Chapter 14
1 Mkaribisheni kwenu mtu aliye dhaifu, lakini msibishane
naye juu ya mawazo yake binafsi.
2 Watu huhitilafiana: mmoja imani yake inamruhusu kula kila
kitu; lakini mwingine ambaye imani yake ni dhaifu, hula tu mboga za majani.
3 Mtu ambaye hula kila kitu asimdharau yule ambaye hawezi
kula kila kitu; naye ambaye hula tu mboga za majani asimhukumu anayekula kila
kitu, maana Mungu amemkubali.
4 Wewe ni nani hata uthubutu kumhukumu mtumishi wa
mwingine? Akisimama au akianguka ni shauri la Bwana wake; naam, atasimama
imara, maana Bwana anaweza kumsimamisha.
5 Mtu anaweza kufikiria siku fulani kuwa ya maana zaidi
kuliko nyingine; mtu mwingine aweza kuzifikiria siku zote kuwa sawa. Kila mmoja
na afuate msimamo wa akili yake.
6 Anayeadhimisha siku fulani anaadhimisha siku hiyo kwa
ajili ya kumtukuza Mungu; naye anayekula chakula fulani anafanya hivyo kwa kumtukuza
Bwana maana anamshukuru Mungu. Kadhalika naye anayeacha kula chakula fulani
anafanya hivyo kwa ajili ya kumtukuza Bwana, naye pia anamshukuru Mungu.
7 Maana hakuna mtu yeyote miongoni mwetu aishiye kwa ajili yake
mwenyewe, wala hakuna anayekufa kwa ajili yake mwenyewe
8 maana tukiishi twaishi kwa ajili ya Bwana; tukifa,
tunakufa kwa ajili ya Bwana. Basi, kama tukiishi au tukifa, sisi ni mali yake
Bwana.
9 Maana Kristo alikufa, akafufuka ili wapate kuwa Bwana wa
wazima na wafu.
10 Kwa nini, basi wewe wamhukumu ndugu yako? Nawe, kwa nini
wamdharau ndugu yako? Sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu.
11 Maana Maandiko yanasema: "Kama niishivyo, asema
Bwana kila mtu atanipigia magoti, na kila mmoja atakiri kwamba mimi ni
Mungu."
12 Kwa hiyo, kila mmoja wetu atatoa hoja yake mbele ya
Mungu.
13 Basi, tuache kuhukumiana, bali tuazimie kutokuwa kamwe
kikwazo kwa ndugu yetu au kumsababisha aanguke katika dhambi.
14 Katika kuungana na Bwana Yesu, nina hakika kwamba hakuna
kitu chochote kilicho najisi kwa asili yake; lakini, mtu akidhani kwamba kitu
fulani ni najisi, basi, kwake huwa najisi.
15 Kama ukimhuzunisha ndugu yako kwa sababu ya chakula
unachokula, basi mwenendo wako hauongozwi na mapendo. Usikubali hata kidogo
chakula chako kiwe sababu ya kupotea kwa mtu mwingine ambaye Kristo alikufa kwa
ajili yake!
16 Basi, msikubalie kitu mnachokiona kuwa kwenu ni kitu
chema kidharauliwe.
17 Maana Utawala wa Mungu si shauri la kula na kunywa, bali
unahusika na kuwa na uadilifu, amani na furaha iletwayo na Roho Mtakatifu.
18 Anayemtumikia Kristo namna hiyo humpendeza Mungu, na
kukubaliwa na watu.
19 Kwa hiyo tuyazingatie daima mambo yenye kuleta amani, na
yanayotusaidia kujengana.
20 Basi, usiiharibu kazi ya Mungu kwa sababu ya ubishi juu
ya chakula. Vyakula vyote ni halali, lakini haifai kula chakula ambacho
kitamfanya mtu aanguke katika dhambi.
21 Afadhali kuacha kula nyama, kunywa divai, au kufanya
chochote ambacho chaweza kumsababisha ndugu yako aanguke.
22 Basi, shikilia unachoamini kati yako na Mungu wako. Heri
mtu yule ambaye, katika kujiamulia la kufanya, haipingi dhamiri yake.
23 Lakini mtu anayeona shaka juu ya chakula anachokula,
anahukumiwa kama akila, kwa sababu msimamo wa kitendo chake haumo katika imani.
Na, chochote kisicho na msingi wake katika imani ni dhambi.
|