Chapter 16
1 Paulo alifika Derbe na Lustra, ambako aliishi mfuasi
mmoja aitwaye Timotheo. Mama yake ambaye pia alikuwa mfuasi, alikuwa Myahudi;
lakini baba yake alikuwa Mgiriki.
2 Timotheo alikuwa na sifa kubwa kati ya wale ndugu wa
Lustra na Ikonio.
3 Paulo alitaka Timotheo aandamane naye safarini, kwa hiyo
alimtahiri. Alifanya hivyo kwa sababu Wayahudi wote walioishi sehemu hizo
walijua kwamba baba yake Timotheo alikuwa Mgiriki.
4 Walipokuwa wanapita katika ile miji waliwapa watu yale
maagizo yaliyotolewa na mitume na wazee kule Yerusalemu, wakawaambia
wayazingatie.
5 Hivyo, yale makanisa yalizidi kuwa imara katika imani, na
idadi ya waumini ikaongezeka kila siku.
6 Walipitia sehemu za Frugia na Galatia kwani Roho
Mtakatifu hakuwaruhusu kuhubiri huo ujumbe mkoani Asia.
7 Walipofika kwenye mipaka ya Musia, walijaribu kuingia
mkoani Bithunia, lakini Roho wa Yesu hakuwaruhusu.
8 Basi, walipitia Musia, wakaenda moja kwa moja mpaka Troa.
9 Usiku huo, Paulo aliona ono ambalo alimwona mtu mmoja wa
Makedonia amesimama pale na kumwomba: "Vuka, uje Makedonia
ukatusaidie."
10 Mara baada ya Paulo kuona ono hilo, tulijitayarisha
kwenda Makedonia bila kukawia, tukiwa na hakika kwamba Mungu ametuita
tuwapelekee Habari Njema.
11 Kutoka Troa, tulisafiri kwa meli moja kwa moja mpaka
Samothrake, na kesho yake tukatia nanga Neapoli.
12 Kutoka huko, tulikwenda mpaka Filipi, mji wa wilaya ya
kwanza ya Makedonia, na ambao pia ni koloni la Waroma. Tulikaa katika mji huo
siku kadhaa.
13 Siku ya Sabato tulitoka nje ya mji, tukaenda kando ya
mto ambapo tulidhani ya kuwa ni mahali pa kusali. Tuliketi, tukaongea na
wanawake waliokusanyika mahali hapo.
14 Miongoni mwa wale waliotusikiliza alikuwa mwanamke mmoja
mcha Mungu aitwaye Ludia mwenyeji wa Thuatira, ambaye alikuwa mfanyabiashara ya
nguo za kitani za rangi ya zambarau. Bwana aliufungua moyo wake hata akayapokea
yale maneno Paulo aliyokuwa anasema.
15 Baada ya huyo mama pamoja na jamaa yake kubatizwa,
alitualika akisema, "Kama kweli mmeona kwamba mimi namwamini Bwana,
karibuni nyumbani kwangu mkakae." Akatuhimiza twende.
16 Siku moja, tulipokuwa tunakwenda mahali pa kusali,
msichana mmoja aliyekuwa na pepo mwenye uwezo wa kuagua alikutana nasi.
Msichana huyo alikuwa anawapatia matajiri wake fedha nyingi kwa uaguzi wake.
17 Basi, huyo msichana alimfuata Paulo na sisi, akipiga
kelele na kusema, "Hawa watu ni watumishi wa Mungu Mkuu. Wanawatangazieni
njia ya wokovu."
18 Akawa anafanya hivyo kwa siku nyingi hata siku moja
Paulo alikasirika, akamgeukia na kumwambia huyo pepo, "Nakuamuru kwa jina
la Yesu Kristo, mtoke huyu!" Mara huyo pepo akamtoka.
19 Matajiri wa yule msichana walipoona kwamba tumaini lao
la kupata mali limekwisha, waliwakamata Paulo na Sila, wakawaburuta mpaka
hadharani, mbele ya wakuu.
20 Wakawashtaki kwa mahakimu wakisema, "Watu hawa ni
Wayahudi na wanafanya fujo katika mji wetu.
21 Wanafundisha desturi ambazo sisi raia wa Roma
haturuhusiwi kuzikubali wala kuzifuata."
22 Kundi la watu likajiunga nao, likawashambulia. Wale
mahakimu wakawatatulia Paulo na Sila mavazi yao, wakaamuru wapigwe viboko.
23 Baada ya kupigwa sana wakatiwa ndani, na askari wa gereza
akaamriwa kuwaweka chini ya ulinzi mkali.
24 Kutokana na maagizo hayo, huyo askari aliwaweka katika
chumba cha ndani kabisa cha gereza na kuifunga miguu yao kwenye nguzo.
25 Karibu na usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa
wakisali na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, huku wafungwa wengine wakiwa
wanasikiliza.
26 Ghafla, kulitokea mtetemeko mkuu wa ardhi ambao
uliitikisa misingi ya gereza. Mara, milango yote ikafunguka na minyororo
iliyowafunga hao wafungwa ikaachana.
27 Askari wa gereza alipoamka na kuiona milango ya gereza
imefunguliwa, alidhani kwamba wafungwa wote walikuwa wametoroka na hivyo
akauchomoa upanga wake, akataka kujiua.
28 Lakini Paulo akaita kwa sauti kubwa: "Usijidhuru
mwenyewe kwa maana sisi sote tuko hapa."
29 Baada ya kumwita mtu alete taa, huyo askari wa gereza
alikimbilia ndani, akajitupa mbele ya miguu ya Paulo na Sila huku akitetemeka
kwa hofu.
30 Halafu aliwaongoza nje, akawauliza, "Waheshimiwa,
nifanye nini nipate kuokoka?"
31 Wao wakamjibu, "Mwamini Bwana Yesu nawe utaokolewa
pamoja na jamaa yako yote."
32 Basi, wakamhubiria neno la Bwana yeye pamoja na jamaa
yake.
33 Yule askari aliwachukua saa ileile ya usiku akawasafisha
majeraha yao, kisha yeye na jamaa yake wakabatizwa papo hapo.
34 Halafu akawachukua Paulo na Sila nyumbani kwake, akawapa
chakula. Yeye na jamaa yake yote wakafanya sherehe kwa vile sasa walikuwa
wanamwamini Mungu.
35 Kesho yake asubuhi, mahakimu waliwatuma maofisa wao
wakisema, "Wafungueni wale watu."
36 Yule askari wa gereza alimpasha habari Paulo:
"Mahakimu wametuma ujumbe ili mfunguliwe. Sasa mnaweza kutoka na kwenda
zenu kwa amani."
37 Lakini Paulo alimjibu, "Ati nini? Ingawa hatukuwa
na kosa, walitupiga viboko hadharani hali sisi ni raia wa Roma. Tena, walitutia
ndani na sasa wanataka kutufungulia kwa siri! Hata kidogo! Ni lazima wao
wenyewe waje hapa watufungulie."
38 Hao maofisa waliwapasha habari mahakimu juu ya jambo
hilo, nao waliposikia kwamba Paulo na Sila walikuwa raia wa Roma, waliogopa.
39 Hivyo, walikwenda kuwataka radhi na baada ya kuwatoa
ndani waliwaomba watoke katika mji ule.
40 Paulo na Sila walitoka gerezani, wakaenda nyumbani kwa
Ludia. Huko walionana na ndugu waumini na baada ya kuwatia moyo wakaondoka.
|