Chapter 14
1 Jitahidini
kuwa na upendo. Vilevile fanyeni bidii ya kupata vipaji vingine vya kiroho,
hasa kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu.
2 Mwenye kunena
lugha ngeni hasemi na watu bali anasema na Mungu. Yeye hunena kwa nguvu ya Roho
mambo yaliyofichika.
3 Lakini mwenye
kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, husema na watu kwa ajili ya kuwajenga,
kuwafariji na kuwatia moyo.
4 Mwenye kunena
lugha ngeni anajijenga mwenyewe. Lakini mwenye kipaji cha kutangaza ujumbe wa
Mungu, analijenga kanisa.
5 Basi,
ningependa ninyi nyote mseme kwa lugha ngeni lakini ningependelea hasa muwe na
kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, maana mtu mwenye kipaji cha kutangaza
ujumbe wa Mungu, ni wa maana zaidi kuliko yule mwenye kusema lugha ngeni,
isipokuwa tu kama yupo hapo mtu awezaye kuyafafanua hayo mambo asemayo, ili
kanisa lipate kujengwa.
6 Hivyo, ndugu
zangu, kama nikija kwenu na kusema nanyi kwa lugha ngeni itawafaa nini?
Haitawafaa chochote, isipokuwa tu kama nitawaelezeni ufunuo wa Mungu au ujuzi
fulani au ujumbe wa Mungu au mafundisho fulani.
7 Ndivyo ilivyo
kwa vyombo visivyo na uhai vyenye kutoa sauti kama vile filimbi au kinanda. Je,
mtu anawezaje kuutambua wimbo unaochezwa kama vyombo hivyo havitoi sauti
waziwazi vinapopigwa?
8 La mgambo
likilia bila kufuata taratibu zake, nani atajiweka tayari kwa vita?
9 Hali kadhalika
na ninyi, kama ulimi wenu hausemi kitu chenye kueleweka, nani ataweza kufahamu
mnayosema? Maneno yenu yatapotea hewani.
10 Zipo lugha
mbalimbali ulimwenguni, na hakuna hata mojawapo isiyo na maana.
11 Lakini ikiwa
mimi sifahamu maana ya lugha asemayo mtu fulani, mimi ni mgeni kwake mtu huyo
naye pia ni mgeni kwangu.
12 Hali kadhalika
na ninyi, maadam mna hamu ya kupata vipaji vya Roho, jitahidini hasa kujipatia
vile vinavyosaidia kulijenga kanisa.
13 Kwa hiyo,
mwenye kunena lugha ngeni na aombe apate uwezo wa kuzifafanua.
14 Maana,
nikisali kwa lugha ngeni roho yangu ndiyo inayosali, lakini akili yangu hubaki
bure.
15 Nifanye nini, basi? Nitasali kwa roho yangu, nitasali
pia kwa akili yangu; nitaimba kwa roho yangu, nitaimba pia kwa akili yangu.
16 Ukimsifu Mungu kwa roho yako tu, atawezaje mtu wa
kawaida aliye katika mkutano kuitikia sala yako ya shukrani kwa kusema:
"Amina," kama haelewi unachosema?
17 Sala yako ya shukrani yaweza kweli kuwa bora, lakini
huyo mwingine haitamfaidia.
18 Namshukuru Mungu kwamba mimi nasema kwa lugha ngeni
zaidi kuliko ninyi nyote.
19 Lakini katika mikutano ya waumini napendelea zaidi
kusema maneno matano yenye kueleweka ili niwafundishe wengine, kuliko kusema
maneno elfu ya lugha ngeni.
20 Ndugu, msiwe kama watoto katika fikira zenu. Kuhusu uovu
muwe kama watoto wachanga lakini katika kufikiri ni lazima muwe kama watu
waliokomaa.
21 Imeandikwa katika Sheria: "Bwana asema hivi: `Kwa
njia ya wenye kunena lugha ngeni, na kwa midomo ya wageni, nitasema na watu
hawa, hata hivyo, hawatanisikiliza."`
22 Hivyo basi, kipaji cha kusema lugha ngeni ni ishara, si
kwa ajili ya watu wenye imani, bali kwa ajili ya wale wasioamini; lakini kipaji
cha kutangaza ujumbe wa Mungu ni kwa ajili ya wale wanaoamini na si kwa ajili
ya wasioamini.
23 Basi, kanisa lote linapokutana pamoja, na wote wakaanza
kusema kwa lugha ngeni, kama wakija watu wa kawaida au wasioamini, je,
hawatasema kwamba ninyi mna wazimu?
24 Lakini, wote wakiwa wanautangaza ujumbe wa Mungu, akija
mtu wa kawaida au asiyeamini, yote atakayosikia yatamhakikishia ubaya wake
mwenyewe; yote atakayosikia yatamhukumu.
25 Siri za moyo wake zitafichuliwa, naye atapiga magoti na
kumwabudu Mungu akisema: "Kweli Mungu yupo pamoja nanyi."
26 Ndugu, tuseme nini, basi? Mnapokutana pamoja, mmoja
aimbe wimbo, mwingine atoe mafundisho, mwingine awe na ufunuo kutoka kwa Mungu,
mwingine atumie kipaji cha kusema kwa lugha ngeni na mwingine afafanue
yanayosemwa. Yote yawe kwa ajili ya kulijenga kanisa.
27 Wakiwepo watu wenye vipaji vya kusema kwa lugha ngeni,
waseme wawili au watatu, si zaidi, tena mmojammoja; na aweko mtu wa kufafanua
yanayosemwa.
28 Lakini kama hakuna awezaye kufafanua, basi, mwenye
kusema lugha ngeni anyamaze mkutanoni, aseme na nafsi yake mwenyewe na Mungu.
29 Kuhusu wale wenye kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu,
waseme wawili au watatu, na wengine wayapime maneno yao.
30 Ikiwa mmoja anaposema mwingine wa wasikilizaji amepata
ufunuo kutoka kwa Mungu, basi, yule anayesema anyamaze.
31 Maana nyote mwaweza kutangaza ujumbe wa Mungu, mmoja
baada ya mwingine, ili nyote mpate kujifunza na kutiwa moyo.
32 Kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu ni lazima
kitawaliwe na huyo mwenye hicho kipaji.
33 Maana Mungu si Mungu wa fujo, ila wa amani.
34 Kama ilivyo desturi katika makanisa yote ya watu wa
Mungu, wanawake wakae kimya katika mikutano ya waumini. Hawana ruhusa kusema;
ila wawe watii kama isemavyo Sheria.
35 Ikiwa wanayo maswali ya kuuliza, wawaulize waume zao
nyumbani, maana ni aibu kwa mwanamke kusema katika mikutano ya waumini.
36 Je, mnadhani neno la Mungu limetoka kwenu ninyi au
kwamba limewajieni ninyi peke yenu?
37 Kama mtu yeyote anadhani kwamba yeye ni mjumbe wa Mungu au
kwamba anacho kipaji cha Roho, na ajue kwamba haya ninayowaandikia ninyi ni
amri ya Bwana.
38 Lakini mtu asiyetambua hayo, basi, mtu asimjali mtu
huyo.
39 Hivyo basi, ndugu zangu, mnapaswa kuwa na hamu ya
kutangaza ujumbe wa Mungu; lakini msimkataze mtu kusema kwa lugha ngeni.
40 Lakini yote yafanyike kwa heshima na kwa utaratibu.
|