Chapter 11
1 Basi,
nauliza: je, Mungu amewakataa watu wake? Hata kidogo! Mini binafsi ni Mwisraeli
mzawa wa Abrahamu, wa kabila la Benyamini.
2 Mungu
hakuwakataa watu wake aliowateua tangu mwanzo. Mnakumbuka yasemavyo Maandiko
Matakatifu juu ya Eliya wakati alipomnung`unikia Mungu kuhusu Israeli:
3
"Bwana, wamewaua manabii wako na kubomoa madhabahu yako. Ni mimi tu peke
yangu niliyebaki, nao wanataka kuniua?"
4 Je,
Mungu alimjibu nini? Alimwambia: "Nimejiwekea elfu saba ambao
hawakumwabudu Baali."
5 Basi,
ndivyo ilivyo pia wakati huu wa sasa: ipo idadi ya waliobaki ambao Mungu
aliwateua kwa sababu ya neema yake.
6 Uteuzi
wake unatokana na neema yake, na si kwa sababu ya matendo yao. Maana, kama
uteuzi wake ungetegemea matendo ya watu, neema yake haingekuwa neema tena.
7 Sasa,
je? Watu wa Israeli hawakukipata kile walichokuwa wanakitafuta; lakini wote
walioteuliwa walikipata. Wengine walipumbazwa,
8 kama
yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Mungu ameifanya mioyo yao kuwa mizito, na
mpaka leo hii hawawezi kuona kwa macho yao wala kusikia kwa masikio yao."
9 Naye
Daudi anasema: "Karamu zao na ziwe mtego wa kuwanasa, waanguke na
kuadhibiwa.
10 Macho
yao yatiwe giza wasiweze kuona. Migongo yao ipindike kwa taabu daima!"
11 Basi,
nauliza: je, Wayahudi wamejikwaa hata wakaangamia kabisa? Hata kidogo! Kutokana
na kosa lao ukombozi umewajia watu wa mataifa mengine, ili Wayahudi wapate
kuwaonea wivu.
12 Kosa la
Wayahudi limesababisha baraka nyingi kwa ulimwengu, na utovu wao kwa kiroho
umeleta baraka nyingi kwa watu wa mataifa mengine. Basi, ni dhahiri zaidi
kwamba utimilifu wao utasababisha baraka nyingi zaidi.
13 Basi,
sasa nawaambieni ninyi watu wa mataifa mengine: Maadamu mimi nimekuwa mtume kwa
watu wa mataifa mengine, ninajivunia huduma yangu,
14 nipate
kuwafanya wananchi wenzangu wawaonee ninyi wivu, na hivyo nipate kuwaokoa
baadhi yao.
15 Maana
ikiwa kukataliwa kwao kulisababisha ulimwengu upatanishwe na Mungu, itakuwaje
wakati watakapokubaliwa na Mungu? Wafu watafufuka!
16 Ikiwa
kipande cha kwanza cha mkate kimewekwa wakfu, mkate wote umewekwa wakfu; mizizi
ya mti ikiwa mizuri, na matawi yake huwa mazuri pia.
17 Naam,
baadhi ya matawi ya mzeituni bustanini yalikatwa, na mahali pake tawi la
mzeituni mwitu likapandikizwa. Ninyi watu wa mataifa mengine ndio hilo tawi la
mzeituni mwitu; na sasa mnashiriki nguvu na utomvu wa mzeituni bustanini.
18 Basi,
msiwadharau wale waliokatwa kama matawi! Na, hata kama kuna la kujivunia,
kumbukeni kwamba si ninyi mnaoitegemeza mizizi, bali mizizi ndiyo
inayowategemeza ninyi.
19 Lakini
utasema: "Matawi yalikatwa kusudi mimi nipandikizwe mahali pake."
20 Sawa!
Yalikatwa kwa sababu ya kukosa imani, bali wewe unasimama kwa imani yako.
Lakini usijivune; ila uwe na tahadhari.
21 Kwa
maana, ikiwa Mungu hakuwahurumia Wayahudi ambao ni kama matawi ya asili, je,
unadhani atakuhurumia wewe?
22
Kumbuka, basi, jinsi Mungu alivyo mwema na mkali. Yeye ni mkali kwa wale
walioanguka, na ni mwema kwako wewe ikiwa utaendelea katika wema wake; la
sivyo, nawe pia utakatwa.
23 Nao
Wayahudi, hali kadhalika; wakiacha utovu wao wa imani, watapandikizwa tena.
Maana Mungu anao uwezo wa kuwapandikiza tena.
24 Ninyi
watu wa mataifa mengine, kwa asili ni kama tawi la mzeituni mwitu, lakini
mmeondolewa huko, mkapandikizwa katika mzeituni bustanini mahali ambapo kwa
asili si penu. Lakini, Wayahudi kwa asili ni kama mzeituni bustanini, na
itakuwa jambo rahisi zaidi kwao kupandikizwa tena katika mti huohuo wao.
25 Ndugu
zangu, napenda mjue ukweli huu uliofichika msije mkajiona wenye akili sana.
Ukaidi wa Wayahudi ulikuwa ni wa muda tu, mpaka watu wa mataifa mengine
watakapokuwa wamemfikia Mungu.
26 Hapo
ndipo taifa lote la Israeli litakapookolewa, kama yesemavyo Maandiko Matakatifu:
"Mkombozi atakuja kutoka Sioni, atauondoa uovu wa Yakobo.
27 Hili
ndilo agano nitakalofanya nao wakati nitakapoziondoa dhambi zao."
28 Kwa
sababu wanaikataa Habari Njema, Wayahudi wamekuwa adui wa Mungu, lakini kwa faida
yenu nyinyi watu wa mataifa. Lakini, kwa kuwa waliteuliwa, bado ni rafiki wa
Mungu kwa sababu ya baba zao.
29 Maana
Mungu akisha wapa watu zawadi zake na kuwateua, hajuti kwamba amefanya hivyo.
30 Hapo
awali ninyi mlikuwa mmemwasi Mungu, lakini sasa mmepata huruma yake kutokana na
kuasi kwao.
31 Hali
kadhalika, kutokana na huruma mliyojaliwa ninyi, Wayahudi wanamwasi Mungu sasa
ili nao pia wapokee sasa huruma ya Mungu.
32 Maana
Mungu amewafunga watu wote katika uasi wao ili wapate kuwahurumia wote.
33
Utajiri, hekima na elimu ya Mungu ni kuu mno! Huruma zake hazichunguziki, na
njia zake hazieleweki! Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu:
34
"Nani aliyepata kuyajua mawazo ya Bwana? Nani awezaye kuwa mshauri wake?
35 Au,
nani aliyempa yeye kitu kwanza hata aweze kulipwa tena kitu hicho?"
36 Kwa
maana vitu vyote vyatoka kwake, vyote vipo kwa uwezo wake na kwa ajili yake.
Utukufu na uwe kwake hata milele! Amina.
|