Chapter 9
1 Nasema ukweli
mtupu; nimeungana na Kristo nami sisemi uongo. Dhamiri yangu ikiongozwa na Roho
Mtakatifu inanithibitishia jambo hili pia.
2 Nataka kusema
hivi: nina huzuni kubwa na maumivu yasiyopimika moyoni mwangu
3 kwa ajili ya
watu wangu, walio damu moja nami! Kama ingekuwa kwa faida yao, ningekuwa radhi
kulaaniwa na kutengwa na Kristo.
4 Hao ndio watu
wa Israeli ambao Mungu aliwateua wawe watoto wake, akawashirikisha utukufu
wake; aliagana nao, akawapa Sheria yake, imani ya kweli na ahadi zake.
5 Wao ni wajukuu
wa mababu, naye Kristo, kadiri ya ubinadamu wake, ametoka katika ukoo wao.
Mungu atawalaye juu ya yote, na atukuzwe milele! Amina.
6 Sisemi kwamba
ahadi ya Mungu imebatilika; maana si watu wote wa Israeli ni wateule wa Mungu.
7 Wala, si
wazawa wote wa Abrahamu ni watoto wake wa kweli. Ila, kama yasemavyo Maandiko
Matakatifu: "Wazao wake watatokana na Isaka."
8 Nido kusema,
wale waliozaliwa kimaumbile ndio watoto wa Mungu, bali wale waliozaliwa
kutokana na ahadi ya Mungu ndio watakaoitwa watoto wake.
9 Maana ahadi
yenyewe ni hii: "Nitakujia wakati maalum, naye Sara atapata mtoto."
10 Tena si hayo
tu ila pia Rebeka naye alipata mapacha kwa baba mmoja, yaani Isaka, babu yetu.
11 Lakini, ili
Mungu aonekane kwamba anao uhuru wa kuchagua, hata kabla wale ndugu
hawajazaliwa na kabla hawajaweza kupambanua jema na baya,
12 Rebeka
aliambiwa kwamba yule mtoto wa kwanza atamtumikia yule wa nyuma. Hivyo uchaguzi
wa Mungu unategemea jinsi anavyoita mwenyewe, na si matendo ya binadamu.
13 Kama Maandiko
Matakatifu yasemavyo: "Yakobo nilimpenda, lakini Esau nilimchukia."
14 Basi, tuseme nini? Je, Mungu amekosa haki? Hata kidogo!
15 Maana alimwambia Mose: "Nitamhurumia mtu yeyote
ninayetaka kumhurumia; nitamwonea huruma mtu yeyote ninayetaka."
16 Kwa hiyo, yote hutegemea huruma ya Mungu, na si bidii au
mapenzi ya mtu.
17 Maana Maandiko Matakatifu yasema hivi kwa Farao:
"Nilikufanya mfalme ili kwa njia yako, uwezo wangu ujulikane, na jina
langu litangazwe popote duniani."
18 Ni wazi,basi, kwamba Mungu humhurumia yeyote anayetaka
kumhurumia, na akipenda kumfanya mtu awe mkaidi, hufanya hivyo.
19 Labda utaniuliza: "Ikiwa mambo yako hivyo, Mungu
anawezaje kumlaumu mtu? Nani awezaye kuyapinga mapenzi yake?"
20 Lakini, ewe binadamu, u nani hata uthubutu kumhoji
Mungu? Je, chungu chaweza kumwuliza mfinyanzi wake: "Kwa nini
umenitengeneza namna hii?"
21 Mfinyanzi anaweza kuutumia udongo apendavyo na
kufinyanga vyungu viwili kwa udongo uleule; kimoja kwa matumizi ya heshima, na
kingine kwa matumizi ya kawaida.
22 Hivyo ndivyo ilivyo kwa Mungu. Alitaka kuonyesha
ghadhabu yake na kujulisha uwezo wake, Basi, alikuwa na saburi sana,
akiwavumilia wale ambao walikuwa lengo la ghadhabu yake, ambao walistahili
kuangamizwa.
23 Alitaka pia kudhihirisha wingi wa utukufu wake ambao
alitumiminia sisi tulio lengo la huruma yake; sisi ambao alikwisha
kututayarisha kuupokea utukufu wake.
24 Maana sisi ndio hao aliowaita, si tu kutoka miongoni mwa
Wayahudi bali pia kutoka kwa watu wa mataifa mengine.
25 Maana ndivyo asemavyo katika kitabu cha Hosea:
"Wale waliokuwa `Si watu wangu` nitawaita: `Watu wangu!` Naye `Sikupendi`
ataitwa: `Mpenzi wangu!`
26 Na pale walipoambiwa: `Ninyi si wangu` hapo wataitwa:
`Watoto wa Mungu hai."`
27 Naye nabii Isaya, kuhusu Israeli anapaaza sauti:
"Hata kama watoto wa Israeli ni wengi kama mchanga wa pwani, ni wachache
tu watakaookolewa;
28 maana, Bwana ataitekeleza upesi hukumu yake kamili juu
ya ulimwengu wote."
29 Ni kama Isaya alivyosema hapo awali: "Kama Bwana
Mwenye Nguvu asingalituachia baadhi ya watoto wa Israeli, tungalikwisha kuwa
kama Sodoma, tungalikwisha kuwa ma Gomora."
30 Basi, tuseme nini? Ni hivi: watu wa mataifa ambao
hawakutafuta kukubaliwa kuwa waadilifu, wamekubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya
imani,
31 hali watu wa Israeli waliokuwa wakitafuta Sheria iletayo
kukubaliwa kuwa waadilifu, hawakuipata.
32 Kwa nini? Kwa sababu walitegemea matendo yao badala ya
kutegemea imani. Walijikwaa juu ya jiwe la kujikwaa
33 kama yesemavyo Maandiko Matakatifu: "Tazama! Naweka
huko Sioni jiwe likwazalo, mwamba utakaowafanya watu waanguke. Mtu
atakayemwamini yeye aliye hilo jiwe, hataaibishwa!"
|