Chapter 26
1 Basi,
Agripa akamwambia Paulo, "Unaruhusiwa kujitetea." Hapo Paulo
alinyosha mkono wake akajitetea hivi:
2
"Mfalme Agripa, ninajiona mwenye bahati leo kujitetea mbele yako kuhusu
yale mashtaka yote ambayo Wayahudi walikuwa wamesema juu yangu.
3 Hasa kwa
vile wewe mwenyewe ni mtaalamu wa desturi za Wayahudi na migogoro yao,
ninakuomba basi unisikilize kwa uvumilivu.
4
"Wayahudi wanajua habari za maisha yangu tangu utoto, jinsi nilivyoishi tangu
mwanzo kati ya taifa langu huko Yerusalemu.
5
Wananifahamu kwa muda mrefu, na wanaweza kushuhudia, kama wakipenda, kwamba
tangu mwanzo niliishi kama mmoja wa kikundi chenye siasa kali zaidi katika dini
yetu, yaani kikundi cha Mafarisayo.
6 Na sasa
niko hapa nihukumiwe kwa sababu ninaitumainia ile ahadi ambayo Mungu
aliwaahidia babu zetu.
7 Ahadi
hiyo ndiyo ileile inayotumainiwa na makabila kumi na mawili ya taifa letu,
wakimtumikia Mungu kwa dhati mchana na usiku. Mheshimiwa mfalme, Wayahudi
wananishtaki kwa sababu ya tumaini hilo!
8 Kwa nini
ninyi mnaona shida sana kuamini kwamba Mungu huwafufua wafu?
9 Kwa
kweli mimi mwenyewe niliamini kwamba ni wajibu wangu kufanya mambo mengi
kulipinga jina la Yesu wa Nazareti.
10 Mambo
hayo ndiyo niliyoyafanya huko Yerusalemu. Mimi binafsi, nikiwa nimepewa mamlaka
kutoka kwa makuhani wakuu, nilipata kuwatia gerezani wengi wa watu wa Mungu.
Nao walipohukumiwa kuuawa, nilipiga kura ya kukubali.
11 Mara
nyingi niliwafanya waadhibiwe katika masunagogi yote nikiwashurutisha waikane
imani yao. Hasira yangu kwao ilikuwa kubwa hata nikawasaka mpaka miji ya mbali.
12
"Kwa mujibu huohuo, nilikwenda Damasko wakati mmoja, nikiwa na mamlaka na
maagizo kutoka kwa makuhani wakuu.
13
Mheshimiwa, wakati nilipokuwa njiani, saa sita mchana, niliona mwanga mkubwa
kuliko wa jua ukiangaza kutoka mbinguni, ukanizunguka mimi na wale wasafiri
wenzangu.
14 Sisi sote tulianguka chini, nami nikasikia sauti
ikiniambia kwa Kiebrania: `Saulo, Saulo! Kwa nini unanitesa? Unajiumiza bure
kama punda anayepiga teke fimbo ya bwana wake.`
15 Mimi nikauliza: `Ni nani wewe Bwana?` Naye Bwana
akajibu: `Mimi ni Yesu ambaye wewe unamtesa.
16 Haidhuru, inuka sasa; simama wima. Nimekutokea ili
nikuweke rasmi kuwa mtumishi wangu. Utawathibitishia watu wengine mambo
uliyoyaona leo na yale ambayo bado nitakuonyesha.
17 Nitakuokoa na watu wa Israeli na watu wa mataifa mengine
ambao mimi ninakutuma kwao.
18 Utayafumbua macho yao na kuwawezesha watoke gizani na
kuingia katika mwanga; watoke katika utawala wa Shetani, wamgeukie Mungu; ili
kwa kuamini, wapate kusamehewa dhambi na kuchukua nafasi yao kati ya wale ambao
wamepata kuwa watu wa Mungu.`
19 "Hivyo, mfalme Agripa, sikuweza kuwa mkaidi kwa
maono hilo la mbinguni.
20 Ila nilianza kuhubiri kwanza kwa watu wa Damasko, halafu
kwa wale wa Yerusalemu na nchi yote ya Yudea, na pia kwa watu wa mataifa
mengine. Niliwahimiza wamgeukie Mungu na kuonyesha kwa vitendo kwamba
wamebadilisha mioyo yao.
21 Kwa sababu hiyo, Wayahudi walinikamata nikiwa Hekaluni,
wakajaribu kuniua.
22 Lakini Mungu alinisaidia; na hivyo mpaka siku ya leo
nimesimama imara nikitoa ushuhuda kwa wote, wakubwa na wadogo. Ninayosema ni
yale ambayo manabii na Mose walisema yatatukia;
23 yaani ilimpasa Kristo ateseke na kuwa wa kwanza kufufuka
kutoka wafu, ili atangaze kwamba mwanga wa ukombozi unawaangazia sasa watu
wote, Wayahudi na pia watu wa mataifa mengine."
24 Paulo alipofika hapa katika kujitetea kwake, Festo
alisema kwa sauti kubwa, "Paulo! Una wazimu! Kusoma kwako kwingi kunakutia
wazimu!"
25 Lakini Paulo akasema, "Sina wazimu mheshimiwa
Festo: Ninachosema ni ukweli mtupu.
26 Wewe Mfalme unayafahamu mambo haya, kwa hiyo ninaweza
kuongea bila uoga mbele yako. Sina mashaka kwamba matukio hayo yanajulikana
kwako maana jambo hili halikutendeka mafichoni.
27 Mfalme Agripa, je, una imani na manabii? Najua kwamba
unaamini."
28 Agripa akamjibu Paulo, "Kidogo tu utanifanya
Mkristo!"
29 Paulo akamjibu, "Namwomba Mungu kwamba, kwa muda
mfupi au mrefu, si wewe tu bali wote wanaonisikia leo wapate kuwa kama nilivyo
mimi, lakini bila hii minyororo."
30 Hapo mfalme Agripa, mkuu wa mkoa, Bernike na wale wote
waliokuwa pamoja nao, walisimama.
31 Walipokwisha ondoka, waliambiana, "Mtu huyu
hakufanya chochote kinachostahili adhabu ya kifo au kifungo."
32 Naye Agripa akamwambia Festo, "Mtu huyu angeweza
kufunguliwa kama asingalikuwa amekata rufani kwa Kaisari."
|