Chapter 14
1 Kule Ikonio, mambo yalikuwa kama yalivyokuwa kule
Antiokia; Paulo na Barnaba walikwenda katika sunagogi la Wayahudi wakaongea kwa
uhodari hata Wayahudi wengi na Wagiriki wakawa waumini.
2 Lakini Wayahudi wengine waliokataa kuwa waumini
walichochea na kutia chuki katika mioyo ya watu wa mataifa mengine ili
wawapinge hao ndugu.
3 Paulo na
Barnaba waliendelea kukaa huko kwa muda mrefu. Waliongea kwa uhodari juu ya
Bwana, naye Bwana akathibitisha ukweli wa ujumbe walioutoa juu ya neema yake,
kwa kuwawezesha kutenda miujiza na maajabu.
4 Watu wa
mji huo waligawanyika: wengine waliwaunga mkono Wayahudi, na wengine walikuwa
upande wa mitume.
5
Mwishowe, baadhi ya watu wa mataifa mengine na Wayahudi, wakishirikiana na
wakuu wao, waliazimu kuwatendea vibaya hao mitume na kuwapiga mawe.
6 Mitume
walipogundua jambo hilo, walikimbilia Lustra na Derbe, miji ya Lukaonia, na
katika sehemu za jirani,
7 wakawa
wanahubiri Habari Njema huko.
8 Kulikuwa
na mtu mmoja huko Lustra ambaye alikuwa amelemaa miguu tangu kuzaliwa, na
alikuwa hajapata kutembea kamwe.
9 Mtu huyo
alikuwa anamsikiliza Paulo alipokuwa anahubiri. Paulo alimtazama kwa makini, na
alipoona kuwa alikuwa na imani ya kuweza kuponywa,
10 akasema
kwa sauti kubwa, "Simama wima kwa miguu yako!" Huyo mtu aliyelemaa
akainuka ghafla, akaanza kutembea.
11 Umati
wa watu walipoona alichofanya Paulo, ulianza kupiga kelele kwa lugha ya
Kilukaonia: "Miungu imetujia katika sura za binadamu!"
12 Barnaba
akaitwa Zeu, na Paulo, kwa vile yeye ndiye aliyekuwa anaongea, akaitwa Herme.
13 Naye
kuhani wa hekalu la Zeu lililokuwa nje ya mji akaleta fahali na shada za maua
mbele ya mlango mkuu wa mji, na pamoja na ule umati wa watu akataka
kuwatambikia mitume.
14 Barnaba
na Paulo walipopata habari hiyo waliyararua mavazi yao na kukimbilia katika
lile kundi la watu wakisema kwa sauti kubwa:
15
"Ndugu, kwa nini mnafanya mambo hayo? Sisi pia ni binadamu kama
ninyi. Na, tuko hapa kuwahubirieni Habari Njema, mpate kuziacha hizi sanamu
tupu, mkamgeukie Mungu aliye hai, Mungu aliyeumba mbingu na nchi, bahari na
vyote vilivyomo.
16 Zamani Mungu aliruhusu kila taifa lifanye lilivyopenda.
17 Hata hivyo, Mungu hakuacha kujidhihirisha kwa mambo mema
anayowatendea: huwanyeshea mvua toka angani, huwapa mavuno kwa wakati wake,
huwapa chakula na kuijaza mioyo yenu furaha."
18 Ingawa walisema hivyo haikuwa rahisi kuwazuia wale watu
wasiwatambikie.
19 Lakini Wayahudi kadhaa walikuja kutoka Antiokia na
Ikonio, wakawafanya watu wajiunge nao, wakampiga mawe Paulo na kumburuta hadi
nje ya mji wakidhani amekwisha kufa.
20 Lakini waumini walipokusanyika na kumzunguka, aliamka
akarudi mjini. Kesho yake, yeye pamoja na Barnaba walikwenda Derbe.
21 Baada ya Paulo na Barnabas kuhubiri Habari Njema huko
Derbe na kupata wafuasi wengi, walifunga safari kwenda Antiokia kwa kupitia
Lustra na Ikonio.
22 Waliwaimarisha waumini wa miji hiyo na kuwatia moyo
wabaki imara katika imani. Wakawaambia, "Ni lazima sisi sote tupitie
katika taabu nyingi ili tuingie katika ufalme wa Mungu."
23 Waliteua wazee katika kila kanisa kwa ajili ya waumini,
na baada ya kusali na kufunga, wakawaweka chini ya ulinzi wa Bwana ambaye
walikuwa wanamwamini.
24 Baada ya kupitia katika nchi ya Pisidia, walifika
Pamfulia.
25 Baada ya kuhubiri ule ujumbe huko Perga, walikwenda
Atalia.
26 Kutoka huko walisafiri kwa meli wakarudi Antiokia ambako
hapo awali walikuwa wamewekwa chini ya ulinzi wa neema ya Mungu kwa ajili ya
kazi ambayo sasa walikuwa wameitimiza.
27 Walipofika huko Antiokia walifanya mkutano wa kanisa la
mahali hapo, wakawapa taarifa juu ya mambo Mungu aliyofanya pamoja nao, na
jinsi alivyowafungulia mlango watu wa mataifa mengine mlango wa kuingia katika
imani.
28 Wakakaa pamoja na wale waumini kwa muda mrefu.
|