Chapter 27
1 Walipokwisha amua tusafiri mpaka Italia, walimweka Paulo
pamoja na wafungwa wengine chini ya ulinzi wa Yulio aliyekuwa ofisa wa jeshi
katika kikosi kiitwacho "Kikosi cha Augusto."
2 Tulipanda meli ya Adiramito iliyokuwa inasafiri na
kupitia bandari kadhaa za mkoa wa Asia, tukaanza safari. Aristarko, mwenyeji wa
Makedonia kutoka Thesalonika, alikuwa pamoja nasi.
3 Kesho yake tulitia nanga katika bandari ya Sidoni. Yulio
alimtendea Paulo vizuri kwa kumruhusu awaone rafiki zake na kupata mahitaji
yake.
4 Kutoka huko tuliendelea na safari, lakini kwa kuwa upepo
ulikuwa unavuma kwa kasi kutujia kwa mbele, tulipitia upande wa kisiwa cha
Kupro ambapo upepo haukuwa mwingi.
5 Halafu tulivuka bahari ya Kilikia na Pamfulia, tukatia
nanga Mura, mji wa Lukia.
6 Hapo yule ofisa alikuta meli moja ya Aleksandria
iliyokuwa inakwenda Italia, na hivyo akatupandisha ndani.
7 Kwa muda wa siku nyingi tulisafiri polepole, na kwa shida
tulifika karibu na Nido. Kwa sababu upepo ulikuwa bado unatupinga, tuliendelea
mbele moja kwa moja tukapitia upande wa Krete karibu na rasi Salmone ambapo
upepo haukuwa mwingi.
8 Tulipita kando yake polepole tukafika mahali paitwapo
"Bandari Nzuri", karibu na mji wa Lasea.
9 Muda mrefu ulikuwa umepita, na hata siku ya kufunga
ilikuwa imekwisha pita. Sasa ilikuwa hatari sana kusafiri kwa meli. Basi, Paulo
aliwapa onyo:
10 "Waheshimiwa, nahisi kwamba safari hii itakuwa ya
shida na hasara nyingi si kwa shehena na meli tu, bali pia kwa maisha yetu."
11 Lakini yule ofisa alivutiwa zaidi na maoni ya nahodha na
ya mwenye meli kuliko yale aliyosema Paulo.
12 Kwa kuwa bandari hiyo haikuwa mahali pazuri pa kukaa wakati
wa baridi, wengi walipendelea kuendelea na safari, ikiwezekana mpaka Foinike.
Foinike ni bandari ya Krete inayoelekea kusini-magharibi na
kaskazini-magharibi; na huko wangeweza kukaa wakati wa baridi.
13 Basi, upepo mzuri wa kusi ulianza kuvuma, nao wakadhani
wamefanikiwa lengo lao; hivyo wakang`oa nanga, wakaiendesha meli karibu sana na
pwani ya Krete.
14 Lakini haukupita muda, upepo mkali uitwao "Upepo wa
Kaskazi" ulianza kuvuma kutoka kisiwani.
15 Upepo uliipiga ile meli, na kwa kuwa hatukuweza
kuukabili, tukaiacha ikokotwe na huo upepo.
16 Kisiwa kimoja kiitwacho Kanda kilitukinga kidogo na ule
upepo; na tulipopita kusini mwake tulifaulu, ingawa kwa shida, kuusalimisha ule
mtumbwi wa meli.
17 Wale wanamaji waliuvuta mtumbwi ndani, kisha
wakaizungushia meli kamba na kuifunga kwa nguvu. Waliogopa kwamba wangeweza
kukwama kwenye ufuko wa bahari, pwani ya Libya. Kwa hiyo walishusha matanga na kuiacha meli
ikokotwe na upepo.
18 Dhoruba
iliendelea kuvuma na kesho yake wakaanza kutupa nje shehena ya meli.
19 Siku ya
tatu, wakaanza pia kutupa majini vifaa vya meli kwa mikono yao wenyewe.
20 Kwa
muda wa siku nyingi hatukuweza kuona jua wala nyota; dhoruba iliendelea kuvuma
sana, hata matumaini yote ya kuokoka yakatuishia.
