Chapter 6
1
Anathubutuje mmoja wenu kumshtaki ndugu muumini mbele ya mahakama ya watu
wasiomjua Mungu badala ya kumshtaki mbele ya watu wa Mungu?
2 Je,
hamjui kwamba watu wa Mungu watauhukumu ulimwengu? Ikiwa basi, ulimwengu
utahukumiwa nanyi, kwa nini hamstahili kuhukumu hata katika mambo madogo?
3 Je,
hamjui kwamba, licha ya kuhukumu mambo ya kawaida ya kila siku, tutawahukumu
hata malaika?
4
Mnapokuwa na mizozo juu ya mambo ya kawaida, je, mnawaita wawe mahakimu watu
ambao hata hawalijali kanisa?
5 Aibu kwenu!
Ndiyo kusema hakuna hata mmoja miongoni mwenu mwenye hekima kiasi cha kuweza
kutatua tatizo kati ya ndugu waumini?
6 Badala
yake, kweli imekuwa mtindo ndugu kumpeleka ndugu yake mahakamani, tena mbele ya
mahakimu wasioamini.
7 Kwa
kweli huko kushtakiana tu wenyewe kwa wenyewe kwabainisha kwamba mmeshindwa
kabisa! Je, haingekuwa jambo bora zaidi kwenu kudhulumiwa! Haingekuwa bora
zaidi kwenu kunyang`anywa mali yenu?
8 Lakini,
badala yake, ninyi ndio mnaodhulumu na kunyang`anya; tena, hayo mnawafanyia
ndugu zenu!
9 Au je,
hamjui kwamba watu wabaya hawataurithi Utawala wa Mungu? Msijidanganye! Watu
wanaoishi maisha ya uasherati, wanaoabudu sanamu, wazinzi, au walawiti,
10 wevi,
wachoyo, walevi, wasengenyaji, wanyang`anyi, hao wote hawatashiriki Utawala wa
Mungu.
11 Baadhi
yenu mlikuwa hivyo; lakini sasa mmeoshwa, mkafanywa watakatifu, na kupatanishwa
na Mungu kwa jina la Bwana Yesu Kristo na kwa Roho wa Mungu wetu.
12 Mtu
anaweza kusema: "Kwangu mimi kila kitu ni halali." Sawa; lakini si
kila kitu kinafaa. Nakubali kwamba kila kitu ni halali kwangu lakini sitaki
kutawaliwa na kitu chochote.
13 Unaweza
kusema: "Chakula ni kwa ajili ya tumbo, na tumbo ni kwa ajili ya
chakula." Sawa; lakini Mungu ataviharibu vyote viwili. Mwili wa mtu si kwa
ajili ya uzinzi bali ni kwa ajili ya kumtumikia Bwana, naye Bwana ni kwa ajili
ya mwili.
14 Basi,
Mungu aliyemfufua Bwana kutoka wafu atatufufua nasi pia kwa nguvu yake.
15 Je,
hamjui kwamba miili yenu ni viungo vya mwili wa Kristo? Je, mnadhani naweza
kuchukua sehemu ya mwili wa Kristo na kuifanya kuwa sehemu ya mwili wa kahaba?
Hata kidogo!
16 Maana,
kama mjuavyo, anayeungana na kahaba huwa mwili mmoja naye - kama ilivyoandikwa:
"Nao wawili watakuwa mwili mmoja."
17 Lakini
aliyejiunga na Bwana huwa roho moja naye.
18
Jiepusheni kabisa na uzinzi. Dhambi nyingine zote hutendwa nje ya mwili lakini
mzinzi hutenda dhambi dhidi ya mwili wake mwenyewe.
19 Je,
hamjui kwamba miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, ambaye
mlimpokea kutoka kwa Mungu? Ninyi basi, si mali yenu wenyewe.
20
Mlinunuliwa kwa bei kubwa. Kwa hiyo, itumieni miili yenu kwa ajili ya kumtukuza
Mungu.
|