Chapter 2
1 Basi, rafiki, kama unawahukumu wengine, huwezi kamwe
kujitetea haidhuru wewe ni nani. Kwa maana, kwa kuwahukumu wengine, unajilaani
wewe mwenyewe kwa vile nawe unayafanya mambo yaleyale unayohukumu.
2 Tunajua kwamba hukumu ya Mungu kwa wale wanaofanya mambo
kama hayo ni hukumu ya haki.
3 Lakini wewe, rafiki, unayewahukumu wale wanaofanya mambo
kama hayo bali wewe pia unayafanya, je unadhani utaiepa hukumu ya Mungu?
4 Au labda unaudharau wema wake mkuu, uvumilivu wake na
saburi yake, bila kutambua kwamba wema wake huo una shabaha ya kukuongoza upate
kutubu?
5 Lakini unao ugumu na ukaidi wa moyo, na hivyo
unajilundikia adhabu kwa Siku ile ambayo ghadhabu ya Mungu na hukumu zake za
haki vitadhihirishwa.
6 Siku hiyo Mungu atamlipa kila mmoja kufuatana na matendo
yake.
7 Wale wanaozingatia kutenda mema, kutafuta utukufu na
heshima ya Mungu na kutokufa, watapata uzima wa milele.
8 Lakini wale wengine wenye ubinafsi, wenye kukataa mambo
ya haki na kufuata uovu, wataangukiwa na ghadhabu na hasira ya Mungu.
9 Mateso
na maumivu yatampata binadamu yeyote atendaye uovu. Yatawapata Wayahudi kwanza,
na watu wa mataifa mengine pia.
10 Lakini
Mungu atawapa utukufu, heshima na amani wale wanaotenda mema; Wayahudi kwanza,
na watu wa mataifa mengine pia.
11 Maana
Mungu hambagui mtu yeyote.
12 Wale
wanaotenda dhambi bila kuijua Sheria ya Mose wataangamia ingawaje hawajui
Sheria. Na wale wanaotenda dhambi wakiwa wanaijua Sheria watahukumiwa kisheria.
13 Mtu
hafanywi kuwa mwadilifu mbele yake Mungu kwa kuisikia Sheria, bali kwa kuitii
Sheria.
14 Mathalan:
watu wa mataifa mengine hawana Sheria ya Mose; lakini kila wanapotimiza matakwa
ya Sheria wakiongozwa na dhamiri zao, wao wenyewe wanakuwa kipimo cha Sheria
ingawa hawaijui Sheria.
15
Mwenendo wao unaonyesha kwamba matakwa ya Sheria yameandikwa mioyoni mwao.
Dhamiri zao zinashuhudia pia jambo hilo, maana fikira zao mara nyingine
huwashtaki, na mara nyingine huwatetea.
16 Hivyo,
kufuatana na hii Habari Njema ninayohubiri, ndivyo itakavyokuwa wakati Mungu
atakapohukumu mambo ya siri ya binadamu kwa njia ya Yesu Kristo.
17 Na
wewe, je? Wewe mwenyewe unajiita Myahudi; unaitumainia Sheria na kujivunia kuwa
wa Mungu;
18 kwa
njia ya Sheria unajua matakwa ya Mungu na unaweza kuchagua jambo jema;
19 wewe
unajiona kuwa kiongozi wa vipofu na mwanga kwa wale walio gizani;
20
unajiona kuwa mkufunzi wa wajinga na mwalimu wa wale wasiokomaa bado. Unayo
katika Sheria picha kamili ya elimu na ukweli.
21 Basi,
wewe unawafundisha wengine; kwa nini hujifundishi wewe mwenyewe? Unawahubiria
wengine wasiibe, lakini kumbe wewe mwenyewe unaiba.
22
Unasema: "Msizini," na huku wewe unazini; unachukia sanamu za miungu
hali wewe unajitajirisha kwa kuiba katika nyumba za miungu.
23 Kwa
kujigamba ati unayo Sheria ya Mungu, je huoni kwamba kwa kuivunja Sheria
unamdharau Mungu?
24 Kama
vile Maandiko Matakatifu yasemavyo: "Watu wa mataifa mengine wamelikufuru
jina la Mungu kwa sababu yenu ninyi Wayahudi!"
25
Kutahiriwa kwako kutakuwa na maana kama ukiitii Sheria. Lakini kama unaivunja
Sheria, basi, ni afadhali ungalibaki bila kutahiriwa.
26 Kama
mtu wa mataifa mengine ambaye hakutahiriwa akitimiza matakwa ya Sheria, hakika
atafikiriwa kana kwamba ametahiriwa.
27 Watu wa
mataifa mengine watakuhukumu wewe Myahudi kama ukiivunja Sheria, ingawaje unayo
maandishi ya Sheria na umetahiriwa, hali wao wanaitii Sheria ingawa hawakutahiriwa.
28 Ndiyo
kusema, si kila anayeonekana kwa nje kuwa Myahudi ni Myahudi wa kweli, wala mtu
hawi Myahudi wa kweli ati kwa kuwa ametahiriwa kimwili.
29 Myahudi
wa kweli ni yule aliye Myahudi kwa ndani, yaani yule ambaye ametahiriwa moyoni.
Hili ni jambo la Roho, na si jambo la maandishi ya Sheria. Mtu wa namna
hiyo anapata sifa, si kutoka kwa watu, bali kutoka kwa Mungu.
|