Chapter 23
1 Paulo aliwakodolea macho wale wanabaraza, halafu akaanza
kusema, "Ndugu zangu, mpaka hivi leo nimekuwa nikiishi na dhamiri njema
mbele ya Mungu."
2 Hapo Kuhani Mkuu Anania akaamuru wale waliokuwa
wamesimama karibu na Paulo wampige kofi mdomoni.
3 Basi, Paulo akamwambia, "Mungu mwenyewe atakupiga
kofi wewe uliye kama ukuta uliopakwa chokaa! Unawezaje kukaa hapo ili unihukumu
kisheria na huku wewe mwenyewe unaivunja Sheria kwa kuamuru nipigwe?"
4 Watu waliokuwa wamesimama pale wakamwambia Paulo,
"Unamtukana Kuhani Mkuu wa Mungu!"
5 Paulo akajibu, "Ndugu zangu, sikujua kama yeye ni
Kuhani Mkuu. Maana Maandiko yasema hivi: `Usiseme vibaya juu ya mtawala wa watu
wako."`
6 Wakati huo Paulo alikwisha tambua kwamba sehemu moja ya
wanabaraza wale ilikuwa ni Masadukayo na nyingine Mafarisayo. Basi, alipaaza
sauti yake mbele ya Baraza: "Ndugu zangu, mimi ni Mfarisayo, mwana wa
Mfarisayo. Mimi nimeletwa mahakamani kwa kuwa ninatumaini kwamba wafu
watafufuka."
7 Baada ya kusema hivyo, mzozo mkali ulitokea kati ya
Mafarisayo na Masadukayo na mkutano ukagawanyika sehemu mbili.
8 Kisa chenyewe kilikuwa hiki: Masadukayo hushikilia kwamba
wafu hawafufuki, hakuna malaika, na roho nazo hazipo. Lakini Mafarisayo
husadiki hayo yote matatu.
9 Kelele ziliongezeka na baadhi ya walimu wa Sheria wa
kikundi cha Mafarisayo walisimama na kutoa malalamiko yao kwa nguvu:
"Hatuoni chochote kilicho kiovu katika mtu huyu; huenda ikawa kwamba roho
au malaika ameongea naye."
10 Mzozo ulizidi kuwa mwingi hata mkuu wa jeshi akaogopa
kwamba Paulo angeraruliwa vipandevipande. Kwa hiyo, aliwaamuru askari wake
kuingia kati ya lile kundi, wamtoe Paulo na kumrudisha ndani ya ngome.
11 Usiku uliofuata, Bwana alisimama karibu na Paulo,
akamwambia, "Jipe moyo! Umenishuhudia katika Yerusalemu, utafanya vivyo
hivyo mjini Roma."
12 Kulipokucha, Wayahudi walifanya kikao cha faragha.
Wakala kiapo: "Hatutakula wala kunywa mpaka tutakapokuwa tumekwisha muua
Paulo."
13 Watu zaidi ya arobaini ndio waliokula njama kufanya
hivyo.
14 Basi, walikwenda kwa makuhani wakuu na wazee, wakasema,
"Sisi tumeapa kwamba hatutaonja chochote kwa vinywa vyetu mpaka hapo
tutakapokuwa tumemuua Paulo.
15 Sasa basi, ninyi pamoja na Baraza tumeni ujumbe kwa mkuu
wa jeshi ili amlete Paulo kwenu mkijisingizia kwamba mnataka kupata habari
kamili zaidi juu yake. Tuko tayari kumuua hata kabla hajafika karibu."
16 Lakini mtoto wa kiume wa dada yake Paulo alisikia juu ya
mpango huo; hivyo akaenda ndani ya ngome, akamjulisha Paulo juu ya njama hiyo.
17 Hapo Paulo akamwita mmoja wa askari, akamwambia,
"Mchukue kijana huyu kwa mkuu wa jeshi; ana kitu cha kumwambia."
18 Askari akamchukua huyo kijana, akamwongoza mpaka kwa
mkuu wa jeshi, akasema, "Yule mfungwa Paulo ameniita akaniomba nimlete
kijana huyu kwako kwa maana ana jambo la kukwambia."
19 Mkuu wa jeshi alimshika huyo kijana mkono, akampeleka
mahali pa faragha, akamwuliza, "Una nini cha kuniambia?"
20 Yeye akasema, "Wayahudi wamepatana wakuombe
umpeleke Paulo Barazani wakijisingizia kwamba Baraza lingependa kupata habari
kamili zaidi juu yake.
21 Lakini wewe usikubali kwa maana kuna watu zaidi ya
arobaini walio tayari kumvamia. Wameapa kutokula wala kunywa mpaka watakapokuwa
wamemuua. Sasa wako tayari, wanangojea tu uamuzi wako."
22 Mkuu wa jeshi alimwacha aende zake akimwonya asimwambie
mtu yeyote kwamba amemletea habari hizo.
23 Basi, mkuu wa jeshi aliwaita askari wawili akawaambia,
"Wekeni tayari askari mia mbili, wapanda farasi sabini na askari mia mbili
wa mikuki, waende Kaisarea; muwe tayari kuondoka kabla ya saa tatu leo usiku.
24 Wekeni farasi kadhaa kwa ajili ya Paulo; mfikisheni
salama kwa Felisi, mkuu wa mkoa."
25 Halafu mkuu huyo wa jeshi akaandika barua hivi:
26 "Mimi Klaudio Lusia ninakuandikia wewe Mheshimiwa
Felisi, mkuu wa mkoa. Salamu!
27 "Wayahudi walimkamata mtu huyu na karibu wangemuua
kama nisingalifahamishwa kwamba yeye ni raia wa Roma na hivyo nikaenda pamoja
na askari nikamwokoa.
28 Nilimpeleka mbele ya Baraza lao kuu nikitaka kujua kisa
cha mashtaka yao.
29 Niligundua kwamba mashtaka yenyewe yalihusu ubishi juu
ya sehemu kadha wa kadha za Sheria yao na hivyo sikuona kwamba amefanya
chochote kinachostahili auawe au afungwe gerezani.
30 Nilipofahamishwa kwamba Wayahudi walikuwa wamefanya
njama za kumuua, niliamua kumleta kwako. Nikamwambia washtaki wake walete
mashtaka yao mbele yako."
31 Basi, hao askari walimchukua Paulo kama walivyoamriwa;
wakampeleka usiku uleule mpaka Antipatri.
32 Kesho yake askari wa miguu walirudi ngomeni, wakawaacha
wale askari wapanda farasi waendelee na safari pamoja na Paulo.
33 Walipofika Kaisarea walimpa mkuu wa mkoa ile barua na
kumweka Paulo chini ya mamlaka yake.
34 Felisi alipoisoma hiyo barua aliwauliza Paulo ametoka
mkoa gani. Alipofahamishwa kwamba alikuwa ametoka mkoa wa Kilikia,
35 akasema, "Nitasikiliza kesi yako baada ya washtaki
wako kufika." Kisha akaamuru Paulo awekwe chini ya ulinzi ndani ya ukumbi
wa Herode.
|