Chapter 3
1 Siku hizo Yohane Mbatizaji alitokea, akaanza kuhubiri
katika jangwa la Yudea:
2 "Tubuni, maana Ufalme wa mbinguni umekaribia."
3 Huyu Yohane ndiye yule ambaye nabii Isaya alinena juu
yake aliposema: "Sauti ya mtu imesikika jangwani: `Mtayarishieni Bwana
njia yake, nyoosheni vijia vyake."`
4 Yohane alivaa vazi lililoshonwa kwa manyoya ya ngamia, na
ukanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya
mwituni.
5 Basi, watu kutoka Yerusalemu, kutoka mkoa wote wa Yudea
na sehemu zote za kandokando ya mto Yordani, walimwendea,
6 wakaziungama dhambi zao, naye akawabatiza katika mto
Yordani.
7 Lakini alipowaona Mafarisayo wengi na Masadukayo wanamjia
ili awabatize, aliwaambia, "Enyi kizazi cha nyoka! Ni nani aliyewadokezea
kwamba mnaweza kuiepuka ghadhabu inayokuja?
8 Onyesheni basi kwa matendo, kwamba mmetubu kweli.
9 Msidhani kwamba mtaweza kujitetea kwa kusema, `Baba yetu
ni Abrahamu!` Nawaambieni hakika, Mungu anaweza kuyafanya mawe haya yawe watoto
wa Abrahamu.
10 Basi, shoka liko tayari kuikata mizizi ya miti; hivyo,
kila mti usiozaa matunda mazuri, utakatwa na kutupwa motoni.
11 Mimi ninawabatizeni kwa maji kuonyesha kwamba mmetubu.
Lakini yule anayekuja baada yangu ana uwezo kuliko mimi. Mimi sistahili hata
kubeba viatu vyake. Yeye atawabatizeni kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.
12 Yeye anashika mkononi chombo cha kupuria nafaka, ili
aipure nafaka yake; akusanye ngano ghalani, na makapi ayachome kwa moto
usiozimika." ic
13 Wakati huo Yesu alitoka Galilaya akafika katika mto
Yordani, akamwendea Yohane ili abatizwe naye.
14 Lakini Yohane alijaribu kumzuia akisema, "Je, wewe
unakuja kwangu? Mimi hasa ndiye ninayehitaji kubatizwa nawe."
15 Lakini Yesu akamjibu, "Acha tu iwe hivyo kwa sasa,
maana kwa namna hii inafaa tuyatekeleze yale yote Mungu anayotaka." Hapo
Yohane akakubali.
16 Mara tu Yesu alipokwisha batizwa, alitoka majini; na
ghafla mbingu zikafunguka, akaona Roho wa Mungu akishuka kama njiwa na kutua
juu yake.
17 Sauti kutoka mbinguni ikasema, "Huyu ndiye Mwanangu
mpendwa, nimependezwa naye."
|