Chapter 10
1 Ndugu zangu, ninataka na kutazamia kwa moyo wangu wote
hao wananchi wenzangu wakombolewe. Tena nawaombea kwa Mungu daima.
2 Maana naweza kuthibitisha kwa niaba yao kwamba wanayo
bidii ya kumtafuta Mungu; lakini bidii hiyo haikujengwa juu ya ujuzi wa kweli.
3 Maana hawakufahamu jinsi Mungu anavyowafanya watu wawe
waadilifu, na wamejaribu kuanzisha mtindo wao wenyewe, na hivyo hawakuikubali
njia hiyo ya Mungu ya kuwafanya wawe waadilifu.
4 Maana kwa kuja kwake Kristo, Sheria imefikia kikomo
chake, ili kila mtu anayeamini akubaliwe kuwa mwadilifu.
5 Kuhusu kukubaliwa kuwa mwadilifu kwa kuitii Sheria, Mose
aliandika hivi: "Mtu yeyote anayetimiza matakwa ya Sheria ataishi."
6 Lakini, kuhusu kukubaliwa kuwa mwadilifu kwa njia ya
imani, yasemwa hivi: "Usiseme moyoni mwako: `Nani atapanda mpaka
mbinguni?` (yaani, kumleta Kristo chini);
7 wala usiseme: `Nani atashuka mpaka Kuzimu` (yaani,
kumleta Kristo kutoka kwa wafu)."
8 Maandiko Matakatifu yesema hivi, "Ujumbe huo wa
Mungu uko karibu nawe, uko kinywani mwako na moyoni mwako" nao ndio ile
imani tunayoihubiri.
9 Kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba Yesu ni Bwana na
kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka wafu, utaokoka.
10 Maana tunaamini kwa moyo na kukubaliwa kuwa waadilifu;
na tunakiri kwa midomo yetu na kuokolewa.
11 Maandiko Matakatifu yasema: "Kila amwaminiye
hatakuwa na sababu ya kuaibika."
12 Jambo hili ni kwa wote, kwani hakuna tofauti kati ya
Wayahudi na wasio Wayahudi; Bwana wa wote ni mmoja, naye ni mkarimu sana kwao
wote wamwombao.
13 Maana Maandiko Matakatifu yasema: "Kila mtu
atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa."
14 Basi,
watamwombaje yeye ambaye hawamwamini? Tena, watamwaminije kama hawajapata
kusikia habari zake? Na watasikiaje habari zake kama hakuna mhubiri?
15 Na watu
watahubirije kama hawakutumwa? Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Ni
jambo la kupendeza mno kuja kwa wale wanaohubiri Habari Njema!"
16 Lakini
wote hawakuipokea hiyo Habari Njema. Maana Isaya alisema: "Bwana, ni nani
aliyeamini ujumbe wetu?"
17 Hivyo
basi, imani inatokana na kuusikiliza ujumbe, na huo ujumbe unatokana na neno la
Kristo.
18 Lakini
nauliza: je, hawakuusikia huo ujumbe? Naam, waliusikia; kama Maandiko
Matakatifu yasemavyo: "Sauti yao imeenea duniani kote; maneno yao yamefika
mpaka kingo za ulimwengu."
19 Tena
nauliza: je, yawezekana kwamba watu wa Israeli hawakufahamu? Mose mwenyewe ni
kwa kwanza kujibu: "Nitawafanyeni mwaonee wivu watu ambao si taifa;
nitawafanyeni muwe na hasira juu ya taifa la watu wapumbavu."
20 Tena
Isaya anathubutu hata kusema: "Wale ambao hawakunitafuta wamenipata;
nimejionyesha kwao wasiouliza habari zangu."
21 Lakini
kuhusu Israeli anasema: "Mchana kutwa niliwanyoshea mikono yangu watu
waasi na wasiotii."
|