Chapter 13
1 Katika
kanisa la Antiokia kulikuwa na watu wengine waliokuwa manabii na walimu; miongoni
mwao akiwa Barnaba, Simoni aitwaye pia Mweusi, Lukio wa Kurene, Manaeni ambaye
alikuwa amelelewa pamoja na mfalme Herode, na Saulo.
2
Walipokuwa wanafanya ibada yao kwa Bwana na kufunga, Roho Mtakatifu alisema:
"Niteulieni Barnaba na Saulo kwa ajili ya kazi niliyowaitia."
3 Basi,
baada ya kusali na kufunga zaidi, wakawawekea mikono, wakawaacha waende zao.
4 Basi,
Barnaba na Saulo walipokwisha tumwa na Roho Mtakatifu, walishuka hadi Seleukia,
na kutoka huko walipanda meli hadi kisiwa cha Kupro.
5
Walipofika Salami walihubiri neno la Mungu katika masunagogi ya Kiyahudi.
Yohane (Marko) alikuwa msaidizi wao.
6
Walitembea toka upande mmoja wa kisiwa mpaka Pafo upande wa pili, na huko
walimkuta mchawi mmoja Myahudi aitwaye Baryesu ambaye alijisingizia kuwa nabii.
7 Huyu
alikuwa pamoja na Sergio Paulo, mkuu wa kile kisiwa, ambaye alikuwa mtu mwelewa
sana. Sergio Paulo aliwaita Barnaba na Saulo ili asikie neno la Mungu.
8 Lakini
huyo mchawi Elima (kama alivyokuwa anaitwa kwa Kigiriki), alijaribu kuwapinga
ili kumzuia huyo mkuu wa kisiwa asije akaigeukia imani ya Kikristo.
9 Basi,
Saulo ambaye aliitwa pia Paulo, akiwa amejaa Roho Mtakatifu, alimkodolea macho
huyo mchawi,
10
akasema, "Mdanganyifu wa kupindukia na mlaghai wewe! Wewe ni mtoto wa
Ibilisi! Wewe ni adui wa chochote kile kilicho cha kweli; hukomi hata mara moja
kujaribu kuzipotosha njia za Bwana zilizonyoka.
11 Sasa,
mkono wa Bwana utakuadhibu: utakuwa kipofu na hutaweza kuuona mwanga wa jua kwa
kitambo." Mara kila kitu kikawa kama ukungu na giza kwake, akaanza kwenda
huku na huku akitafuta mtu wa kumshika mkono amwongoze.
12 Yule
mkuu wa kisiwa alipoona hayo, aliongoka akawa muumini; akastaajabia sana
mafundisho aliyosikia juu ya Bwana.
13 Kutoka
Pafo, Paulo na wenzake walipanda meli wakaenda hadi Perga katika Pamfulia;
lakini Yohane (Marko) aliwaacha, akarudi Yerusalemu.
14 Lakini wao waliendelea na safari toka Pisga hadi mjini
Antiokia Pisidia. Siku ya Sabato waliingia ndani ya Sunagogi, wakakaa.
15 Baada ya masomo katika kitabu cha Sheria ya Mose na
katika maandiko ya manabii, wakuu wa lile sunagogi waliwapelekea ujumbe huu:
"Ndugu, kama mnalo jambo la kuwaambia watu ili kuwapa moyo, semeni."
16 Basi, Paulo alisimama, akatoa ishara kwa mkono, akaanza
kuongea: "Wananchi wa Israeli na wengine wote mnaomcha Mungu, sikilizeni!
17 Mungu wa taifa hili la Israeli aliwateua babu zetu na
kuwafanya wawe taifa kubwa walipokuwa ugenini kule Misri. Mungu aliwatoa huko
kwa uwezo wake mkuu.
18 Aliwavumilia kwa muda wa miaka arobaini kule jangwani.
19 Aliyaangamiza mataifa ya nchi ya Kanaani akawapa hao
watu wake ile nchi kuwa mali yao.
20 Miaka mia nne na hamsini ilipita, halafu akawapatia waamuzi
wawaongoze mpaka wakati wa nabii Samweli.
21 Hapo wakapendelea kuwa na mfalme, na Mungu akawapa
Saulo, mtoto wa Kishi wa kabila la Benyamini, awe mfalme wao kwa muda wa miaka
arobaini.
22 Baada ya kumwondoa Saulo, Mungu alimteua Daudi kuwa
mfalme wao. Mungu alionyesha kibali chake kwake akisema: `Nimemwona Daudi mtoto
wa Yese; ni mtu anayepatana na moyo wangu; mtu ambaye atatimiza yale yote
ninayotaka kuyatenda.`
23 Kutokana na ukoo wake mtu huyu, Mungu, kama alivyoahidi,
amewapelekea watu wa Israeli Mwokozi, ndiye Yesu.
24 Kabla ya kuja kwake Yesu, Yohane alimtangulia
akiwahubiria watu wote wa Israeli kwamba ni lazima watubu na kubatizwa.
