Chapter 12
1 Kwa
hiyo, ndugu zangu, maadam Mungu ni mwenye huruma nyingi, nawasihi kwa moyo wote:
jitoleeni nafsi zenu kwa Mungu kama tambiko iliyo hai, takatifu na yenye
kupendeza. Hii ndiyo njia yenu halisi ya kumwabudu.
2 Msiige
mitindo ya ulimwengu huu, bali Mungu afanye mabadiliko ndani yenu kwa kuzigeuza
fikira zenu. Hapo ndipo mtakapoweza kuyajua mapenzi ya Mungu, kutambua jambo
lililo jema, linalompendeza na kamilifu.
3 Kutokana
na neema aliyonijalia Mungu, nawaambieni ninyi nyote: msijione kuwa ni kitu
zaidi kuliko mnavyopaswa kuwa. Fikira zenu na ziwe na kiasi kufuatana na kipimo
cha imani Mungu aliyomgawia kila mmoja.
4 Mwili
una viungo vingi, kila kimoja na kazi yake.
5 Hali
kadhalika ingawa sisi ni wengi, tu mwili mmoja kwa kuungana na Kristo, na kila
mmoja ni kiungo cha mwenzake.
6 Basi,
tunavyo vipaji mbalimbali kufuatana na neema tuliyopewa. Mwenye kipaji cha
unabii na akitumie kadiri ya imani yake.
7 Mwenye
kipaji cha utumishi na atumikie. mwenye kipaji cha kufundisha na afundishe.
8 Mwenye
kipaji cha kuwafariji wengine na afanye hivyo. Mwenye kumgawia mwenzake alicho
nacho na afanye hivyo kwa ukarimu. Msimamizi na asimamie kwa bidii; naye mwenye
kutenda jambo la huruma na afanye hivyo kwa furaha.
9 Mapendo
yenu na yawe bila unafiki wowote. Chukieni jambo lolote ovu, zingatieni jema.
10
Pendaneni kidugu; kila mmoja amfikirie mwenzake kwanza kwa heshima.
11
Msilegee katika bidii, muwe wachangamfu rohoni katika kumtumikia Bwana.
12 Tumaini
lenu liwaweke daima wenye furaha; muwe na saburi katika shida na kusali daima.
13
Wasaidieni watu wa Mungu katika mahitaji yao; wapokeeni wageni kwa ukarimu.
14
Watakieni baraka wote wanaowadhulumu ninyi; naam, watakieni baraka na wala
msiwalaani.
15
Furahini pamoja na wanaofurahi, lieni pamoja na wanaolia.
16 Muwe na
wema uleule kwa kila mtu. Msijitakie makuu, bali jishugulisheni na watu wadogo.
Msijione kuwa wenye hekima sana.
17 Msilipe
ovu kwa ovu. Zingatieni mambo mema mbele ya wote.
18 Kadiri inavyowezekana kwa upande wenu, muwe na amani na
watu wote.
19 Wapenzi wangu, msilipize kisasi, bali mwachieni Mungu
jambo hilo; maana Maandiko Matakatifu yasema: "Kulipiza kisasi ni shauri
langu; mimi nitalipiza asema Bwana."
20 Tena, Maandiko yasema: "Adui yako akiwa na njaa,
mpe chakula; akiwa na kiu, mpe kinywaji. Maana kwa kufanya hivyo utamfanya
apate aibu kali kama makaa ya moto juu ya kichwa chake."
21 Usikubali kushindwa na ubaya, bali ushinde ubaya kwa
wema.
|