukaa Harani. Baada ya kifo cha baba yake, Mungu alimtoa tena Harani akaja
kukaa katika nchi hii mnayokaa sasa.
5 Mungu hakumpa hata sehemu moja ya nchi hii iwe mali yake;
hata hivyo, alimwahidia kumpa nchi hii iwe yake na ya wazawa wake, ingawaje
wakati huu hakuwa na mtoto.
6 Mungu alimwambia hivi: `Wazao wako watapelekwa katika
nchi inayotawaliwa na watu wengine, na huko watafanywa watumwa na kutendewa
vibaya kwa muda wa miaka mia nne.
7 Lakini mimi nitalihukumu taifa hilo litakalowafanya
watumwa. Kisha nitawatoa katika nchi hiyo ili waje kuniabudu mahali hapa.`
8 Halafu Mungu aliifanya tohara iwe ishara ya agano. Hivyo,
Abrahamu alimtahiri mtoto wake Isaka, siku ya nane baada ya kuzaliwa. Na Isaka,
vivyo hivyo, alimtahiri Yakobo. Naye Yakobo aliwatendea wale mababu kumi na
wawili vivyo hivyo.
9 "Wale mababu walimwonea wivu Yosefu, wakamuuza
utumwani Misri. Lakini Mungu alikuwa pamoja naye,
10 akamwokoa katika taabu zake zote. Mungu alimjalia
fadhili na hekima mbele ya Farao, mfalme wa Misri, hata Farao akamweka awe mkuu
wa ile nchi na nyumba ya kifalme.
11 Kisha, kulizuka njaa kubwa katika nchi yote ya Misri na
Kanaani, ikasababisha dhiki kubwa. Babu zetu hawakuweza kupata chakula
chochote.
12 Basi, Yakobo alipopata habari kwamba huko Misri kulikuwa
na nafaka, aliwatuma watoto wake, yaani babu zetu, waende huko Misri mara ya
kwanza.
13 Katika safari yao ya pili, Yosefu alijitambulisha kwa
ndugu zake, na Farao akaifahamu jamaa ya Yosefu.
14 Yosefu alituma ujumbe kwa baba yake na jamaa yote, jumla
watu sabini na tano, waje Misri.
15 Hivyo, Yakobo alikwenda Misri ambako yeye na babu zetu
wengine walikufa.
16 Miili yao ililetwa mpaka Shekemu, ikazikwa katika kaburi
Abrahamu alilonunua kutoka kwa kabila la Hamori kwa kiasi fulani cha fedha.
17 "Wakati ulipotimia Mungu aitimize ahadi aliyompa
Abrahamu, idadi ya wale watu kule Misri ilikwisha ongezeka na kuwa kubwa zaidi.
18 Mwishowe, mfalme mmoja ambaye hakumtambua Yosefu alianza
kutawala huko Misri.
19 Alilifanyia taifa letu ukatili, akawatendea vibaya babu
zetu kwa kuwalazimisha waweke nje watoto wao wachanga ili wafe.
20 Mose alizaliwa wakati huo. Alikuwa mtoto mzuri sana.
Alilelewa nyumbani kwa muda wa miezi mitatu,
21 na alipotolewa nje, binti wa Farao alimchukua, akamlea
kama mtoto wake.
22 Mose alifundishwa mambo yote ya hekima ya Wamisri akawa
mashuhuri kwa maneno na matendo.
23 "Alipokuwa na umri wa miaka arobaini aliamua kwenda
kuwaona ndugu zake Waisraeli.
24 Huko alimwona mmoja wao akitendewa vibaya, akaenda
kumwokoa, na kulipiza kisasi, akamuua yule Mmisri.
25 Alidhani kwamba Waisraeli wenzake wangeelewa kwamba
Mungu angemtumia yeye kuwakomboa, lakini hawakuelewa hivyo.)
26 Kesho yake, aliwaona Waisraeli wawili wakipigana,
akajaribu kuwapatanisha, akisema: `Ninyi ni ndugu; kwa nini basi, kutendeana
vibaya ninyi kwa ninyi?`
27 Yule aliyekuwa anampiga mwenzake alimsukuma Mose kando
akisema: `Ni nani aliyekuweka wewe kuwa kiongozi na mwamuzi wa watu?
28 Je, unataka kuniua kama ulivyomuua yule Mmisri jana?`
29 Baada ya kusikia hayo Mose alikimbia, akaenda kukaa
katika nchi ya Midiani na huko akapata watoto wawili.
30 "Miaka arobaini ilipotimia, malaika wa Bwana
alimtokea Mose katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto kule jangwani karibu na
mlima Sinai.
31 Mose alistaajabu sana kuona jambo hilo hata akasogea
karibu ili achungulie; lakini alisikia sauti ya Bwana:
32 `Mimi ni Mungu wa baba zako, Mungu wa Abrahamu, Isaka na
Yakobo!` Mose akatetemeka kwa hofu na wala hakuthubutu kutazama zaidi.
33 Bwana akamwambia: `Vua viatu vyako maana hapa
unaposimama ni mahali patakatifu.
