Chapter 22
1 "Ndugu zangu na akina baba, nisikilizeni sasa
nikijitetea mbele yenu!"
2 Waliposikia akiongea nao kwa Kiebrania wakazidi kukaa
kimya zaidi kuliko hapo awali. Naye Paulo akaendelea kusema,
3 "Mimi ni Myahudi, mzaliwa wa Tarso katika Kilikia.
Lakini nililelewa papa hapa mjini Yerusalemu chini ya mkufunzi Gamalieli.
Nilifundishwa kufuata kwa uthabiti Sheria ya wazee wetu. Nilijitolea kwa moyo
wote kwa Mungu kama ninyi wenyewe mlivyo hivi leo.
4 Niliwatesa hata kuwaua wale watu waliofuata Njia hii.
Niliwatia nguvuni wanaume kwa wanawake na kuwafunga gerezani.
5 Kuhani Mkuu na baraza lote la wazee wanaweza kushuhudia
jambo hilo. Kutoka kwao nilipokea barua walioandikiwa wale ndugu Wayahudi
waliokuwa huko Damasko. Nilikwenda Damasko ili niwatie nguvuni watu hao na
kuwaleta wamefungwa mpaka Yerusalemu ili waadhibiwe.
6 "Basi, nilipokuwa njiani karibu kufika Damasko,
yapata saa sita mchana, mwangu mkubwa kutoka mbinguni ulitokea ghafla
ukaniangazia pande zote.
7 Hapo nilianguka chini, nikasikia sauti ikiniambia:
`Saulo, Saulo! Kwa nini unanitesa?`
8 Nami nikauliza: `Nani wewe, Bwana?` Naye akaniambia:
`Mimi ni Yesu wa Nazareti ambaye wewe unamtesa.`
9 Wale wenzangu waliuona ule mwanga lakini hawakusikia
sauti ya yule aliyeongea nami.
10 Basi, mimi nikauliza: `Nifanye nini Bwana?` Naye Bwana
akaniambia: `Simama, nenda Damasko na huko utaambiwa yote ambayo umepangiwa
kufanya.`
11 Kutokana na ule mwanga mkali sikuweza kuona na hivyo
iliwabidi wale wenzangu kuniongoza kwa kunishika mkono mpaka nikafika Damasko.
12 "Huko kulikuwa na mtu mmoja aitwaye Anania, mtu
mcha Mungu, mwenye kuitii Sheria yetu na aliyeheshimika sana mbele ya Wayahudi
waliokuwa wanaishi Damasko.
13 Yeye alikuja kuniona, akasimama karibu nami, akasema:
`Ndugu Saulo! Ona tena.` Papo hapo nikaona tena, nikamwangalia.
14 Halafu Anania akasema: `Mungu wa babu zetu amekuchagua
upate kujua matakwa yake na kumwona yule mtumishi wake mwadilifu na kumsikia
yeye mwenyewe akiongea.
15 Kwa maana utamshuhudia kwa watu wote ukiwaambia yale
uliyoyaona na kuyasikia.
16 Sasa basi, ya nini kukawia zaidi? Simama ubatizwe na
uondolewe dhambi zako kwa kuliungama jina lake.`
17 "Basi, nilirudi Yerusalemu, na nilipokuwa nikisali
Hekaluni, niliona maono.
18 Nilimwona Bwana akiniambia: `Haraka! Ondoka Yerusalemu
upesi kwa maana watu wa hapa binadamu hawataukubali ushuhuda wako juu yangu.`
19 Nami nikamjibu: `Bwana, wao wanajua wazi kwamba mimi ni
yule aliyekuwa anapitapita katika masunagogi na kuwatia nguvuni na kuwapiga
wale waliokuwa wanakuamini.
20 Na kwamba wakati shahidi wako Stefano alipouawa, mimi
binafsi nilikuwako pale nikakubaliana na kitendo hicho na kuyalinda makoti ya
wale waliokuwa wanamuua.`
21 Naye Bwana akaniambia: `Nenda; ninakutuma mbali kwa
mataifa mengine."`
22 Mpaka hapa, wale watu walikuwa wanamsikiza, lakini
aliposema maneno haya, walianza kusema kwa sauti kubwa, "Mwondoe duniani!
Mtu wa namna hiyo hastahili kuishi."
23 Waliendelea kupayukapayuka huku wakitikisa makoti yao na
kurusha vumbi angani.
24 Mkuu wa jeshi aliwaamuru watu wake wampeleke Paulo ndani
ya ngome, akawaambia wamchape viboko ili wapate kujua kisa cha Wayahudi
kumpigia kelele.
25 Lakini walipokwisha mfunga ili wamchape viboko, Paulo
alimwuliza jemadari mmoja aliyesimama hapo, "Je, ni halali kwenu kumpiga
viboko raia wa Roma kabla hajahukumiwa?"
26 Yule jemadari aliposikia hayo, alimpasha habari mkuu wa
jeshi akisema, "Unataka kufanya nini? Mtu huyu ni raia wa Roma!"
27 Basi, mkuu wa jeshi alimwendea Paulo, akamwambia,
"Niambie; je, wewe ni raia wa Roma?" Paulo akamjibu,
"Naam."
28 Mkuu wa jeshi akasema, "Mimi nami nimekuwa raia wa
Roma kwa kulipa gharama kubwa." Paulo akasema, "Lakini mimi ni raia
wa Roma kwa kuzaliwa."
29 Wale watu ambao walikuwa tayari kumchunguza Paulo
walitoweka mara. Hata yule mkuu wa jeshi aliogopa alipojua kwamba Paulo ni raia
wa Roma na kwamba alikuwa amekwisha mfunga minyororo.
|