Chapter 13
1 Hata kama
nikinena lugha za watu na hata za malaika, lakini kama sina upendo mimi
nimekuwa tu kama sauti ya debe tupu au kengele.
2 Tena, naweza
kuwa na kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, nikafahamu siri zote na kujua
kila kitu; naweza kuwa na imani yote hata nikaweza kuihamisha milima, lakini
kama sina upendo mimi si kitu.
3 Nikitoa mali
yangu yote na kuwapa maskini, na tena nikiutoa mwili wangu uchomwe, kama sina
upendo hiyo hainifai chochote.
4 Mwenye upendo
huvumilia, hufadhili; mwenye upendo hana wivu, hajidai, wala hajivuni.
5 Mwenye upendo
hakosi adabu, hatafuti faida yake binafsi, wala hana wepesi wa hasira; haweki
kumbukumbu ya mabaya,
6 hafurahii
uovu, bali hufurahia ukweli.
7 Mwenye upendo
huvumilia yote, huamini yote, na hustahimili yote.
8 Upendo hauna kikomo
kamwe. Kama kuna vipaji vya kutangaza ujumbe wa Mungu, hivyo vitatoweka siku
moja; kama ni vipaji vya kusema lugha ngeni, vitakoma; kama kuna elimu, nayo
itapita.
9 Maana ujuzi
wetu si kamili, na kipaji chetu cha kutangaza neno la Mungu si kamili.
10 Lakini kile
kilicho kikamilifu kitakapofika, vyote visivyo vikamilifu vitatoweka.
11 Nilipokuwa
mtoto mchanga nilisema kitoto, nilifahamu kitoto, nilifikiri kitoto. Lakini
sasa, maadam mimi ni mtu mzima, mambo ya kitoto nimeyaacha.
12 Tunachoona
sasa ni kama tu sura hafifu katika kioo, lakini hapo baadaye tutaona uso kwa
uso. Sasa ninajua kiasi fulani tu, lakini hapo baadaye nitajua yote kikamilifu,
kama vile Mungu anavyonijua mimi.
13 Sasa yanadumu
haya matatu: imani, tumaini na upendo; lakini lililo kuu kupita yote ni upendo.
|