Chapter 17
1 Kwa kupitia Amfipoli na Apolonia, walisafiri mpaka
Thesalonika ambako kulikuwa na sunagogi la Wayahudi.
2 Paulo alijiunga nao kama ilivyokuwa desturi yake
akajadiliana nao Sabato tatu mfululizo, akatumia Maandiko Matakatifu.
3 Aliyaeleza na kuonyesha kwamba ilimbidi Kristo kuteswa na
kufufuka kutoka wafu. Akawaambia, "Yesu ambaye mimi namhubiri kwenu ndiye
Kristo."
4 Baadhi yao walikubali wakajiunga na Paulo na Sila.
Kadhalika, idadi kubwa ya Wagiriki waliomcha Mungu pamoja na wanawake wengi wa
tabaka la juu, walijiunga nao.
5 Lakini Wayahudi wakaona wivu; wakawakodi wafidhuli sokoni,
wakafanya kikundi na kuzusha fujo mjini kote. Wakaivamia nyumba ya Yasoni
wakitumaini kuwapata humo Paulo na Sila ili wawalete hadharani.
6 Lakini hawakuwapata na hivyo walimburuta Yasoni pamoja na
ndugu wengine mpaka kwa wakuu wa mji, wakapiga kelele: "Watu hawa wamekuwa
wakivuruga dunia yote na sasa wako hapa mjini.
7 Yasoni amewakaribisha nyumbani kwake. Wote wanafanya
kinyume cha amri ya Kaisari wakisema eti `Kuna mfalme mwingine aitwaye
Yesu."`
8 Kwa maneno hayo waliwatia wasiwasi wakuu wa mji na kundi
la watu.
9 Wakawafanya Yasoni na wenzake watoe dhamana, kisha
wakawaacha waende zao.
10 Usiku, wale ndugu waliwahimiza Paulo na Sila waende
Berea. Mara tu walipofika huko, walikwenda katika sunagogi la Wayahudi.
11 Watu wa huko walikuwa wasikivu zaidi kuliko wale wa
Thesalonika. Waliupokea ule ujumbe kwa hamu kubwa, wakawa wanayachunguza
Maandiko Matakatifu kila siku, ili kuona kama yale waliyosema Paulo na Sila
yalikuwa kweli.
12 Wengi wao waliamini na pia wanawake wa Kigiriki wa
tabaka la juu na wanaume pia.
13 Lakini, Wayahudi wa Thesalonika walipogundua kwamba
Paulo alikuwa anahubiri neno la Mungu huko Berea, walikwenda huko, wakaanza
kufanya fujo na kuchochea makundi ya watu.
14 Wale ndugu wakamsindikiza haraka aende pwani lakini Sila
na Timotheo walibaki Berea.
15 Wale ndugu waliomsindikiza Paulo walikwenda pamoja naye
mpaka Athene. Kisha, wakarudi pamoja na maagizo kutoka kwa Paulo kwamba Sila na
Timotheo wamfuate upesi iwezekanavyo.
16 Paulo alipokuwa anawasubiri Sila na Timotheo huko
Athene, moyo wake ulighadhibika sana alipoona jinsi mji huo ulivyokuwa umejaa
sanamu za miungu.
17 Alijadiliana na Wayahudi na watu wengine waliomcha Mungu
katika sunagogi; na kila siku alikuwa na majadiliano sokoni pamoja na wowote
wale waliojitokeza.
18 Wengine waliofuata falsafa ya Epikuro na Stoiki walibishana
naye. Wengine walisema, "Anataka kusema nini huyu bwanamaneno?" Kwa
kuwa Paulo alikuwa anahubiri juu ya Yesu na juu ya ufufuo, wengine walisema,
"Inaonekana kama anahubiri juu ya miungu ya kigeni."
19 Hivyo walimchukua Paulo, wakampeleka Areopago, wakasema,
"Tunataka kujua jambo hili jipya ulilokuwa unazungumzia.
20 Vitu vingine tulivyosikia kwa masikio yetu vinaonekana
kuwa viroja kwetu. Tungependa kujua mambo haya yana maana gani."
21 Wananchi wa Athene na wakazi wengine wa huko walikuwa
wanatumia wakati wao wote kuhadithiana na kusikiliza habari mpyampya. ic
22 Basi, Paulo alisimama mbele ya baraza la Areopago,
akasema, "Wananchi wa Athene! Ninaona kwamba ninyi, kwa vyovyote, ni watu
wa dini sana.
23 Sababu yenyewe ni kwamba katika pitapita yangu
niliangalia sanamu zenu za ibada nikakuta madhabahu moja ambayo imeandikwa:
`Kwa ajili ya Mungu yule Asiyejulikana.` Basi, huyo mnayemwabudu bila kujua,
ndiye ninayemhubiri kwenu.
24 Mungu, aliyeumba ulimwengu na vyote vilivyomo, ni Bwana
wa mbingu na nchi; yeye hakai katika hekalu zilizojengwa na watu.
25 Wala hatumikiwi kwa mikono ya watu kana kwamba anahitaji
chochote kile, kwa maana yeye mwenyewe ndiye anayewapa watu uhai, anawawezesha
kupumua na anawapa kila kitu.
26 Kutokana na mtu mmoja aliumba mataifa yote na
kuyawezesha kuishi duniani kote. Aliamua na kupanga kabla kabisa lini na wapi
mataifa hayo yangeishi.
27 Alifanya hivyo, ili mataifa hayo yapate kumfuata, na
kama vile kwa kupapasapapasa, yapate kumfikia. Hata hivyo lakini, Mungu hayuko
mbali na kila mmoja wetu.
28 Kama alivyosema mtu mmoja: `Ndani yake yeye sisi
tunaishi, tunajimudu, na tuko!` Ni kama washairi wenu wengine walivyosema:
`Sisi ni watoto wake.`
29 Ikiwa basi, sisi ni watoto wa Mungu, haifai kumfikiria
Mungu kuwa kama dhahabu, fedha au hata jiwe lililochongwa na kutiwa nakshi na
binadamu.
30 Mungu alifanya kama kwamba haoni nyakati zile watu
walipokuwa wajinga. Lakini sasa, anaamuru watu wote kila mahali watubu.
31 Kwa maana amekwisha weka siku ambayo atauhukumu
ulimwengu kwa haki kwa njia ya mtu mmoja aliyemteua. Mungu amewathibitishia
wote jambo hili kwa kumfufua mtu huyo kutoka wafu!"
32 Walipomsikia Paulo anasema juu ya jambo la kufufuka kwa
wafu, wengine wao waliangua kicheko; lakini wengine walisema, "Tunataka
kukusikia tena juu ya jambo hili!"
33 Hivyo, Paulo aliwaacha, akatoka barazani.
34 Lakini watu kadhaa waliandamana naye, wakawa waumini.
Miongoni mwao walikuwa Dionisio wa Areopago, mwanamke mmoja aitwaye Damari na
wengineo.
|