Chapter 6
1 Tuseme nini basi? Je, twendelee kubaki katika dhambi ili
neema ya Mungu iongezeke?
2 Hata kidogo! Kuhusu dhambi sisi tumekufa - tutaendeleaje
kuishi tena katika dhambi?
3 Maana, mnajua kwamba sisi tuliobatizwa tukaungana na
Kristo Yesu, tulibatizwa na kuungana na kifo chake.
4 Tulipobatizwa tuliungana na kifo chake, tukazikwa pamoja
naye, ili kama vile Kristo alivyofufuliwa kutoka wafu kwa kitendo kitukufu cha
Baba, sisi pia tuweze kuishi maisha mapya.
5 Maana, kama sisi tumeungana naye katika kufa kama yeye,
vivyo hivyo tutaungana naye kwa kufufuliwa kutoka wafu kama yeye.
6 Tunajua kwamba utu wetu wa kale ulisulubiwa pamoja na
Kristo, ili hali ya dhambi iharibiwe, tusiwe tena watumwa wa dhambi.
7 Kwa maana, mtu aliyekufa, amenasuliwa kutoka katika nguvu
ya dhambi.
8 Basi, ikiwa tumekufa pamoja na Kristo, tunaamini kwamba
tutaishi pia pamoja naye.
9 Maana, tunajua kwamba Kristo amekwisha fufuliwa kutoka
wafu na hafi tena; kifo hakimtawali tena.
10 Hivyo, kwa kuwa alikufa - mara moja tu - dhambi haina
nguvu tena juu yake; na sasa anaishi maisha yake katika umoja na Mungu.
11 Hali kadhalika nanyi lazima mjione kuwa mmekufa kuhusu
dhambi, lakini kama mnaoishi katika umoja na Mungu kwa njia ya Kristo Yesu.
12 Kwa hiyo, dhambi isiitawale tena miili yenu ambayo hufa,
na hivyo kuzitii tamaa zake.
13 Wala msitoe hata sehemu moja ya miili yenu iwe chombo
cha kutenda uovu na dhambi. Badala yake, jitoleeni ninyi wenyewe kwa Mungu kama
watu waliofufuliwa kutoka wafu; toeni nafsi zenu zote kwa Mungu kwa ajili ya
uadilifu.
14 Maana, dhambi haitawatawala ninyi tena, kwani hamko
chini ya Sheria, bali chini ya neema.
15 Basi, tuseme nini? Je, tutende dhambi ati kwa sababu
hatuko chini ya Sheria bali chini ya neema? Hata kidogo!
16 Mnajua kwamba mkijitolea ninyi wenyewe kama watumwa na
kumtii fulani, mnakuwa kweli watumwa wake mtu huyo - au watumwa wa dhambi, na
matokeo yake ni kifo, au wa utii, na matokeo yake ni kukubaliwa kuwa waadilifu.
17 Ingawa mlikuwa watumwa wa dhambi zamani, sasa lakini -
namshukuru Mungu - mmetii kwa moyo wote yale maazimio na mafundisho mliyopokea.
18 Mlikombolewa kutoka utumwa wa dhambi, mkawa watumwa wa
uadilifu.
19 (Hapa natumia lugha ya kawaida ya watu kwa sababu ya
udhaifu wenu wenyewe.) Kama vile wakati fulani mlivyojitolea ninyi wenyewe
kutumikia uchafu na uhalifu kwa ajili ya uovu, vivyo hivyo sasa jitoleeni nafsi
zenu wenyewe kutumikia uadilifu kwa ajili ya utakatifu.
20 Mlipokuwa watumwa wa dhambi, mlikuwa huru mbali na
uadilifu.
21 Sasa, mlipata faida gani siku zile kutokana na mambo
yale ambayo mnayaonea aibu sasa? Maana, matokeo ya mambo haya ni kifo!
22 Lakini sasa, mmekwisha kombolewa kutoka utumwa wa dhambi
na mmekuwa watumishi wa Mungu; faida mliyo nayo sasa ni utakatifu, na matokeo
yake ni uzima wa milele.
23 Kwa maana mshahara wa dhambi ni kifo; lakini zawadi
anayotoa Mungu ni uzima wa milele katika kuungana na Kristo Yesu, Bwana wetu.
|