34 Nimeyaona mabaya wanayotendewa watu wangu kule Misri.
Nimesikia kilio chao, nami nimekuja kuwaokoa. Basi sasa, nitakutuma Misri.`
35 "Huyu Mose ndiye yule watu wa Israeli waliyemkataa
waliposema: `Ni nani aliyekuweka wewe kuwa kiongozi na mwamuzi wetu?` Kwa njia
ya yule malaika aliyemtokea katika kichaka kilichokuwa kinawaka moto, Mungu
alimtuma Mose huyo awe kiongozi na mkombozi.
36 Ndiye aliyewaongoza wale watu watoke Misri kwa kufanya
miujiza na maajabu katika nchi ya Misri, katika bahari ya Shamu na jangwani kwa
muda wa miaka arobaini.
37 Mose ndiye aliyewaambia watu wa Israeli: `Mungu
atawateulieni nabii kama mimi kutoka katika ndugu zenu ninyi wenyewe.`
38 Wakati watu wa Israeli walipokutana pamoja kule
jangwani, Mose ndiye aliyekuwako huko pamoja nao. Alikuwa huko pamoja na babu
zetu na yule malaika aliyeongea naye mlimani Sinai; ndiye aliyekabidhiwa yale
maneno yaletayo uzima atupe sisi.
39 "Lakini yeye ndiye babu zetu waliyemkataa kumsikiliza;
walimsukuma kando, wakatamani kurudi Misri.
40 Walimwambia Aroni: `Tutengenezee miungu itakayotuongoza
njiani, maana hatujui yaliyompata Mose huyu aliyetuongoza kutoka Misri!`
41 Hapo ndipo walipojitengenezea sanamu ya ndama,
wakaitambikia na kukifanyia sherehe kitu ambacho ni kazi ya mikono yao wenyewe.
42 Lakini Mungu aliondoka kati yao, akawaacha waabudu nyota
za anga, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha manabii: `Enyi watu wa Israeli!
Si mimi mliyenitolea dhabihu na sadaka kwa muda wa miaka arobaini kule
jangwani!
43 Ninyi mlikibeba kibanda cha mungu Moloki, na sanamu ya
nyota ya mungu wenu Refani. Sanamu mlizozifanya ndizo mlizoabudu. Kwa sababu
hiyo nitakupeleka mateka mbali kupita Babuloni!`
44 Kule jangwani babu zetu walikuwa na lile hema
lililoshuhudia kuweko kwa Mungu. Lilitengenezwa kama Mungu alivyomwambia Mose
alifanye; nakala kamili ya kile alichoonyeshwa.
45 Kisha babu zetu walilipokezana wao kwa wao mpaka wakati
wa Yoshua, walipoinyakua ile nchi kutoka kwa mataifa ambayo Mungu aliyafukuza
mbele yao. Hapo lilikaa mpaka nyakati za Daudi.
46 Daudi alipata upendeleo kwa Mungu, akamwomba Mungu ruhusa
ya kumjengea makao yeye aliye Mungu wa Yakobo.
47 Lakini Solomoni ndiye aliyemjengea Mungu nyumba.
48 "Hata hivyo, Mungu Mkuu haishi katika nyumba
zilizojengwa na binadamu; kama nabii asemavyo:
49 `Bwana asema: Mbingu ni kiti changu cha enzi na dunia ni
kiti changu cha kuwekea miguu.
50 Ni nyumba ya namna gani basi mnayoweza kunijengea, na ni
mahali gani nitakapopumzika? Vitu hivi vyote ni mimi nimevifanya, au sivyo?`
51 "Enyi wakaidi wakuu! Mioyo na masikio yenu ni kama
ya watu wa mataifa. Ninyi ni kama baba zenu. Siku zote mnampinga Roho
Mtakatifu.
52 Je, yuko nabii yeyote ambaye baba zenu hawakumtesa?
Waliwaua hao Mungu aliowatuma watangaze kuja kwake yule Mwenye Haki. Na sasa,
ninyi mmemsaliti, mkamuua.
53 Ninyi mliipokea ile Sheria iliyoletwa kwenu na Malaika,
lakini hamkuitii."
54 Wale wazee wa Baraza waliposikia hayo, walighadhibika
sana, wakamsagia meno kwa hasira.
55 Lakini Stefano akiwa amejawa na Roho Mtakatifu,
akatazama juu mbinguni, akauona utukufu wa Mungu na Yesu amekaa upande wa kulia
wa Mungu.
56 Akasema, "Tazameni! Ninaona mbingu zimefunuliwa na
Mwana wa Mtu amesimama upande wa kulia wa Mungu."
57 Hapo, watu wote katika kile kikao cha Baraza, wakapiga
kelele na kuziba masikio yao kwa mikono yao. Kisha wakamrukia wote kwa pamoja,
58 wakamtoa nje ya mji, wakampiga mawe. Wale mashahidi
wakayaweka makoti yao chini ya ulinzi wa kijana mmoja jina lake Saulo.
59 Waliendelea kumpiga mawe Stefano, huku akiwa anasali:
"Bwana Yesu, ipokee roho yangu!"
60 Akapiga magoti, akalia kwa sauti kubwa: "Bwana,
usiwalaumu kwa sababu ya dhambi hii." Baada ya kusema hivyo, akafa.
|