Chapter 13
1 Kila mtu anapaswa kuwatii wenye mamlaka katika serikali;
maana mamlaka yote hutoka kwa Mungu; nao wenye mamlaka wamewekwa na Mungu.
2 Anayepinga mamlaka ya viongozi anapinga agizo la Mungu;
nao wafanyao hivyo wanajiletea hukumu wenyewe,
3 Maana, watawala hawasababishi hofu kwa watu wema, ila kwa
watu wabaya. Basi, wataka usimwogope mtu mwenye mamlaka? Fanya mema naye
atakusifu;
4 maana yeye ni mtumishi wa Mungu anayefanya kazi kwa faida
yako. Lakini ukifanya mabaya, basi, huna budi kumwogopa, maana anao kweli uwezo
wa kutoa adhabu. Yeye ni mtumishi wa Mungu na huitekeleza ghadhabu ya Mungu
kwao watendao maovu.
5 Kwa hiyo ni lazima kuwatii wenye mamlaka, si tu kwa
sababu ya kuogopa ghadhabu ya Mungu, bali pia kwa sababu dhamiri inadai hivyo.
6 Kwa sababu hiyohiyo ninyi hulipa kodi; maana viongozi hao
humtumikia Mungu ikiwa wanatimiza wajibu wao.
7 Mpeni kila mtu haki yake; mtu wa ushuru, ushuru; wa kodi,
kodi; na astahiliye heshima, heshima.
8 Msiwe na deni kwa mtu yeyote, isipokuwa tu deni la
kupendana. Ampendaye jirani yake ameitekeleza Sheria.
9 Maana, amri hizi: "Usizini; Usiue; Usitamani;"
na nyingine zote, zimo katika amri hii moja: "Mpende jirani yako kama
unavyojipenda mwenyewe."
10 Ampendaye jirani yake hamtendei vibaya. Basi, kwa
mapendo Sheria yote hutimizwa.
11 Zaidi ya hayo, ninyi mnajua tumo katika wakati gani: sasa
ndio wakati wa kuamka usingizini; naam, wokovu wetu u karibu zaidi sasa kuliko
wakati ule tulipoanza kuamini.
12 Usiku unakwisha na mchana unakaribia. Basi, tutupilie
mbali mambo yote ya giza, tukajitwalie silaha za mwanga.
13 Mwenendo wetu uwe wa adabu kama inavyostahili wakati wa
mchana; tusiwe na ulafi na ulevi, uchafu na uasherati, ugomvi na wivu.
14 Bwana Yesu Kristo awe vazi lenu; msishughulikie tena
tamaa zenu za maumbile na kuziridhisha.
|