Chapter 15
1 Basi, watu wengine walifika Antiokia kutoka Yudea
wakaanza kuwafundisha wale ndugu wakisema, "Kama hamtatahiriwa kufuatana
na mapokeo ya Sheria ya Mose, hamtaweza kuokolewa."
2 Jambo hili lilisababisha ubishi mkubwa, na baada ya Paulo
na Barnaba kujadiliana nao, ikaamuliwa Paulo na Barnaba pamoja na waumini
kadhaa wa lile kanisa la Antiokia waende Yerusalemu kuwaona wale mitume na wazee
kuhusu jambo hilo.
3 Basi, kanisa liliwaaga, nao walipokuwa wanapitia Foinike
na Samaria waliwaeleza watu jinsi mataifa mengine yalivyomgeukia Mungu. Habari
hizo zikawafurahisha sana ndugu hao wote.
4 Walipofika Yerusalemu walikaribishwa na kanisa, mitume na
wazee; nao wakawapa taarifa juu ya yote Mungu aliyoyafanya pamoja nao.
5 Lakini waumini wengine waliokuwa wa kikundi cha
Mafarisayo walisimama, wakasema, "Ni lazima watu wa mataifa mengine
watahiriwe na kufundishwa kuifuata Sheria ya Mose."
6 Basi, mitume na wazee walifanya mkutano maalum wa
kuchunguza jambo hilo.
7 Baada ya majadiliano marefu, Petro alisimama, akasema,
"Ndugu zangu, ninyi mnafahamu kwamba hapo awali Mungu alipenda kunichagua
mimi miongoni mwenu niihubiri Habari Njema, ili watu wa mataifa wapate kusikia
na kuamini.
8 Naye Mungu anayejua mioyo ya watu, alithibitisha kwamba
amewakubali kwa kuwapa nao Roho Mtakatifu kama alivyotupa sisi.
9 Hakufanya ubaguzi wowote kati yetu na wao; aliitakasa
mioyo yao kwa imani.
10 Sasa basi, kwa nini kumjaribu Mungu kwa kuwatwika hao
waumini mzigo ambao wala babu zetu, wala sisi hatukuweza kuubeba?
11 Isiwe hivyo, ila tunaamini kwamba, sisi kama vile wao,
tunaokolewa kwa njia ya neema ya Bwana Yesu."
12 Kikundi chote kilikaa kimya, kikawasikiliza Barnaba na
Paulo wakieleza miujiza na maajabu ambayo Mungu alitenda kwa mikono yao kati ya
watu wa mataifa mengine.
13 Walipomaliza kuongea, Yakobo alianza kusema: "Ndugu
zangu, nisikilizeni!
14 Simoni ameeleza jinsi Mungu hapo awali
alivyojishughulisha na watu wa mataifa mengine, akachagua baadhi yao wawe watu
wake.
15 Jambo hili ni sawa kabisa na maneno ya manabii, kama
Maandiko Matakatifu yasemavyo:
16 `Baada ya mambo haya nitarudi. Nitaijenga tena ile
nyumba ya Daudi iliyoanguka; nitayatengeneza magofu yake na kuijenga tena.
17 Hapo watu wengine wote, watu wa mataifa yote niliowaita
wawe wangu, watamtafuta Bwana.
18 Ndivyo asemavyo Bwana, aliyefanya jambo hili lijulikane
tangu kale.`
19 "Kwa hiyo, uamuzi wangu ni huu: tusiwataabishe watu
wa mataifa wanomgeukia Mungu.
20 Bali tuwapelekee barua kuwaambia wasile vyakula
vilivyotiwa najisi kwa kutambikiwa sanamu za miungu; wajiepushe na uasherati;
wasile mnyama yeyote aliyenyongwa, na wasinywe damu.
21 Kwa maana kwa muda mrefu maneno ya Mose yamekuwa
yakihubiriwa katika kila mji na kusomwa katika masunagogi yote kila siku ya
Sabato." ic
22 Mitume, wazee na kanisa lote waliamua kuwachagua watu
fulani miongoni mwao na kuwatuma Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba. Basi,
wakamchagua Yuda aitwaye pia Barsaba, na Sila ambao wote walikuwa wanajulikana
zaidi kati ya ndugu.
23 Wakawapa barua hii: mataifa mengine mlioko huko
Antiokia, Siria na Kilikia.
24 Tumesikia kwamba watu wengine kutoka huku kwetu
waliwavurugeni kwa maneno yao, wakaitia mioyo yenu katika wasiwasi. Lakini
wamefanya hivyo bila ya idhini yoyote kutoka kwetu.
25 Hivyo, tumeamua kwa pamoja kuwachagua watu kadhaa na
kuwatuma kwenu pamoja na wapenzi wetu Barnaba na Paulo,
26 ambao wamehatarisha maisha yao kwa ajili ya jina la
Bwana wetu Yesu Kristo.
27 Kwa hiyo, tunawatuma Yuda na Sila kwenu; hawa
watawaambieni wao wenyewe haya tuliyoandika.
28 Basi, Roho Mtakatifu na sisi tumekubali tusiwatwike
mzigo zaidi ya mambo haya muhimu:
29 Msile vyakula vilivyotambikiwa sanamu; msinywe damu;
msile nyama ya mnyama aliyenyongwa; na mjiepushe na uasherati. Mtakuwa mmefanya
vema kama mkiepa kufanya mambo hayo. Wasalaam!"
30 Baada ya kuwaaga, hao wajumbe walielekea Antiokia ambako
waliita mkutano wa waumini, wakawapa hiyo barua.
31 Walipoisoma hiyo barua, maneno yake yaliwatia moyo,
wakafurahi sana.
32 Yuda na Sila, ambao nao walikuwa manabii, walizungumza
na hao ndugu kwa muda mrefu wakiwatia moyo na kuwaimarisha.
33 Baada ya kukaa huko kwa muda fulani, ndugu wa Antiokia
waliwaaga wakiwatakia amani, kisha wakarudi kwa wale waliokuwa wamewatuma.*fb*
34 missing
35 Paulo na Barnaba walibaki huko Antiokia kwa muda;
wakafundisha na kuhubiri neno la Bwana, pamoja na watu wengine wengi.
36 Baada ya siku kadhaa, Paulo alimwambia Barnaba,
"Turudi tukawatembelee wale ndugu katika kila mji tulikolihubiri neno la
Bwana tukajionee jinsi wanavyoendelea."
37 Barnaba alitaka wamchukue pia Yohane aitwaye Marko.
38 Lakini Paulo hakupendelea kumchukua Marko, ambaye awali
aliwaacha kule Pamfulia na kukataa kushiriki katika kazi yao.
39 Basi kukatokea ubishi mkali kati yao, na wakaachana.
Barnaba akamchukua Marko, wakapanda meli kwenda Kupro.
40 Naye Paulo akamchagua Sila, na baada ya ndugu wa mahali
hapo kumweka chini ya ulinzi wa neema ya Bwana, akaondoka.
41 Katika safari hiyo alipitia Siria na Kilikia
akiyaimarisha makanisa.
|