21 Baada
ya kukaa muda mrefu bila kula chakula, Paulo alisimama kati yao, akasema,
"Waheshimiwa, ingalikuwa afadhali kama mngalinisikiliza na kuacha kusafiri
kutoka Krete. Kama mngalifanya hivyo tungaliiepuka shida hii na hasara hizi
zote.
22 Lakini
sasa ninawaombeni muwe na moyo; hakuna hata mmoja wenu atakayepoteza maisha
yake; meli tu ndiyo itakayopotea.
23 Kwa
maana jana usiku malaika wa yule Mungu ambaye mimi ni wake na ambaye mimi
ninamwabudu alinitokea,
24 akaniambia: `Paulo usiogope! Ni lazima utasimama mbele
ya Kaisari; naye Mungu, kwa wema wake, amekufadhili kwa kuwaokoa wote wanaosafiri
nawe wasiangamie.`
25 Hivyo, waheshimiwa, jipeni moyo! Maana ninamwamini Mungu
kwamba itakuwa sawa kama nilivyoambiwa.
26 Lakini ni lazima tutatupwa ufukoni mwa kisiwa
fulani."
27 Usiku wa siku ya kumi na nne, tulikuwa tunakokotwa huku
na huku katika bahari ya Adria. Karibu na usiku wa manane wanamaji walijihisi
kuwa karibu na nchi kavu.
28 Hivyo walitafuta kina cha bahari kwa kuteremsha kamba
iliyokuwa imefungiwa kitu kizito, wakapata kina cha mita arobaini. Baadaye
wakapima tena wakapata mita thelathini.
29 Kwa sababu ya kuogopa kukwama kwenye miamba,
waliteremsha nanga nne nyuma ya meli; wakaomba kuche upesi.
30 Wanamaji walitaka kutoroka, na walikwisha kuteremsha ule
mtumbwi majini, wakijisingizia kwamba wanakwenda kuteremsha nanga upande wa
mbele wa meli.
31 Lakini Paulo alimwambia yule ofisa wa jeshi na askari
wake, "Kama wanamaji hawa hawabaki ndani ya meli, hamtaokoka."
32 Hapo wale askari walizikata kamba zilizokuwa
zimeshikilia ule mtumbwi, wakauacha uchukuliwe na maji.
33 Karibu na alfajiri, Paulo aliwahimiza wote wale chakula:
"Kwa siku kumi na nne sasa mmekuwa katika mashaka na bila kula; hamjala
kitu chochote.
34 Basi, ninawasihi mle chakula kwa maana mnakihitaji ili
mweze kuendelea kuishi. Maana hata unywele mmoja wa vichwa vyenu
hautapotea."
35 Baada ya kusema hivyo, Paulo alichukua mkate,
akamshukuru Mungu mbele yao wote, akaumega, akaanza kula.
36 Hapo wote wakapata moyo, nao pia wakala chakula.
37 Jumla tulikuwa watu mia mbili na sabini na sita katika
meli.
38 Baada ya kila mmoja kula chakula cha kutosha,
walipunguza uzito wa meli kwa kutupa nafaka baharini.
39 Kulipokucha, wanamaji hawakuweza kuitambua nchi ile, ila
waliona ghuba moja yenye ufuko; wakaamua kutia nanga huko kama ikiwezekana.
40 Hivyo walikata nanga na kuziacha baharini, na wakati
huohuo wakazifungua kamba zilizokuwa zimeufunga usukani, kisha wakatweka tanga
moja mbele kushika upepo, wakaelekea ufukoni.
41 Lakini walifika mahali ambapo mikondo miwili ya bahari
hukutana, na meli ikakwama. Sehemu ya mbele ilikuwa imezama mchangani bila
kutikisika. Sehemu ya nyuma ya meli ilianza kuvunjika vipandevipande kwa mapigo
ya nguvu ya mawimbi.
42 Askari walitaka kuwaua wafungwa wote kwa kuogopa kwamba
wangeogelea hadi pwani na kutoroka.
43 Lakini kwa vile yule ofisajeshi alitaka kumwokoa Paulo,
aliwazuia wasifanye hivyo. Aliamuru wale waliojua kuogelea waruke kutoka melini
na kuogelea hadi pwani,
44 na wengine wafuate wakijishikilia kwenye mbao au kwenye
vipande vya meli iliyovunjika. Ndivyo sisi sote tulivyofika salama pwani.
|