Chapter 18
1 Baada ya hayo, Paulo aliondoka Athene, akaenda Korintho.
2 Huko Korintho, alimkuta Myahudi mmoja aitwaye Akula,
mzaliwa wa Ponto. Akula pamoja na mkewe aitwaye Priskila, walikuwa wamerudi
kutoka Italia siku hizohizo kwa sababu Kaisari Klaudio alikuwa ameamuru
Wayahudi wote waondoke Roma. Paulo alikwenda kuwaona,
3 na kwa vile wao walikuwa mafundi wa kushona mahema kama
alivyokuwa yeye, Paulo alikaa nao akafanya kazi.
4 Kila Sabato alifanya majadiliano katika sunagogi
akijaribu kuwavuta Wayahudi na Wagiriki.
5 Baada ya Sila na Timotheo kuwasili kutoka Makedonia,
Paulo alianza kutumia wakati wake wote kwa ajili ya kuhubiri, akawathibitishia
Wayahudi kwamba Yesu ndiye Kristo.
6 Walipompinga na kuanza kumtukana, aliyakung`uta mavazi
yake mbele yao akisema, "Mkipotea ni shauri lenu wenyewe; mimi sina lawama
yoyote juu ya jambo hilo. Na tangu sasa nitawaendea watu na mataifa mengine."
7 Basi, akatoka hapo akaenda kukaa nyumbani kwa mtu mmoja
mcha Mungu aitwaye Tito Yusto. Nyumba yake Tito ilikuwa karibu na lile
sunagogi.
8 Lakini Krispo, mkuu wa sunagogi, alimwamini Bwana yeye
pamoja na jamaa yake yote. Wakorintho wengi waliusikiliza ujumbe huo, wakaamini
na kubatizwa.
9 Siku moja usiku, Bwana alimwambia Paulo katika maono:
"Usiogope, endelea kuhubiri tu bila kufa moyo,
10 maana mimi niko pamoja nawe. Hakuna mtu atakayejaribu
kukudhuru maana hapa mjini pana watu wengi walio upande wangu."
11 Basi, Paulo alikaa huko akifundisha neno la Mungu kati
yao kwa muda wa mwaka mmoja na nusu.
12 Lakini wakati Galio alipokuwa mkuu wa mkoa wa Akaya,
Wayahudi walimvamia Paulo kwa pamoja na kumpeleka mahakamani.
13 Wakasema, "Tunamshtaki mtu huyu kwa sababu ya
kuwashawishi watu wamwabudu Mungu kwa namna inayopingana na Sheria."
14 Kabla tu Paulo hajaanza kusema, Galio aliwaambia
Wayahudi, "Sikilizeni enyi Wayahudi! Kama kweli jambo hili lingekuwa juu
ya uhalifu au uovu ningekuwa tayari kuwasikilizeni.
15 Lakini kama ni shauri la ubishi kuhusu maneno na majina
ya Sheria yenu, amueni ninyi wenyewe. Mimi sitaki kuwa hakimu wa mambo
haya!"
16 Basi, akawafukuza kutoka mahakamani.
17 Nao wote wakamkamata Sosthene ambaye alikuwa kiongozi wa
sunagogi, wakampiga palepale mbele ya mahakama. Lakini Galio hakujali kitendo
hicho hata kidogo.
18 Paulo alikaa bado na wale ndugu huko Korintho kwa siku
nyingi. Kisha aliwaaga,
akapanda meli kwenda Siria pamoja na Priskila na Akula. Huko Kenkrea, alinyoa
nywele zake kwa sababu ya nadhiri aliyokuwa ameweka.
19
Walifika Efeso na hapo Paulo aliwaacha Priskila na Akula, akaenda katika
sunagogi, akajadiliana na Wayahudi.
20
Walimwomba akae nao muda mrefu zaidi, lakini hakupenda.
21 Bali
alipokuwa anaondoka, alisema, "Mungu akipenda nitakuja kwenu tena."
Akaondoka Efeso kwa meli.
22 Meli
ilitia nanga Kaisarea, naye Paulo akaenda Yerusalemu kulisalimia lile kanisa,
kisha akaenda Antiokia.
23 Alikaa
huko muda mfupi, halafu akaendelea na safari kwa kupitia sehemu za Galatia na
Frugia akiwatia moyo wafuasi wote.
24 Myahudi
mmoja aitwaye Apolo, mzaliwa wa Aleksandria, alifika Efeso. Alikuwa mtu mwenye
ufasaha wa kuongea na mwenye ujuzi mkubwa wa Maandiko Matakatifu.
25 Alikuwa
amefundishwa juu ya hiyo njia ya Bwana, na akiwa motomoto, aliongea juu ya
habari za Yesu. Akafundisha kwa usahihi ingawa alikuwa amepata ubatizo wa
Yohane tu.
26
Priskila na Akula walipomsikia akiongea kwa uhodari ndani ya sunagogi,
walimchukua kwao wakamfundisha hiyo Njia ya Mungu kwa usahihi zaidi.
27 Apolo
alipoamua kwenda Akaya, wale ndugu walimtia moyo kwa kuwaandikia wafuasi kule
Akaya wampokee. Alipofika huko, aliweza kwa msaada wa neema ya Mungu,
kuwasaidia sana wale ndugu waliopata kuwa waumini;
28 kwa
maana aliendelea kwa uhodari kuwashinda Wayahudi hadharani akithibitisha kwa
Maandiko Matakatifu kuwa Yesu ni Kristo.
|