Chapter 10
1 Ndugu, nataka
mjue kwamba babu zetu wote walikuwa chini ya ulinzi wa lile wingu, na kwamba
wote walivuka salama ile bahari.
2 Wote
walibatizwa katika umoja na Mose kwa lile wingu na ile bahari.
3 Wote
walikula chakula kilekile cha kiroho,
4 wakanywa
pia kinywaji kilekile cha kiroho, maana walikunywa kutoka ule mwamba wa kiroho
uliowafuata; mwamba huo ulikuwa Kristo mwenyewe.
5 Hata
hivyo, wengi wao hawakumpendeza Mungu, na maiti zao zilisambazwa jangwani.
6 Sasa,
mambo hayo yote ni mfano tu kwetu; yanatuonya sisi tusitamani ubaya kama wao
walivyotamani.
7 Msiwe
waabudu sanamu kama baadhi yao walivyokuwa; kama yasemavyo Maandiko: "Watu
waliketi kula na kunywa, wakasimama kucheza."
8 Wala
tusizini kama baadhi yao walivyozini, wakaangamia siku moja watu ishirini na
tatu elfu.
9
Tusimjaribu Bwana kama baadhi yao walivyomjaribu, wakauawa na nyoka.
10 Wala
msinung`unike kama baadhi yao walivyonung`unika, wakaangamizwa na Mwangamizi!
11 Basi,
mambo hayo yaliyowapata wao ni kielelezo kwa wengine, na yaliandikwa ili
kutuonya sisi, ambao mwisho wa nyakati unatukabili.
12
Anayedhani amesimama imara ajihadhari asianguke.
13
Majaribu mliyokwisha pata ni ya kawaida kwa binadamu. Mungu ni mwaminifu, naye
hataruhusu mjaribiwe kupita nguvu zenu, ila pamoja na majaribu, yeye atawapeni
pia nguvu ya kustahimili na njia ya kutoka humo salama.
14 Kwa
hiyo, wapenzi wangu, epeni ibada za sanamu.
15 Naongea
nanyi, watu wenye busara; jiamulieni wenyewe hayo nisemayo.
16
Tunapomshukuru Mungu kwa kikombe kile cha baraka, je, huwa hatushiriki damu ya
Kristo? Na tunapoumega mkate, je, huwa hatushiriki mwili wa Kristo?
17 Kwa
kuwa mkate huo ni mmoja, sisi, ingawa ni wengi, tu mwili mmoja; maana sote
twashiriki mkate huohuo.
18
Chukueni, kwa mfano, Wayahudi wenyewe: kwao, wenye kula vilivyotambikiwa
madhabahuni waliungana na hiyo madhabahu.
19 Nataka kusema nini, basi? Kwamba chakula
kilichotambikiwa sanamu ni kitu zaidi ya chakula? Na hizo sanamu, je, ni kitu
kweli zaidi ya sanamu?
20 Hata kidogo! Ninachosema ni kwamba tambiko wanazotoa
watu wasiomjua Mungu wanawatolea pepo, sio Mungu. Sipendi kamwe ninyi muwe na
ushirika na pepo.
21 Hamwezi kunywa kikombe cha Bwana na kikombe cha pepo;
hamwezi kushiriki katika meza ya Bwana na katika meza ya pepo.
22 Au je, tunataka kumfanya Bwana awe na wivu? Mnadhani
tuna nguvu zaidi kuliko yeye?
23 Vitu vyote ni halali, lakini si vyote vinafaa. Vitu
vyote ni halali lakini si vyote vinajenga.
24 Mtu asitafute faida yake mwenyewe, ila faida ya
mwenzake.
25 Kuleni chochote kile kiuzwacho sokoni bila ya
kuulizauliza kwa sababu ya dhamiri zenu;
26 maana Maandiko yasema: "Dunia na vyote vilivyomo ni
mali ya Bwana."
27 Kama mtu ambaye si muumini akiwaalikeni nanyi mkakubali
kwenda, basi, kuleni vyote atakavyowaandalieni bila kuulizauliza kwa sababu ya
dhamiri zenu.
28 Lakini mtu akiwaambieni: "Chakula hiki kimetambikiwa
sanamu," basi, kwa ajili ya huyo aliyewaambieni hivyo na kwa ajili ya
dhamiri, msile.
29 Nasema, "kwa ajili ya dhamiri," si dhamiri
yenu, bali dhamiri yake huyo aliyewaambieni. Mtaniuliza: "Kwa nini uhuru
wangu utegemee dhamiri ya mtu mwingine?
30 Ikiwa mimi nashiriki chakula hicho huku namshukuru
Mungu, kwa nini nilaumiwe kwa chakula ambacho kwa ajili yake nimemshukuru
Mungu?"
31 Basi, chochote mfanyacho iwe ni kula au kunywa, fanyeni
yote kwa ajili ya utukufu wa Mungu.
32 Msiwe kikwazo kwa Wayahudi au kwa Wagiriki au kwa kanisa
la Mungu.
33 Muwe kama mimi; najaribu kuwapendeza wote kwa kila njia,
bila kutafuta faida yangu mwenyewe ila faida ya wote, wapate kuokolewa.
|