1 Corinthians
Chapter 1
1 Mimi Paulo, niliyeitwa kuwa mtume wa Kristo Yesu kwa
mapenzi ya Mungu, na ndugu Sosthene,
2 tunawaandikia ninyi mlio kanisa la Mungu huko Korintho.
Ninyi mmefanywa watakatifu katika kuungana na Kristo Yesu, mkaitwa muwe watu wa
Mungu, pamoja na watu wote popote wanaomwomba Bwana wetu Yesu Kristo aliye
Bwana wao na wetu pia.
3 Nawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na
Bwana wetu Yesu Kristo.
4 Ninamshukuru Mungu wangu daima kwa ajili yenu kwa sababu
amewatunukia ninyi neema yake kwa njia ya Kristo Yesu.
5 Maana, kwa kuungana na Kristo mmetajirishwa katika kila
kitu. Mmejaliwa elimu yote na uwezo wote wa kuhubiri,
6 kwani, ujumbe juu ya Kristo umethibitishwa ndani yenu,
7 hata hampungukiwi kipaji chochote cha kiroho mkiwa
mnangojea kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo.
8 Yeye atawaimarisha ninyi mpaka mwisho mpate kuonekana
bila hatia Siku ile ya Bwana wetu Yesu Kristo.
9 Mungu ni mwaminifu; yeye aliwaita ninyi muwe na umoja na
Mwanae Yesu Kristo Bwana wetu.
10 Ndugu, ninawasihi kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo:
pataneni nyote katika kila jambo msemalo; yasiweko mafarakano kati yenu; muwe
na fikira moja na nia moja.
11 Ndugu zangu, habari nilizopata kutoka kwa watu kadhaa wa
jamaa ya Kloe, zaonyesha wazi kwamba kuna kutoelewana kati yenu.
12 Nataka kusema hivi: kila mmoja anasema chake: mmoja
husema, "Mimi ni wa Paulo," mwingine: "Mimi ni wa Apolo,"
mwingine: "Mimi ni wa Kefa," na mwingine: "Mimi ni wa
Kristo,".
13 Je, Kristo
amegawanyika? Je, Paulo ndiye aliyesulubiwa kwa ajili yenu? Au je, mlibatizwa
kwa jina la Paulo?
14 Namshukuru
Mungu kwamba sikumbatiza mtu yeyote miongoni mwenu isipokuwa tu Krispo na Gayo.
15 Kwa hiyo
hakuna awezaye kusema amebatizwa kwa jina langu.
16 Samahani,
nilibatiza pia jamaa ya Stefana; lakini zaidi ya hawa, sidhani kama nilimbatiza
mtu mwingine yeyote.)
17 Kristo
hakunituma kubatiza, bali kuhubiri Habari Njema; tena, niihubiri bila kutegemea
maarifa ya hotuba za watu kusudi nguvu ya kifo cha Kristo msalabani
isibatilishwe.
18 Maana ujumbe
kuhusu kifo cha Kristo msalabani ni jambo la kipumbavu kwa wale walio katika
mkumbo wa kupotea, lakini kwetu sisi tulio katika njia ya wokovu ujumbe huo ni
nguvu ya Mungu.
19 Maana
Maandiko Matakatifu yasema: "Nitaiharibu hekima yao wenye hekima, na elimu
ya wataalamu nitaitupilia mbali."
20 Yu wapi basi,
mwenye hekima? Yu wapi basi, mwalimu wa Sheria? Naye bingwa wa mabishano wa
nyakati hizi yuko wapi? Mungu ameifanya hekima ya ulimwengu kuwa upumbavu.
21 Maana, kadiri
ya hekima ya Mungu, watu hawawezi kumjua Mungu kwa njia ya hekima yao wenyewe. Badala
yake, Mungu amependa kuwaokoa wale wanaoamini kwa njia ya kile ambacho wenye
hekima wanakiona kuwa ni upumbavu, yaani ujumbe tunaohubiri.
22 Wayahudi
wanataka ishara, na Wagiriki wanatafuta hekima;
23 lakini sisi
tunamhubiri Kristo aliyesulubiwa. Kwa Wayahudi jambo hili ni kikwazo, na kwa
watu wa mataifa ni upumbavu;
24 lakini kwa
wale walioitwa, Wayahudi kwa Wagiriki, Kristo ni nguvu ya Mungu na hekima ya
Mungu.
25 Maana
kinachoonekana kuwa ni upumbavu wa Mungu, kina busara zaidi kuliko hekima ya
binadamu; na kinachoonekana kuwa ni udhaifu wa Mungu, kina nguvu zaidi kuliko
nguvu za binadamu.
26 Ndugu,
kumbukeni wakati mlipoitwa: wengi wenu hawakuwa wenye hekima hata kwa fikira za
binadamu; wengi hawakuwa wenye nguvu au watu wa tabaka ya juu.
27 Ndiyo kusema,
Mungu aliyachagua yale ambayo ulimwengu huyaona ni upumbavu, ili awaaibishe
wenye hekima; na aliyachagua yale ambayo ulimwengu huyaona ni dhaifu, ili
awaaibishe wenye nguvu.
28 Mungu
ameyachagua yale ambayo kwa fikira za dunia ni mambo yaliyo duni na
yanayodharauliwa, mambo ambayo hata hayakuwako, ili kwa hayo ayafutilie mbali
yale ambayo kwa fikira za binadamu ni mambo ya maana.
29 Basi, hakuna
mtu awezaye kujivunia chochote mbele ya Mungu.
30 Mungu
mwenyewe ndiye aliyewaunganisha ninyi na Kristo Yesu. Mungu amemfanya Kristo
awe hekima yetu; kwa njia yake sisi tunapatanishwa na Mungu, tunakuwa watu wake
Mungu na kukombolewa.
31 Basi, kama
yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Mwenye kutaka kujivuna, basi, na ajivunie
kazi ya Bwana."
|