Chapter 20
1 Ile
ghasia ya Efeso ilipokwisha tulia Paulo aliwaita pamoja wale waumini, akawatia
moyo. Kisha akawaaga, akasafiri kwenda Makedonia.
2 Alipitia
sehemu za nchi zile akiwatia watu moyo kwa maneno mengi. Halafu akafika
Ugiriki.
3 ambako
alikaa kwa miezi mitatu. Alipokuwa anajitayarisha kwenda Siria, aligundua
kwamba Wayahudi walikuwa wanamfanyia mpango mbaya; hivyo aliamua kurudi kwa
kupitia Makedonia.
4 Sopatro,
mwana wa Pirho kutoka Berea, aliandamana naye; pia Aristarko na Sekundo kutoka
Thesalonika, Gayo kutoka Derbe, Timotheo, Tukiko na Trofimo wa mkoa wa Asia.
5 Hao
walitutangulia na kutungojea kule Troa.
6 Sisi,
baada ya sikukuu ya Mikate Isiyotiwa chachu, tulipanda meli kutoka Filipi na
baada ya siku tatu tukawafikia kule Troa. Huko tulikaa kwa muda wa juma moja.
7 Jumamosi
jioni, tulikutana ili kumega mkate. Kwa vile Paulo alikuwa amekusudia kuondoka
kesho yake, aliwahutubia watu na kuendelea kuongea nao hadi usiku wa manane.
8 Katika
chumba tulimokuwa, ghorofani, kulikuwa na taa nyingi zinawaka.
9 Kijana
mmoja aitwaye Eutuko alikuwa ameketi dirishani wakati Paulo alipokuwa
anaendelea kuhutubu. Eutuko alianza kusinzia kidogokidogo na hatimaye usingizi
ukambana, akaanguka chini kutoka ghorofa ya tatu. Wakamwokota amekwisha kufa.
10 Lakini
Paulo alishuka chini, akainama, akamkumbatia na kusema, "Msiwe na wasiwasi
maana kuna uhai bado ndani yake."
11 Kisha
akapanda tena ghorofani, akamega mkate, akala. Aliendelea kuhubiri kwa muda
mrefu hadi alfajiri, halafu akaondoka.
12 Wale
watu walimchukua yule kijana nyumbani akiwa mzima kabisa, wakapata kitulizo
kikubwa.
13 Sisi
tulipanda meli tukatangulia kwenda Aso ambako tungemchukua Paulo. Ndivyo
alivyopanga; maana alitaka kufika huko kwa kupitia nchi kavu.
14 Basi, alitukuta kule Aso, tukampandisha melini, tukaenda
Mitulene.
15 Kutoka huko tulisafiri tukafika Kio kesho yake. Siku ya
pili, tulitia nanga Samo na kesho yake tukafika Mileto.
16 Paulo alikuwa amekusudia kuendelea na safari kwa meli
bila kupitia Efeso ili asikawie zaidi huko Asia. Alikuwa na haraka ya kufika
Yerusalemu kwa sikukuu ya Pentekoste kama ingewezekana.
17 Kutoka Mileto Paulo alituma ujumbe kwa wazee wa Efeso
wakutane naye.
18 Walipofika kwake aliwaambia, "Mnajua jinsi
nilivyotumia wakati wote pamoja nanyi tangu siku ile ya kwanza nilipofika Asia.
19 Mnajua jinsi nilivyomtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote,
kwa machozi na matatizo yaliyonipata kutokana na mipango ya hila ya Wayahudi.
20 Mnajua kwamba sikusita hata kidogo kuwahubiria hadharani
na nyumbani mwenu na kuwafundisha chochote ambacho kingewasaidieni.
21 Niliwaonya wote - Wayahudi kadhalika na watu wa mataifa,
wamgeukie Mungu na kumwamini Bwana wetu Yesu.
22 Sasa, sikilizeni! Mimi, nikiwa ninamtii Roho, nakwenda
Yerusalemu bila kufahamu yatakayonipata huko.
23 Ninachojua tu ni kwamba Roho Mtakatifu ananithibitishia
katika kila mji kwamba vifungo na mateso ndivyo vinavyoningojea.
24 Lakini, siuthamini uhai wangu kuwa ni kitu sana kwangu.
Nataka tu nikamilishe ule utume wangu na kumaliza ile kazi aliyonipa Bwana Yesu
niifanye, yaani nitangaze Habari Njema ya neema ya Mungu.
25 "Nimekuwa nikienda huko na huko kati yenu
nikiuhubiri Ufalme wa Mungu. Sasa lakini, najua hakuna hata mmoja wenu
atakayeniona tena.
26 Hivyo, leo hii ninawathibitishieni rasmi kwamba
ikijatokea akapotea mmoja wenu, mimi sina lawama yoyote.
27 Kwa maana sikusita hata kidogo kuwatangazieni azimio
lote la Mungu.
28 Jihadharini wenyewe; lilindeni lile kundi ambalo Roho
Mtakatifu amewaweka ninyi muwe walezi wake. Lichungeni kanisa la Mungu ambalo
amejipatia kwa damu ya Mwanae.
29 Nafahamu vizuri sana kwamba baada ya kuondoka kwangu
mbwa mwitu wakali watawavamieni, na hawatakuwa na huruma kwa kundi hilo.
30 Hata kutoka miongoni mwenu watatokea watu ambao watasema
mambo ya uongo ili kuwapotosha watu na kuwafanya wawafuate wao tu.
31 Kwa hiyo, muwe macho mkikumbuka kwamba kwa muda wa miaka
mitatu, usiku na mchana, sikuchoka kumwonya kila mmoja wenu kwa machozi.
32 "Na sasa basi, ninawaweka ninyi chini ya ulinzi wa
Mungu na ujumbe wa neema yake. Yeye anao uwezo wa kuwajenga ninyi na
kuwawezesha mzipate zile baraka alizowawekea watu wake.
33 Mimi sikutamani hata mara moja fedha, wala dhahabu, wala
nguo za mtu yeyote.
34 Mnajua ninyi wenyewe kwamba nimefanya kazi kwa mikono
yangu mwenyewe, ili kujipatia mahitaji yangu na ya wenzangu.
35 Nimekuwa nikiwapeni daima mfano kwamba kwa kufanya kazi
mithili hiyo tunapaswa kuwasaidia walio dhaifu, tukikumbuka maneno ya Bwana
Yesu mwenyewe: `Heri zaidi kutoa kuliko kupokea."`
36 Baada ya kusema hayo, Paulo alipiga magoti pamoja nao
wote, akasali.
37 Wote
walikuwa wanalia; wakamwaga kwa kumkumbatia na kumbusu.
38 Jambo
lililowahuzunisha zaidi lilikuwa neno alilosema kwamba hawangemwona tena. Basi,
wakamsindikiza hadi melini.
|