25 Yohane alipokuwa anamaliza ujumbe wake aliwaambia watu:
`Mnadhani mimi ni nani? Mimi si yule mnayemtazamia. Huyo anakuja baada yangu na
mimi sistahili hata kuzifungua kamba za viatu vyake.`
26 "Ndugu, ninyi mlio watoto wa ukoo wa Abrahamu, na
wengine wote mnaomcha Mungu! Ujumbe huu wa wokovu umeletwa kwetu.
27 Kwa maana wenyeji wa Yerusalemu na wakuu wao
hawakumtambua yeye kuwa Mwokozi. Wala hawakuelewa maneno ya manabii yanayosomwa
kila Sabato. Hata hivyo, waliyafanya maneno ya manabii yatimie kwa kumhukumu
Yesu adhabu ya kifo.
28 Ingawa hawakumpata na hatia inayostahili auawe,
walimwomba Pilato amhukumu auawe.
29 Na baada ya kutekeleza yote yaliyokuwa yameandikwa
kumhusu yeye, walimshusha kutoka msalabani, wakamweka kaburini.
30 Lakini Mungu alimfufua kutoka wafu.
31 Naye, kwa siku nyingi aliwatokea wale waliofuatana naye
kutoka Galilaya mpaka Yerusalemu. Hao ndio walio sasa mashahidi wake kwa watu
wa Israeli.
32 Sisi tumekuja hapa kuwaleteeni Habari Njema: jambo lile
Mungu alilowaahidia babu zetu amelitimiza sasa kwa ajili yetu sisi tulio
wajukuu wao kwa kumfufua Yesu kutoka wafu. Kama ilivyoandikwa katika zaburi ya
pili: `Wewe ni Mwanangu, mimi leo nimekuwa baba yako.`
33 []
34 Na juu ya kumfufua kutoka wafu, asipate tena kurudi huko
na kuoza, Mungu alisema hivi: `Nitakupa baraka takatifu na za kweli
nilizomwahidia Daudi.`
35 Naam, na katika sehemu nyingine za zaburi asema:
`Hutamwacha Mtakatifu wako aoze.`
36 Sasa, Daudi mwenyewe alitimiza mapenzi ya Mungu wakati
wake; kisha akafa na kuzikwa karibu na wazee wake, na mwili wake ukaoza.
37 Lakini yule ambaye Mungu alimfufua kutoka wafu hakupata
kuoza.
38 Jueni wazi, ndugu zangu, kwamba ujumbe kuhusu kusamehewa
dhambi unahubiriwa kwenu kwa njia ya Yesu Kristo; na ya kwamba kila mmoja
anayemwamini Yesu anasamehewa dhambi zote, jambo ambalo halingewezekana kwa
njia ya Sheria ya Mose.
39 []
40 Jihadharini basi, msije mkapatwa na yale yaliyosemwa na
manabii:
41 `Sikilizeni enyi wenye madharau, shangaeni mpotee! Kwa
maana kitu ninachofanya sasa, nyakati zenu, ni kitu ambacho hamtakiamini hata
kama mtu akiwaelezeni."`
42 Paulo na Barnaba walipokuwa wanatoka katika ile
sunagogi, wale watu waliwaalika waje tena siku ya Sabato iliyofuata, waongee
zaidi juu ya mambo hayo.
43 Mkutano huo ulipomalizika, Wayahudi wengi na watu wa
mataifa mengine waliokuwa wameongokea dini ya Kiyahudi waliwafuata Paulo na
Barnaba. Hao mitume waliongea nao, wakawatia moyo waendelee kuishi wakitegemea
neema ya Mungu.
44 Siku ya Sabato iliyofuata, karibu kila mtu katika ule
mji alikuja kusikiliza neno la Bwana.
45 Lakini Wayahudi walipoliona hilo kundi la watu walijaa
wivu, wakapinga alichokuwa anasema Paulo na kumtukana.
46 Hata hivyo, Paulo na Barnaba waliongea kwa uhodari
zaidi, wakasema, "Ilikuwa ni lazima neno la Mungu liwafikieni ninyi
kwanza; lakini kwa kuwa mmelikataa na kujiona hamstahili uzima wa milele, basi,
tunawaacheni na kuwaendea watu wa mataifa mengine.
47 Maana Bwana alituagiza hivi: `Nimekuteua wewe uwe mwanga
kwa mataifa, uwe njia ya wokovu kwa ulimwengu wote."`
48 Watu wa mataifa mengine waliposikia jambo hilo
walifurahi, wakausifu ujumbe wa Mungu; na wale waliokuwa wamechaguliwa kupata
uzima wa milele, wakawa waumini.
49 Neno la Bwana likaenea kila mahali katika sehemu ile.
50 Lakini Wayahudi waliwachochea wanawake wa tabaka ya juu
wa mataifa mengine ambao walikuwa wacha Mungu, na wanaume maarufu wa mji huo.
Wakaanza kuwatesa Paulo na Barnaba, wakawafukuza kutoka katika eneo lao.
51 Basi, mitume wakayakung`uta mavumbi yaliyokuwa katika
miguu yao kama onyo, kisha wakaenda Ikonio.
52 Lakini hao wafuasi walikuwa wamejaa furaha na Roho
Mtakatifu.
|