Chapter 12
1 Ndugu, kuhusu vipaji vya kiroho, napenda mfahamu vizuri
mambo haya:
2 Mnajua kwamba, kabla ya kuongoka kwenu, mlitawaliwa na
kupotoshwa na sanamu tupu.
3 Basi, jueni kwamba mtu yeyote anayeongozwa na Roho wa
Mungu hawezi kusema: "Yesu alaaniwe!" Hali kadhalika, mtu yeyote
hawezi kusema: "Yesu ni Bwana," asipoongozwa na Roho Mtakatifu.
4 Vipaji vya kiroho ni vya namna nyingi, lakini Roho
avitoaye ni mmoja.
5 Kuna namna nyingi za kutumikia, lakini Bwana
anayetumikiwa ni mmoja.
6 Kuna namna mbalimbali za kufanya kazi ya huduma, lakini
Mungu ni mmoja, anayewezesha kazi zote katika wote.
7 Kila mtu hupewa mwangaza wa Roho kwa faida ya wote.
8 Roho humpa mmoja ujumbe wa hekima, na mwingine ujumbe wa
elimu apendavyo Roho huyohuyo.
9 Roho huyohuyo humpa mmoja imani, na humpa mwingine kipaji
cha kuponya;
10 humpa mmoja kipaji cha kufanya miujiza, mwingine kipaji
cha kusema ujumbe wa Mungu, mwingine kipaji cha kubainisha vipaji vitokavyo kwa
Roho na visivyo vya Roho; humpa mmoja kipaji cha kusema lugha ngeni, na
mwingine kipaji cha kuzifafanua.
11 Hizo zote ni kazi za Roho huyohuyo mmoja, ambaye humpa
kila mtu kipaji tofauti, kama apendavyo mwenyewe.
12 Kama vile mwili ulivyo mmoja wenye viungo vingi, na
viungo hivyo vyote-ingawaje ni vingi - hufanya mwili mmoja, ndivyo ilivyo pia
kwa Kristo.
13 Maana sisi, tukiwa Wayahudi au watu wa mataifa mengine,
watumwa au watu huru, sote tumebatizwa kwa Roho mmoja katika mwili huo mmoja;
na sote tukanyweshwa Roho huyo mmoja.
14 Mwili hauna kiungo kimoja tu, bali una viungo vingi.
15 Kama mguu ungejisemea: "Kwa kuwa mimi si mkono,
basi mimi si mali ya mwili", je, ungekoma kuwa sehemu ya mwili? La hasha!
16 Kama sikio lingejisemea: "Kwa vile mimi si jicho,
basi mimi si mali ya mwili", je, kwa hoja hiyo lingekoma kuwa sehemu ya
mwili? La!
17 Kama mwili wote ungekuwa jicho, sikio lingekuwa wapi? Na
kama mwili wote ungekuwa sikio, mtu angewezaje kunusa?
18 Lakini kama ilivyo, Mungu alizipanga sehemu hizo tofauti
katika mwili kama alivyopenda.
19 Kama sehemu zote zingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa
wapi?
20 Ukweli ni kwamba, sehemu za mwili ni nyingi, lakini
mwili ni mmoja.
21 Basi, jicho haliwezi kuuambia mkono: "Sikuhitaji
wewe", wala kichwa hakiwezi kuiambia miguu: "Siwahitaji ninyi."
22 Zaidi ya hayo, inaonekana kwamba sehemu zile za mwili
zinazoonekana kuwa ni dhaifu ndizo zilizo muhimu zaidi.
23 Tena, viungo vile tunavyovifikiria kuwa havistahili
heshima kubwa, ndivyo tunavyovitunza kwa uangalifu zaidi; viungo vya mwili
ambavyo havionekani kuwa vizuri sana, huhifadhiwa zaidi,
24 ambapo viungo vingine havihitaji kushughulikiwa. Mungu
mwenyewe ameuweka mwili katika mpango, akakipa heshima zaidi kiungo kile
kilichopungukiwa heshima,
25 ili kusiweko na utengano katika mwili bali viungo vyote
vishughulikiane.
26 Kama kiungo kimoja kinaumia viungo vyote huumia pamoja
nacho. Kiungo kimoja kikisifiwa viungo vingine vyote hufurahi pamoja nacho.
27 Basi, ninyi nyote ni mwili wa Kristo; kila mmoja wenu ni
kiungo cha mwili huo.
28 Mungu ameweka katika kanisa: kwanza mitume, pili
manabii, tatu walimu; kisha ameweka wale wenye kipaji cha kufanya miujiza,
kuponya, kusaidia; viongozi na wenye kusema lugha ngeni.
29 Je, wote ni
mitume? Wote ni manabii? Wote ni walimu? Wote ni wenye kipaji cha kufanya miujiza?
30 Je, wote ni
wenye kipaji cha kuponya? Wote ni wenye kipaji cha kusema lugha ngeni? Je, wote
hufafanua lugha?
31 Muwe basi, na
tamaa ya kupata vipaji muhimu zaidi. Nami sasa nitawaonyesheni njia bora zaidi
kuliko hizi zote.
|