Chapter 28
1 Tulipokwisha fika salama kwenye nchi kavu, tuligundua
kwamba kile kisiwa kinaitwa Malta.
2 Wenyeji wa hapo walikuwa wema sana kwetu. Mvua ilikuwa
inaanza kunyesha na kulikuwa na baridi, hivyo waliwasha moto, wakatukaribisha.
3 Paulo aliokota mzigo mdogo wa kuni akawa anazitia motoni.
Hapo, kwa sababu ya lile joto la moto, nyoka akatoka katika kuni akamnasa Paulo
mkononi na kujishikilia hapo.
4 Wenyeji wa pale walipokiona kile kiumbe kinaning`inia
kwenye mkono wake waliambiana, "Bila shaka mtu huyu amekwisha ua mtu, na
ingawa ameokoka kuangamia baharini, `Haki` haitamwacha aendelee kuishi!"
5 Lakini Paulo alikikung`utia kile kiumbe motoni na
hakuumizwa hata kidogo.
6 Wale watu walikuwa wakitazamia kwamba angevimba au
hapohapo angeanguka chini na kufa. Baada ya kungojea kwa muda mrefu bila kuona
kwamba Paulo amepatwa na jambo lolote lisilo la kawaida, walibadilisha fikira
zao juu yake, wakasema kuwa ni mungu.
7 Karibu na mahali pale palikuwa na mashamba ya Publio,
mkuu wa kile kisiwa. Publio alitukaribisha kirafiki, tukawa wageni wake kwa
siku tatu.
8 Basi, ikawa kwamba baba yake Publio alikuwa amelala
kitandani, mgonjwa, ana homa na kuhara. Paulo alikwenda kumwona na baada ya
kusali, akaweka mikono yake juu ya mgonjwa, akamponya.
9 Kutokana na tukio hilo, wagonjwa wote katika kile kisiwa
walikuja wakaponywa.
10 Watu walitupatia zawadi mbalimbali na wakati tulipoanza
tena safari, walitia ndani ya meli masurufu tuliyohitaji.
11 Baada ya miezi mitatu tulianza tena safari yetu kwa meli
moja ya Aleksandria iitwayo "Miungu Pacha". Meli hiyo ilikuwa imetia
nanga kisiwani wakati wote wa baridi.
12 Tulifika katika mji wa Sirakusa, tukakaa hapo kwa siku
tatu.
13 Toka huko tuling`oa nanga, tukazunguka na kufika Regio.
Baada ya siku moja, upepo ulianza kuvuma kutoka kusini, na baada ya siku mbili
tulifika bandari ya Potioli.
14 Huko tuliwakuta ndugu kadhaa ambao walituomba tukae nao
kwa juma moja. Hivi ndivyo tulivyopata kufika Roma.
15 Ndugu wa kule Roma walipopata habari zetu, wakaja
kutulaki kwenye soko la Apio na Mikahawa Mitatu. Paulo alipowaona alimshukuru
Mungu, akapata moyo.
16 Tulipofika Roma, Paulo aliruhusiwa kukaa peke yake
pamoja na askari mmoja wa kumlinda. ic
17 Baada ya siku tatu, Paulo aliwaita pamoja viongozi wa
Kiyahudi wa mahali hapo. Walipokusanyika, Paulo aliwaambia, "Wananchi
wenzangu, mimi, ingawa sikufanya chochote kibaya wala kupinga desturi za wazee
wetu, nilitiwa nguvuni kule Yerusalemu na kutiwa mikononi mwa Waroma.
18 Waliponihoji na kuona kwamba sikuwa na hatia yeyote,
walitaka kuniacha.
19 Lakini Wayahudi wengine walipinga jambo hilo, nami
nikalazimika kukata rufani kwa Kaisari, ingawa sikuwa na chochote cha
kuwashtaki wananchi wenzangu.
20 Ni kwa sababu hiyo nimeomba kuonana na kuongea nanyi,
maana nimefungwa minyororo hii kwa sababu ya tumaini lile la Israeli."
21 Wao wakamwambia, "Sisi hatujapokea barua yoyote
kutoka Yudea, wala hakuna ndugu yeyote aliyefika hapa na kutoa habari rasmi au
kusema chochote kibaya juu yako.
22 Lakini tunafikiri inafaa tusikie kutoka kwako mwenyewe
mambo yaliyo kichwani mwako. Kwa maana tujualo sisi kuhusu hicho kikundi ni
kwamba kinapingwa kila mahali."
23 Basi, walipanga naye siku kamili ya kukutana, na wengi
wakafika huko alikokuwa anakaa. Tangu asubuhi mpaka jioni Paulo aliwaeleza na
kuwafafanulia juu ya Ufalme wa Mungu akijaribu kuwafanya wakubali habari juu ya
Yesu kwa kutumia Sheria ya Mose na maandiko ya manabii.
24 Baadhi yao walikubali maneno yake, lakini wengine
hawakuamini.
25 Basi, kukawa na mtengano wa fikira kati yao. Walipokuwa
wanakwenda zao, Paulo alisema jambo hili, "Kweli ni sawa yale aliyoyanena
Roho Mtakatifu kwa wazee wenu kwa njia ya nabii Isaya
26 akisema: `Nenda kwa watu hawa ukawaambie: kusikia
mtasikia, lakini hamtaelewa; kutazama mtatazama, lakini hamtaona.
27 Maana akili za watu hawa zimepumbaa, wameziba masikio
yao, wamefumba macho yao. La sivyo, wangeona kwa macho yao, wangesikia kwa
masikio yao. Wangeelewa kwa akili zao, na kunigeukia, asema Bwana, nami
ningewaponya."`
28 Halafu Paulo akamaliza na kusema, "Jueni basi,
kwamba ujumbe wa Mungu juu ya wokovu umepelekwa kwa watu wa mataifa. Wao
watasikiliza!"*fd* walijiondokea huku wakiwa wanabishana vikali wao kwa
wao.
29 missing
30 Kwa muda wa miaka miwili mizima Paulo aliishi katika
nyumba aliyoipanga yeye mwenyewe; akawa anawakaribisha wote waliofika
kumsalimu.
31 Alikuwa akihubiri Ufalme wa Mungu na kufundisha juu ya
Bwana Yesu Kristo kwa uhodari, bila kizuizi.
|