Chapter 3
1 Basi, Myahudi ana nini zaidi kuliko watu wengine? Au
kutahiriwa kuna faida gani?
2 Naam,
iko faida kwa kila upande. Kwanza, Mungu aliwakabidhi Wayahudi ujumbe wake.
3 Lakini
itakuwaje iwapo baadhi yao hawakuwa waaminifu? Je, jambo hilo litaondoa
uaminifu wa Mungu?
4 Hata
kidogo! Mungu hubaki mwaminifu daima, ingawaje kila binadamu ni mwongo. Kama
Maandiko Matakatifu yasemavyo: "Kila usemapo, maneno yako ni ya haki; na
katika hukumu, wewe hushinda."
5 Lakini,
ikiwa uovu wetu unathibitisha kwamba Mungu anatenda kwa haki, tutasema nini?
Je, tutasema kwamba anakosa haki akituadhibu? (Hapa naongea kibinadamu).
6 Hata
kidogo! Ingekuwa hivyo, Mungu angewezaje kuuhukumu ulimwengu?
7 Labda
utasema: "Ikiwa ukosefu wa uaminifu kwa upande wangu unamdhihirisha Mungu
kuwa mwaminifu zaidi na hivyo kumpatia utukufu, basi singepaswa kuhukumiwa kuwa
mwenye dhambi!"
8 Ni sawa na kusema: tufanye maovu ili tupate mema! Ndivyo
wengine walivyotukashifu kwa kutushtaki kwamba tumefundisha hivyo. Watahukumiwa
wanavyostahili!
9 Tuseme nini, basi? Je, sisi Wayahudi ni bora zaidi kuliko
wengine? Hata kidogo! Kwa maana nimekwisha bainisha hapo mwanzoni kwamba
Wayahudi na watu wa mataifa mengine wote wako chini ya utawala wa dhambi.
10 Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: "Hakuna hata
mmoja aliye mwadilifu!
11 Hakuna mtu anayeelewa, wala anayemtafuta Mungu.
12 Wote wamepotoka wote wamekosa; hakuna atendaye mema,
hakuna hata mmoja.
13 Makoo yao ni kama kaburi wazi, ndimi zao zimejaa
udanganyifu, midomoni mwao mwatoka maneno yenye sumu kama ya nyoka.
14 Vinywa vyao vimejaa laana chungu.
15 Miguu yao iko mbioni kumwaga damu,
16 popote waendapo husababisha maafa na mateso;
17 njia ya amani hawaijui.
18 Hawajali kabisa kumcha Mungu."
19 Tunajua kwamba Sheria huwahusu walio chini ya Sheria
hiyo, hata hawawezi kuwa na kisingizio chochote, na ulimwengu wote uko chini ya
hukumu ya Mungu.
20 Maana hakuna binadamu yeyote anayekubaliwa kuwa mwadilifu
mbele yake Mungu kwa kuishika Sheria; kazi ya Sheria ni kumwonyesha tu mtu
kwamba ametenda dhambi.
21 Lakini sasa, njia ya Mungu ya kuwakubali watu kuwa
waadilifu imekwisha dhihirishwa, tena bila kutegemea Sheria. Sheria na manabii
hushuhudia jambo hili.
22 Mungu huwakubali watu kuwa waadilifu kwa njia ya imani
yao kwa Yesu Kristo; Mungu hufanya hivyo kwa wote wanaoamini; hakuna ubaguzi
wowote.
23 Watu wote wametenda dhambi na wametindikiwa utukufu wa
Mungu.
24 Lakini kwa zawadi ya neema ya Mungu, watu wote
hukubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya Yesu Kristo anayewakomboa.
25 Mungu alimtoa Yesu kusudi, kwa damu yake, awe njia ya
kuwaondolea watu dhambi zao kwa imani yao kwake. Alifanya hivyo ili apate
kuonyesha kwamba yeye ni mwadilifu. Hapo zamani Mungu alikuwa mvumilivu bila
kuzijali dhambi za watu;
26 lakini sasa, wakati huu, anazikabili dhambi za watu
apate kuonyesha uadilifu wake. Kwa namna hiyo Mungu mwenyewe huonyesha kwamba
yeye ni mwadilifu na kwamba humkubali kuwa mwadilifu mtu yeyote anayemwamini
Yesu.
27 Basi, tunaweza kujivunia nini? Hakuna! Kwa nini? Je, kwa
sababu ya kutimiza Sheria? La! Bali kwa sababu tunaamini.
28 Maana mtu hukubaliwa kuwa mwadilifu kwa imani, wala si
kwa kutimiza matakwa ya Sheria.
29 Au je, Mungu nu Mungu wa Wayahudi tu, ama pia wa watu wa
mataifa mengine? Naam, wa mataifa mengine pia.
30 Mungu ni mmoja, naye atawakubali Wayahudi kuwa waadilifu
kwa imani yao, na watu wa mataifa mengine pia kwa imani yao.
31 Je, tunaitumia imani kuibatilisha Sheria? Hata kidogo;
bali tunaipa Sheria thamani yake kamili.
|