Chapter 12
1 Karibu wakati huohuo, mfalme Herode alianza kuwatesa
baadhi ya Wakristo.
2 Alimwua kwa upanga Yakobo ndugu yake Yohane.
3 Alipoona kuwa kitendo hiki kiliwapendeza Wayahudi,
aliendelea, akamkamata Petro. (Hiyo ilifanyika wakati wa sikukuu ya Mikate
Isiyotiwa chachu.)
4 Baada ya kutiwa nguvuni, Petro alifungwa gerezani,
akawekwa chini ya ulinzi wa vikundi vinne vya askari wannewanne. Herode
alikusudia kumtoa hadharani baada ya sikukuu ya Pasaka.
5 Basi, Petro alipokuwa gerezani, kanisa lilikuwa
linamwombea kwa Mungu kwa moyo.
6 Usiku, kabla ya siku ile ambayo Herode angemtoa Petro
hadharani, Petro alikuwa amelala kati ya askari wawili. Alikuwa amefungwa
minyororo miwili, na walinzi walikuwa wanalinda lango la gereza.
7 Ghafla, malaika wa Bwana akasimama karibu naye na mwanga
ukaangaza kile chumba cha gereza. Malaika akamgusa akisema, "Amka
upesi!" Mara ile minyororo ikaanguka kutoka katika mikono yake.
8 Malaika akamwambia, "Jifunge mshipi wako, vaa viatu
vyako." Akafanya hivyo. Kisha huyo malaika akamwambia, "Vaa koti
lako, unifuate."
9 Petro akamfuata nje lakini hakujua kama hayo yaliyofanywa
na huyo malaika yalikuwa ya kweli; alidhani alikuwa anaota ndoto.
10 Walipita kituo cha kwanza cha ulinzi na cha pili, halafu
wakafika kwenye mlango wa chuma wa kuingilia mjini. Huo mlango ukawafungukia
wenyewe, nao wakatoka nje. Wakawa wanatembea katika barabara moja na mara yule
malaika akamwacha Petro peke yake.
11 Hapo ndipo Petro alipotambua yaliyotukia, akasema,
"Sasa najua kwa hakika kwamba Bwana amemtuma malaika wake akaniokoa kutoka
katika mkono wa Herode na kutoka katika mambo yale yote watu wa Israeli
waliyotazamia."
12 Alipotambua hivyo alikwenda moja kwa moja mpaka nyumbani
kwa Maria mama yake Yohane aitwaye Marko. Humo watu wengi walikuwa
wamekusanyika wakisali.
13 Petro alibisha mlango wa nje na mtumishi mmoja msichana
aitwaye Roda, akaenda mlangoni kuitikia.
14 Huyo msichana aliitambua sauti ya Petro akafurahi mno,
hata badala ya kuufungua ule mlango, akakimbilia ndani na kuwaambia kwamba
Petro alikuwa amesimama nje mlangoni.
15 Wakamwambia yule msichana, "Una wazimu!"
Lakini yeye akasisitiza kwamba ilikuwa kweli. Nao wakamwambia, "Huyo ni
malaika wake."
16 Wakati huo Petro alikuwa anaendelea kupiga hodi.
Mwishowe walifungua mlango, wakamwona, wakashangaa.
17 Petro aliwaashiria kwa mkono wakae kimya, akawaeleza
jinsi Bwana alivyomtoa gerezani. Kisha akawaambia watoe taarifa ya jambo hilo
kwa Yakobo na wale ndugu wengine, halafu akatoka akaenda mahali pengine.
18 Kulipokucha, ulitokea wasiwasi mkubwa kati ya wale
askari kuhusu yaliyokuwa yamempata Petro.
19 Herode aliamuru ufanywe msako lakini hawakuweza kumpata.
Hivyo aliamuru wale askari wahojiwe, akatoa amri wauawe. Halafu akatoka huko
Yudea akaenda Kaisarea ambako alikaa.
20 Herode alikasirishwa
sana na watu wa Tiro na Sidoni. Lakini wao walimpelekea wajumbe. Nao wakafaulu
kwanza kumpata Blasto awe upande wao. Blasto alikuwa msimamizi mkuu wa ikulu ya
mfalme. Kisha, wakamwendea Herode wakamwomba kuwe na amani, kwa maana nchi yao
ilitegemea nchi ya mfalme kwa chakula.
21 Siku
moja iliyochaguliwa, Herode akiwa amevaa mavazi rasmi na kuketi katika kiti cha
kifalme aliwahutubia watu.
22 Wale
watu walimpigia kelele za shangwe wakisema, "Hii ni sauti ya mungu, si ya
mtu."
23 Papo
hapo malaika wa Bwana akamwangusha Herode chini kwa sababu hakumpa Mungu hizo
sifa. Akaliwa na wadudu, akafa.
24 Neno la
Mungu likazidi kuenea na kukua.
25 Baada
ya Barnaba na Saulo kutekeleza shughuli zao, walitoka tena Yerusalemu
wakamchukua Yohane aitwaye pia Marko.
|