Chapter 5
1 Sasa, kwa vile tumekubaliwa kuwa wadilifu kwa imani,
basi, tunayo amani na Mungu kwa ajili ya Bwana wetu Yesu Kristo.
2 Kwa imani yetu, yeye ametuleta katika hali hii ya neema
ya Mungu ambamo sasa tunaishi. Basi, tunajivunia tumaini tulilo nalo la
kushiriki utukufu wa Mungu.
3 Naam, si hayo tu, bali tunafurahi pia katika taabu
tukijua kwamba taabu huleta saburi,
4 nayo saburi huleta uthabiti, na uthabiti huleta tumaini.
5 Tumaini hilo haliwezi kutuhadaa, maana Mungu amekwisha
miminia mioyoni mwetu upendo wake kwa njia ya Roho Mtakatifu aliyetujalia.
6 Tulipokuwa bado wanyonge, Kristo, wakati ulipotimia,
alikufa kwa ajili yetu sisi waovu.
7 Si rahisi mtu kufa kwa ajili ya mtu mwadilifu; labda mtu
anaweza kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema.
8 Lakini Mungu amethibitisha kwamba anatupenda, maana
wakati tulipokuwa bado wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu.
9 Kwa kuwa sasa tumekubaliwa kuwa waadilifu kwa damu ya
Kristo, ni dhahiri zaidi kwamba atatuokoa katika ghadhabu ya Mungu.
10 Maana, tulipokuwa bado adui zake, Mungu alitupatanisha
naye kwa kifo cha Mwanae. Na kwa vile sasa tumepatanishwa naye, ni dhahiri
zaidi kwamba tutaokolewa kwa uzima wa Kristo.
11 Wala si hayo tu, ila tunafurahi pia katika Mungu kwa
njia ya Bwana wetu Yesu Kristo ambaye ametupatanisha na Mungu.
12 Kwa njia ya mtu mmoja dhambi iliingia ulimwenguni, nayo
ikasababisha kifo. Hivyo kifo kimeenea katika jumuiya yote ya binadamu, kwa
maana wote wametenda dhambi.
13 Kabla ya Sheria kuwako, dhambi ilikuwako ulimwenguni;
lakini dhambi haiwekwi katika kumbukumbu bila sheria.
14 Lakini tangu wakati wa Adamu mpaka wakati wa Mose, kifo
kiliwatawala hata wale ambao hawakutenda dhambi kama ile ya Adamu, ya kumwasi
Mungu. Adamu alikuwa kielelezo cha yule ambaye atakuja baadaye.
15 Lakini ipo tofauti: neema ya Mungu si kama dhambi ya
Adamu. Maana, ingawa dhambi ya mtu mmoja ilisababisha kifo kwa wote, kwa
fadhili ya mtu mmoja, yaani Yesu Kristo, Mungu amewazidishia wote neema na
zawadi zake.
16 Kuna tofauti baina ya zawadi ya Mungu, na dhambi ya mtu
yule mmoja. Maana, baada ya kosa la mtu mmoja, Mungu alitoa hukumu; lakini
baada ya makosa ya watu wengi, Mungu aliwapa zawadi yake kwa kuwasamehe.
17 Kweli, kwa dhambi ya mtu mmoja kifo kilianza kutawala
kwa sababu ya huyo mtu mmoja; lakini, ni dhahiri zaidi kwamba alichokifanya
yule mtu mmoja, yaani Yesu Kristo, ni bora zaidi. Wote wanaopokea neema na
zawadi hiyo ya kukubaliwa kuwa waadilifu, watatawala katika uzima kwa njia ya
huyo mmoja, yaani Yesu Kristo.
18 Basi, kama vile kosa la mtu mmoja lilivyoleta hukumu kwa
binadamu wote, kadhalika kitendo kimoja kiadilifu kinawapa uhuru na uzima.
19 Na kama kwa kutotii kwa mtu mmoja watu wengi walifanywa
wenye dhambi, kadhalika kutii kwa mtu mmoja kutawafanya wengi wakubaliwe kuwa
waadilifu.
20 Sheria ilitokea, ikasababisha kuongezeka kwa uhalifu;
lakini pale dhambi ilipoongezeka, neema iliongezeka zaidi.
21 Kama vile dhambi ilivyotawala kwa kifo, kadhalika neema
inatawala kwa njia ya uadilifu, na kuleta uzima wa milele kwa njia ya Yesu
Kristo Bwana wetu.
|