Chapter 3
1 Ndugu, mimi
sikuweza kusema nanyi kama watu mlio na huyo Roho. Nilipaswa kusema nanyi kama
watu wa kidunia, kama watoto wachanga katika maisha ya Kikristo.
2 Ilinibidi
kuwalisheni kwa maziwa, na si kwa chakula kigumu, kwani hamkuwa tayari
kukipokea. Hata sasa hamko tayari.
3 Maana bado mu
watu wa kidunia. Je, si kweli kwamba bado uko wivu na magombano kati yenu?
Mambo hayo yanaonyesha wazi kwamba ninyi bado ni watu wa kidunia, mnaishi
mtindo wa kidunia.
4 Mmoja wenu
anaposema, "Mimi ni wa Paulo", na mwingine, "Mimi ni wa
Apolo", je, hiyo haionyeshi kwamba mnaishi bado kama watu wa dunia hii tu?
5 Apolo ni nani? na Paulo ni nani? Sisi ni watumishi tu
ambao tuliwaleteeni ninyi imani. Kila mmoja wetu anafanya kazi aliyopewa na
Bwana.
6 Mimi nilipanda mbegu, Apolo akamwagilia maji; lakini
aliyeiotesha mbegu ni Mungu.
7 Wa maana si yule aliyepanda mbegu, au yule aliyemwagilia
maji; wa maana ni Mungu aliyeiwezesha mbegu kuota.
8 Yule aliyepanda na yule aliyemwagilia maji wote ni sawa,
ingawa kila mmoja atapokea tuzo lake kufuatana na jitihada yake mwenyewe.
9 Maana sisi ni ndugu, wafanyakazi pamoja na Mungu; na
ninyi ni shamba lake; ninyi ni jengo lake.
10 Kwa msaada wa neema aliyonipa Mungu, nimefaulu, kama
mwashi stadi mwenye busara, kuweka msingi ambao juu yake mtu mwingine anajenga.
Basi, kila mmoja awe mwangalifu jinsi anavyojenga juu yake.
11 Hakuna mtu awezaye kuweka msingi mwingine badala ya ule
uliokwisha wekwa, yaani Yesu Kristo.
12 Juu ya msingi huo mtu anaweza kujenga kwa dhahabu, fedha
au mawe ya thamani; anaweza kutumia miti, majani au nyasi.
13 Iwe iwavyo, ubora wa kazi ya kila mmoja utaonekana
wakati Siku ile ya Kristo itakapoifichua. Maana, Siku hiyo itatokea na moto, na huo moto utaipima na kuonyesha
ubora wake.
14 Ikiwa
alichojenga mtu juu ya huo msingi kitaustahimili huo moto, atapokea tuzo;
15 lakini
kama alichojenga kitaunguzwa, basi, atapoteza tuzo lake; lakini yeye mwenyewe
ataokolewa kana kwamba ameponyoka kutoka motoni.
16 Je,
hamjui kwamba ninyi ni hekalu la Mungu, na kwamba Roho wa Mungu anakaa ndani
yenu?
17 Basi,
mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu; maana hekalu la Mungu ni
takatifu, na hekalu hilo ni ninyi wenyewe.
18
Msijidanganye! Mtu yeyote miongoni mwenu akijidhania mwenye hekima mtindo wa
kidunia, heri awe mjinga kusudi apate kuwa na hekima ya kweli.
19 Maana,
hekima ya kidunia ni upumbavu mbele ya Mungu. Kwani Maandiko Matakatifu yasema:
"Mungu huwanasa wenye hekima katika ujanja wao."
20 Na
tena: "Bwana ajua kwamba mawazo ya wenye hekima hayafai."
21 Basi,
mtu asijivunie watu. Maana kila kitu ni chenu.
22 Paulo,
Apolo na Kefa, ulimwengu, maisha na kifo; mambo ya sasa na ya baadaye, yote ni
yenu.
23 Lakini
ninyi ni wa Kristo naye Kristo ni wa Mungu.
|