Chapter 8
1 Yahusu
sasa vyakula vilivyotambikiwa sanamu: Tunajua kwamba sisi sote tuna ujuzi,
lakini ujuzi huo huwafanya watu wawe na majivuno; lakini mapendo hujenga.
2
Anayefikiri kwamba anajua kitu, kwa kweli hajui chochote kama inavyompasa.
3 Lakini
anayempenda Mungu huyo anajulikana naye.
4 Kwa
hiyo, kuhusu vyakula vilivyotambikiwa sanamu, twajua kwamba sanamu si kitu
duniani; twajua kwamba Mungu ni mmoja tu.
5 Hata
kama viko vitu viitwavyo miungu duniani au mbinguni, na hata kama wako miungu
na mabwana wengi,
6 hata
hivyo, kwetu sisi yuko Mungu mmoja tu: Baba, Muumba wa vyote, ambaye kwa ajili
yake sisi tuko. Pia yuko Bwana mmoja tu, Yesu Kristo, ambaye kwa njia yake vitu
vyote viliumbwa, na sisi twaishi kwa njia yake.
7 Lakini, si kila mtu anao ujuzi huu. Maana wako watu
wengine waliokwisha zoea sanamu, watu ambao mpaka hivi sasa wanapokula vyakula
huviona bado kama vyakula vilivyotambikiwa sanamu. Na kwa vile dhamiri zao ni
dhaifu, hutiwa unajisi.
8 Lakini chakula hakiwezi kutupeleka karibu zaidi na Mungu.
Tukiacha kukila hatupungukiwi kitu, tukikila hatuongezewi kitu.
9 Lakini, jihadharini: huu uhuru wenu usiwafanye walio na
imani dhaifu waanguke katika dhambi.
10 Maana, mtu ambaye dhamiri yake ni dhaifu, akikuona wewe
mwenye ujuzi unakula vyakula hivyo ndani ya hekalu la sanamu, je, hatatiwa moyo
wa kula vyakula vilivyotambikiwa sanamu?
11 Hivyo, huyo ndugu yako dhaifu ambaye Kristo alikufa kwa
ajili yake, atapotea kwa sababu ya ujuzi wako.
12 Kama mkiwakosesha ndugu zenu jinsi hiyo na kuzijeruhi
dhamiri zao dhaifu, mtakuwa mmemkosea Kristo.
13 Kwa hiyo, ikiwa chakula husababisha kuanguka kwa ndugu
yangu, sitakula nyama kamwe, nisije nikamfanya ndugu yangu aanguke katika
dhambi.
|