Romans
Chapter 1
1 Kutoka kwangu mimi Paulo, mtumishi wa Kristo Yesu, na
mtume niliyeteuliwa na kuitwa kwa ajili ya kuhubiri Habari Njema ya Mungu.
2 Hapo kale, Mungu aliwaahidia watu hii Habari Njema kwa
njia ya manabii wake katika Maandiko Matakatifu.
3 Hii Habari Njema inamhusu Mwana wa Mungu, Bwana wetu Yesu
Kristo, ambaye mintarafu ubinadamu wake, alikuwa mzawa wa Daudi;
4 mintarafu utakatifu wake wa kimungu, alithibitishwa kwa
uwezo mkuu kwamba ni Mwana wa Mungu kwa kufufuliwa kutoka wafu.
5 Kwa njia yake, mimi nimepewa neema ya kuwa mtume, ili kwa
ajili yake niwaongoze watu wa mataifa yote wapate kuamini na kutii.
6 Ninyi ni miongoni mwa watu hao; mmeitwa muwe watu wake
Yesu Kristo.
7 Basi, ninawaandikia ninyi nyote mlioko Roma ambao Mungu
anawapenda, akawateua muwe watu wake. Nawatakieni neema na amani kutoka kwa
Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.
8 Awali ya yote, namshukuru Mungu wangu kwa njia ya Yesu
Kristo kwa ajili yenu nyote, kwa sababu imani yenu inasikika duniani kote.
9 Mungu, ambaye ninamtumikia kwa moyo wangu wote katika
kuhubiri Habari Njema ya Mwanae, ni shahidi wangu kwamba ninawakumbukeni
10 daima katika sala zangu. Namwomba Mungu akipenda,
anipatie nafasi nzuri ya kuja kwenu sasa.
11 Kwa maana ninatamani sana kuwaoneni ili nipate
kuwagawieni zawadi ya kiroho na kuwaimarisha.
12 Ndiyo kusema, tutaimarishana: imani yenu itaniimarisha
mimi, na yangu itawaimarisha ninyi.
13 Ndugu zangu, nataka mjue kwamba mara nyingi nilikusudia
kuwatembeleeni, lakini mpaka sasa nimezuiwa. Ningependa kupata mafanikio mema
kati yenu kama nilivyopata kati ya watu wa mataifa mengine.
14 Ninalo jukumu kwa watu wote, waliostaarabika na
wasiostaarabika, wenye elimu na wasio na elimu.
15 Ndiyo maana ninatamani pia kuihubiri Habari Njema kwenu
ninyi mlioko huko Roma.
16 Sioni aibu kutangaza Habari Njema; yenyewe ni nguvu ya
Mungu inayowaokoa wote wanaoamini: Wayahudi kwanza, na wasio Wayahudi pia.
17 Kwa maana Habari Njema inaonyesha wazi jinsi Mungu
anavyowakubali watu kuwa waadilifu; jambo hili hufanyika kwa imani, tangu
mwanzo mpaka mwisho. Kama ilivyoandikwa: "Mwadilifu*fa* kwa imani
ataishi."
18 Ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi
ya uasi na uovu wote wa binadamu ambao kwa njia zao mbaya wanaupinga ukweli
usijulikane.
19 Kwa maana, yote yanayoweza kujulikana juu ya Mungu ni
wazi kwao; maana Mungu mwenyewe ameyadhirisha.
20 Tangu Mungu alipoumba ulimwengu, uwezo wake wa milele na
uungu wake, ingawa havionekani kwa macho, vinafahamika wazi. Watu wanaweza
kuyajua mambo hayo kutokana na vitu hivyo alivyoumba Mungu. Kwa hiyo hawana
njia yoyote ya kujitetea!
21 Ingawa wanajua kuna Mungu, lakini hawampi heshima
anayostahili, wala hawamshukuru. Badala yake, fikira zao zimekuwa batili na
akili zao tupu zimejaa giza.
22 Wanajidai kuwa wenye hekima, kumbe ni wapumbavu.
23 Wanaacha kumwabudu Mungu aishiye milele, na badala yake,
wanaabudu sanamu zilizo mfano wa binadamu ambaye hufa, mfano wa wanyama, ndege,
au wanyama watambaao.
24 Kwa sababu hiyo, Mungu amewaacha wafuate tamaa mbaya za
mioyo yao na kufanyiana mambo ya aibu kwa miili yao.
25 Wanaubadili ukweli juu ya Mungu kwa uongo; wanaheshimu
na kuabudu kiumbe badala ya Muumba mwenyewe, ambaye ndiye astahiliye sifa
milele! Amina.
26 Kwa hiyo, Mungu amewaacha wafuate tamaa mbaya. Hata
wanawake wanabadili matumizi yanayopatana na maumbile.
27 Nao wanaume hali kadhalika, wanaacha kufuata matumizi ya
maumbile ya mume na mke wakawakiana tamaa wao kwa wao. Wanaume wanafanyiana
mambo ya aibu, na hivyo wanajiletea wenyewe adhabu wanayostahili kwa vitendo
vyao viovu.
28 Kwa vile watu walikataa kumtambua Mungu, Mungu amewaacha
katika fikira zao potovu, wakafanya yale ambayo hawangestahili kufanya.
29 Wamejaa kila aina ya uovu, dhuluma, ulafi na ufisadi.
Wamejaa wivu, uuaji, ugomvi, udanganyifu na nia mbaya; husengenya,
30 na kusingiziana; ni watu wa kuchukiza kwa Mungu,
wafidhuli, wenye kiburi na majivuno; hodari sana katika kutenda mabaya, na
hawawatii wazazi wao;
31 hawana dhamiri, hawatimizi ahadi zao, hawana wema wala
huruma kwa wengine.
32 Wanajua kwamba Sheria ya Mungu yasema kwamba watu
wanaoishi mithili hiyo, wanastahili kifo. Zaidi ya hayo, siyo tu kwamba
wanafanya mambo hayo wao wenyewe, bali hata huwapongeza wale wanaofanya mambo
hayohayo.
|