Chapter 4
1 Tuseme nini basi, juu ya Abrahamu baba yetu?
2 Kama Abrahamu alikubaliwa kuwa mwadilifu kutokana na
matendo yake, basi, anacho kitu cha kujivunia mbele ya Mungu.
3 Kwa maana, Maandiko Matakatifu yasema: "Abrahamu
alimwamini Mungu, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu."
4 Mfanyakazi hulipwa mshahara; mshahara wake si zawadi bali
ni haki yake.
5 Lakini mtu asiyetegemea matendo yake mwenyewe, bali
anamwamini Mungu ambaye huwasamehe waovu, basi, Mungu huijali imani ya mtu
huyo, na hivi humkubali kuwa mwadilifu.
6 Naye Daudi asema hivi juu ya furaha ya mtu ambaye Mungu
amemkubali kuwa mwadilifu bila kuyajali matendo yake:
7 "Heri wale waliosamehewa makosa yao ambao makosa yao
yamefutwa.
8 Heri mtu yule ambaye Bwana hataziweka dhambi zake katika
kumbukumbu."
9 Je, hiyo ni kwa wale waliotahiriwa tu, ama pia kwa wale
wasiotahiriwa? Ni kwa wale wasiotahiriwa pia. Kwa maana tumekwisha sema:
"Abrahamu aliamini, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu."
10 Je, Abrahamu alikubaliwa kabla ya kutahiriwa ama baada
ya kutahiriwa? Kabla ya kutahiriwa, na si baada ya kutahiriwa.
11 Abrahamu alitahiriwa baadaye, na kutahiriwa huko
kulikuwa alama iliyothibitisha kwamba Mungu alimkubali kuwa mwadilifu kwa
sababu ya imani yake aliyokuwa nayo kabla ya kutahiriwa. Kwa hiyo, Abrahamu
amekuwa baba wa wale wote ambao, ingawa hawakutahiriwa, wamemwamini Mungu,
wakafanywa waadilifu.
12 Vilevile yeye ni baba wa wale waliotahiriwa; lakini si
kwa kuwa wametahiriwa, bali kwa sababu wanafuata njia ileile ya imani baba yetu
Abrahamu aliyofuata kabla ya kutahiriwa.
13 Mungu alimwahidi Abrahamu na wazawa wake kwamba
ulimwengu ungekuwa mali yao. Ahadi hiyo haikufanywa kwa sababu Abrahamu aliitii
Sheria, bali kwa kuwa aliamini, akakubaliwa kuwa mwadilifu.
14 Maana kama watakaopewa hayo aliyoahidi Mungu ni wale tu
wanaoitii Sheria, basi, imani haina maana yoyote, nayo ahadi ya Mungu si kitu.
15 Sheria husababisha ghadhabu; lakini kama hakuna Sheria,
haiwezekani kuivunja.
16 Kwa sababu hiyo, jambo hili lategemea imani, hivyo
kwamba ahadi hiyo yatokana na neema ya Mungu, na kwamba ni hakika kuwa ahadi
hiyo ni kwa ajili ya wote: si kwa wale tu wanaoishika Sheria, bali pia kwa wale
waishio kwa imani kama Abrahamu. Yeye ni baba yetu sisi sote.
17 Kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: "Nimekuweka uwe
baba wa mataifa mengi." Ahadi hiyo ni kweli mbele ya Mungu ambaye Abrahamu
alimwamini - Mungu ambaye huwapa wafu uzima, na kwa amri yake, vitu ambavyo
havikuwapo huwa.
18 Abrahamu aliamini na kutumaini ingawa hali yenyewe
ilikuwa bila matumaini, na hivyo amekuwa baba wa mataifa mengi kama Maandiko
Matakatifu yasemavyo: "Wazao wako watakuwa wengi kama nyota!"
19 Alikuwa mzee wa karibu miaka mia moja, lakini imani yake
haikufifia ingawa alijua kwamba mwili wake ulikuwa kama umekufa, na pia mkewe,
Sara, alikuwa tasa.
20 Abrahamu hakuionea mashaka ile ahadi ya Mungu; alipata
nguvu kutokana na imani, akamtukuza Mungu.
21 Alijua kwamba Mungu anaweza kuyatekeleza yale
aliyoahidi.
22 Ndiyo maana Mungu alimkubali kuwa mwadilifu.
23 Inaposemwa, "Alimkubali," haisemwi kwa ajili
yake mwenyewe tu.
24 Jambo hili linatuhusu sisi pia ambao tunamwamini Mungu
aliyemfufua Yesu, Bwana wetu, kutoka wafu.
25 Yeye alitolewa auawe kwa ajili ya dhambi zetu, akafufuka
ili tupate kukubaliwa kuwa waadilifu na Mungu.
|