Chapter 2
1 Ndugu, mimi
nilipokuja kwenu sikuwahubiria siri ya ujumbe wa Mungu kwa ufasaha wa lugha, au
kwa hekima ya binadamu.
2 Nilipokuwa
kwenu niliamua kutojua chochote kile isipokuwa tu kumjua Yesu Kristo; naam,
Kristo aliyesulubiwa.
3 Nilipokuwa
kwenu nilikuwa dhaifu, natetemeka kwa hofu nyingi.
4 Hotuba zangu
na mahubiri yangu sikuyatoa kwa maneno ya kuvutia na ya hekima, bali kwa
uthibitisho mwingi na nguvu ya Roho.
5 Nilifanya
hivyo kusudi imani yenu ipate kutegemea nguvu ya Mungu, na si hekima ya
binadamu.
6 Hata hivyo,
sisi tunatumia lugha ya hekima kwa wale waliokomaa kiroho; lakini hekima hiyo
si ya hapa duniani, wala si ya watawala wa dunia hii ambao wako katika mkumbo
wa kupotea.
7 Hekima
tunayotumia ni hekima ya siri ya Mungu, hekima iliyofichika, ambayo Mungu
aliiazimia tangu mwanzo kwa ajili ya utukufu wetu.
8 Ni hekima
ambayo watawala wa dunia hii hawakuielewa; maana wangalielewa,
hawangalimsulubisha Bwana wa utukufu.
9 Lakini, ni
kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Mambo ambayo jicho halijapata kuyaona
wala sikio kuyasikia, mambo ambayo binadamu hajapata kuyafikiria moyoni, hayo
ndiyo Mungu aliyowatayarishia wale wampendao."
10 Hayo ndiyo
mambo Mungu aliyotufunulia kwa njia ya Roho wake. Maana Roho huchunguza kila
kitu hata mambo ya ndani kabisa ya Mungu.
11 Nani awezaye
kujua mambo ya ndani ya mtu isipokuwa roho yake mtu huyo? Hali kadhalika,
hakuna ajuaye mambo ya Mungu isipokuwa Roho wa Mungu.
12 Sasa sisi
hatukuipokea roho ya ulimwengu, bali tumepokea Roho atokaye kwa Mungu ili
atuwezeshe kujua yale tuliyojaliwa na Mungu.
13 Basi sisi twafundisha,
si kwa maneno tuliyofundishwa kwa hekima ya binadamu, bali kwa maneno
tuliyofundishwa na Roho, tukifafanua mambo ya kiroho kwa walio na huyo Roho.
14 Mtu wa
kidunia hapokei mambo ya Roho wa Mungu. Kwake mtu huyo mambo hayo ni upumbavu
mtupu; yanapita akili yake; maana yanaweza tu kutambuliwa kwa msaada wa Roho.
15 Lakini mtu
aliye na huyo Roho anaweza kubainisha ubora wa kila kitu, naye mwenyewe
hahukumiwi na mtu mwingine.
16 Maandiko
yasema: "Nani awezaye kuifahamu akili ya Bwana? Nani awezaye
kumshauri?" Lakini sisi tunayo akili ya Kristo.
|